Friday, December 15, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AAGIZA BENKI ZISIZOKIDHI VIGEZO ZIFUTIWE LESENI

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akihutubia katika mkutano maalum wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, uliofanyika mjini Dodoma ili kujadili masuala ya Mitaji na Mpango wa Kuziunganisha Benki za Wananchi Tanzania.
Washiriki wa mkutano maalum wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo uliofunguliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani), kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Mjini Dodoma.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Benard Kibesse (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Benki za Wananchi –COBAT, Bw. Rukwaro Senkoro, wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), mijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akifurahia jambo na Mbunge wa Mtwara Vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa Ghasia baada ya kufungua mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa Nne kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akibadilishana mawazo na baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioshiriki mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, nje ya Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, Bw. Rukwaro Senkoro, nje ya Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.








Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),(kulia), anaeshughulikia masuala ya kibenki Bw. Kened Nyoni na Kaimu Kamishna Msaidizi Sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Michael Nyagoga (Kushoto) wakifuatalia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (COBAT), uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.


Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT), Bw. Mugwagi Stephen akizungumza katika mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma. Kulia kwake ni Mweyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mhe. Hawa Ghasia na Kushoto kwake ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb).


Mbunge wa Mtwara Vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa Ghasia akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) ili aweze kufungua mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi kwaniaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)


Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania BOT kuzifutia leseni benki zote za biashara pamoja na benki za wananchi zitakazoshindwa kukidhi vigezo vya kuendesha shughuli za kibenki nchini.


Ametoa agizo hilo mjini Dodoma katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati akifungua Mkutano Maalum wa Wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT).


“kwa taarifa niliyonayo hadi sasa baadhi ya benki hazijatimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa kutosha, hali ambayo haiwezi kuachwa iendelea hata kidogo, kwani haiimarishi sekta ya fedha na haiwasaidii wananchi kuendelea kiuchumi” alisema Waziri Kassim Majaliwa katika hotuba hiyo


Alisema Benki Kuu ilitoa muda hadi mwishoni mwa Desemba 2017, benki za wananchi ziweze kuongeza mtaji na kwamba muda huo hautaongezwa na wala Serikali haitatoa mtaji kwa benki hizo.


“Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania haitasita kuifungia benki yoyote na kufuta leseni yake ya biashara pindi itakapobaini inavunja sheria, ikiwa ni pamoja na kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi ambao unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na amana za wateja kama tulivyofanya kwa Mbinga Community Bank PLC kuanzia tarehe 12/5/2017” alisema Dkt. Mpango kwa niaba ya Waziri Mkuu.


Maagizo hayo yamekuja siku moja baada ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango wakati akifungua tawi kuu la Benki ya CRDB mjini Dodoma, kuhakikisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania-BOT, inazifuta benki zote zinazoshindwa kujiendesha kibiashara hata kama zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.


Alisema Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha benki za wananchi zinaimarika zikiwemo kuruhusiwa kuanzisha mifumo ya ushirikiano katika Nyanja ya Mfumo wa Mawasiliano na Habari (ICT), Idara za Ukaguzi wa Ndani (Internal Audit Services), kupunguza wingi wa idara na kuwa na idara tatu (3) tu muhimu, kuruhusiwa kuungana (Federation), ambazo zitapunguza gharama za uendeshaji wa benki za wananchi na kuleta ufanisi katika kutoa huduma.


“Napenda kusisitiza kuwa sekta ya benki ni muhimu sana kwa uhai na ukuaji wa uchumi kama ilivyo damu kwa mwili wa binadamu na kutokana na umuhimu wake huo, sekta hii ni kati ya sekta chache zinazosimamiwa kwa karibu sana ili kulinda amana za wateja pamoja na kuhakikisha uhimilivu wa mfumo mzima wa sekta ya fedha na mwenendo wa uchumi wa Taifa” aliongeza Dkt. Mpango


Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT) Bw. Rukwaro Senkoro, alisema hadi kufikia Juni, 2017, Benki za Wananchi nchini zilikuwa na wateja zaidi ya milioni 1.4, wateja wa vikundi zaidi ya 10,000, Matawi 12, Vituo 59, na wanahisa 66,492.


“Benki hizo zina amana zenye thamani ya shs bilioni 74.2, zimetoa mikopo ya sh. bilioni 56.8, na jumla ya mali zenye thamani ya shs. bilioni 92.3” Alisema Bw. Senkoro


Hata hivyo, kutokana na Utafiti wa Matumizi ya Huduma za Kifedha uliofanyika mwaka 2017 umebaini kuwa asilimia 28 ya wananchi bado hawapati huduma za kifedha hapa nchini hususan vijijini na kutaja changamoto ya ukosefu wa mitaji ya benki hizo kukwaza sekta hiyo. 


Dhana kuu ya mkutano huo wa COBAT uliowashirikisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ni “Mitaji na Mpango wa Kuziunganisha Benki za Wananchi Tanzania”, ambayo ni dhana mpya.

No comments: