Wachimbaji wa Madini ya Jasi Mkoani Singida wametakiwa kufanya shughuli zao kwa uaminifu ili kujihakikishia soko la uhakika.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa wito huo Desemba 11, 2017 Wilayani Itigi mara baada ya kuzungumza na Wachimbaji wa madini hayo wakati wa ziara yake kwenye maeneo yenye uchimbaji wa madini ya Jasi Mkoani Singida.
Wachimbaji wa Madini hayo walimueleza Naibu Waziri Nyongo changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika.
Mara baada ya wachimbaji hao kuelezea changamoto zinazowakabili, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi, Ali Minja alimueleza Naibu Waziri Nyongo kwamba tatizo la soko la Madini ya Jasi yanayochimbwa Singida linasababishwa na wachimbaji wenyewe kwa kuchanganya madini hayo na udongo.
Alisema wakati mwingine wachimbaji wenyewe wanasababisha kupotea kwa soko, kwani mnunuzi akinunua Madini ya Jasi yaliyochanganywa na udongo hawezi kurudi tena kununua.“Baadhi ya wachimbaji wa Jasi Mkoani hapa sio waaminifu kwani wanachanganya madini na takataka ikiwemo udongo, na hii inakimbiza wanunuzi,” alisema.
Kufuatia hali hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliwaasa wachimbaji hao kuwa wakweli kwa kufanya shughuli zao kwa uadilifu na ubunifu mkubwa wa utafutaji wa masoko ili kuvutia wanunuzi wengi zaidi na hivyo kujiongezea kipato.
Alisema mafanikio hayawezi kupatikana kama wachimbaji watafanya shughuli zao kwa ulaghai na aliwataka kuacha kutafuta mafanikio kwa njia ya mkato ikiwemo hiyo ya kuchanganya Jasi na takataka ambayo alisema imewasababishia kukimbiwa na wanunuzi.
“Tukitumia madini haya vizuri huku tukiongeza ubunifu, tutafanikiwa kufikia malengo tuliyojiwekea; vinginevyo tutaendelea kulalamika,” alisema.
Aliongeza kwamba Serikali itafanya jitihada za kutangaza Madini ya Jasi yanayochimbwa nchini na kuwataka wachimbaji wa madini hayo kuhakikisha wanazingatia suala la ubora unaotakiwa Kimataifa.
“Ninawahakikishia tutawatafutia soko mahala popote Duniani, ili kuhakikisha mnanufaika na madini haya mnayochimba ila mkumbuke uaminifu ni muhimu,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Aidha, aliongeza kwamba Serikali inakaribisha wawekezaji wakubwa kuwekeza kwenye biashara ya Madini ya Jasi ikiwemo ujenzi wa viwanda vinavyotumia Madini ya Jasi kama malighafi ya kutengenezea saruji na bidhaa mbalimbali kama mapambo ya majumbani na chaki.
Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Singida kwa ziara ya siku tatu ya kutembelea shughuli za uchimbaji wa Madini mkoani humo pamoja na kuzungumza na wachimbaji ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa lengo la kutafutia ufumbuzi.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Singida, Sosthenes Massola (kushoto) akizungumza na Wafanyakazi, Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini ya Jasi (hawapo pichani) wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia aliyesimama) Mkoani Singida.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Mapambo ya majumbani cha RSR kilichopo Singida Mjini, Rashid Rashid (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) baadhi ya bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo zitokanazo na Madini ya Jasi yanayochimbwa Itigi mkoani humo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (aliyesimama) akizungumza na Wafanyakazi, Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini ya Jasi (hawapo pichani) wakati wa ziara yake Itigi Mkoani Singida. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Pius Luhende.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akitembelea Kiwanda cha kutengeneza Chaki cha Furaha, kilichopo katika Kata ya Tambukareli, Itigi. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Pius Luhende na kushoto ni Meneja wa Kiwanda hicho, Peter Nolasco.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akimsikiliza Meneja wa kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Furaha, Peter Nolasco (kushoto). Kutoka kulia ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Singida, Sosthenes Massola na Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Madini wa Mkoa wa Singida (SIREMA), Farijala Kiunsi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akizungumza jambo alipotembelea Kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Dobercolor kilichopo katika Kijiji cha Majengo, Itigi. Wengine ni baadhi ya wafanyakazi wa Kiwanda hicho.
No comments:
Post a Comment