Monday, December 18, 2017

Wadau Wa Michezo Jitokezeni kuibua Vipaji Vya Michezo Mikoani-Mhe.Shonza

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza akiongea na wakazi wa Mbeya Vijijini waliohudhuria ufungaji wa Mashindano ya Jimbo Cup (Njeza Cup) jana Vijijini hapo.
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Mhe. Oran Njeza akiongea wakati wa ufungaji wa mashindano ya Jimbo Cup (Njeza Cup) mashindano ambayo ameyaratibu yeye na kushirikisha vijiji takribani 200 na kata 30.
Naibu Waziri wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (Kulia) akimpa mkono wa pongezi kiongozi wa Garant Queens Naomy Mbwili wakati wa ufungaji wa Mashindano ya Jimbo Cup (Njeza Cup) jana Mbeya Vijijini.
Naibu Waziri wa Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (Kulia) akimpa zawadi ya fedha kiasi cha laki Tano kiongozi wa timu ya Ilunga David Costa (Kushoto walioibuka washindi wa pili wa Jimbo Cup (Njeza Cup) jana Mbeya Vijijini.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (Katikati) akiwakabidhi washindi wa kwanza wa timu ya Iyanya Kombe la Jimbo Cup (Njeza Cup) ambapo Inyala iliibuka mshindi wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Ilunga hapo jana Mbeya Vijijini.Picha na Lorietha Laurence-WHUSM


*Na Lorietha Laurence-WHUSM, Mbeya Vijijini*

Naibu Waziri wa Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ametoa wito kwa wadau wa michezo nchini kujitokeza kwa wingi kudhamini mashindano ya michezo kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kutengeneza wachezaji bora watakaowakilisha Taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Mhe. Shonza ameyasema hayo alipokuwa akifunga mashindano ya Jimbo yaliyoandaliwa na Mbunge wa Wilaya hiyo Mhe.Oran Njeza katika Wilaya ya Mbeya Vijijini.“Napenda kuelekeza shukrani zangu za dhati kwa Mbunge wa Mbeya Vijijini Mhe.Njeza kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kuibua vipaji vya mpira wa Miguu” amesema Mhe. Shonza

Aidha, Mhe. Shonza alisema kuwa amefurahishwa zaidi kwa kuona mashindano hayo yameshirikisha watoto wa kike wanaocheza mpira wa miguu.Mhe. Shonza alisema wanambeya wanahaja ya kujivunia vipaji walivyobarikiwa kwa kuwa na wachezaji hodari wa mpira wa miguu, wanariadha, waigizaji na waimbaji wa muziki.

“Kwa hakika Mbeya mmebarikiwa kuwa na vipaji vingi nami naahidi kuwa Wizara yangu itashirikiana kwa karibu na wadau wa michezo kuhakikisha tunafika mbali ” amesema Mhe. Shonza.Pia Naibu Waziri Shonza amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)kufanya ziara katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ili kuibua vipaji vya wachezaji watakaosaidia kuunda timu nzuri ya vijana chini ya miaka 17.

Vilevile Mhe. Shonza aliwataka viongozi wa Wilaya ya Mbeya Vijijini , Maafisa Utamaduni na Michezo kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya viwanja vitakavyokuwa vikutumika kwa ajili ya michezo na sanaa.Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Mhe. Oran Njezi amesema kuwa michezo ni chanzo cha ajira na ujenzi wa afya bora hivyo ni budi kuzingatiwa .

Hata hivyo Mhe. Njezi alieleza kuwa japokuwa mashindano hayo yamefanikisha kukusanya vijiji 200 katika michuano ya awali ukosefu wa wadhamini ndiyo changamoto kubwa walikabiliana nayo pamoja na ukosefu wa viwanja vya mpira.

No comments: