Friday, December 1, 2017

Upasuaji wa Kihistoria, Aliyepandikizwa Figo Muhimbili Aruhusiwa

Bibi Prisca Mwingira ambaye alifanyiwa upasuaji wa kupandikizwa figo Novemba 21, mwaka huu akiishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), madaktari bingwa wa hospitali hiyo pamoja na Rais John Pombe Magufuli baada ya afya yake kuendelea vizuri. Bibi Prisca ameruhusiwa kurejea nyumbani leo saa 6:00 mchana baada madaktari bingwa wa magonjwa figo kufanikisha upasuaji huo wa kihistoria. Kulia ni Bathelomayo Mwingira ambaye amempatia dada yake figo. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Jacqueline Shoo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo Dkt. Kisanga (katikati), wote wa Muhimbili.
Bibi Prisca Mwingira akimshukuru kaka yake, Bathelomayo Mwingira kwa kumpatia figo kutokana na tatizo hilo kumsumbua katika kipindi cha mwaka mmoja.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini wakishudia tukio hilo lakihistoria ambalo limefanywa na madaktari bingwa wa Muhimbili.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Jacqueline Shoo akizungumza na waandishi wa habari baada ya Bibi Prisca kuruhusiwa kurejea nyumbani kutokana na afya yake kuendelea vizuri.
Baadhi ya wananchi wakishudia tukio hilo leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mzazi wa Bibi Prisca, Mzee Mwingira akiwashukuru madaktari wa hospitali hiyo kwa kufanikisha upasuaji huo na sasa mtoto wake anaendelea vizuri kiafya.Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

………….

Dar es salaam, Tanzania. Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kihistoria wa kupandikizwa figo leo ameruhusiwa kutoka katika hospitalini akiwa na afya njema.

Bibi Prisca Mwingira ambaye amefanyiwa upasuaji mkubwa na wa kwanza kufanyika hapa nchini alipandikizwa figo Novemba 21, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) chini ya timu ya wataalam wa MNH kwa kushirikiana na watalaam wa Hospitali ya BLK ya nchini India.

Akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini Bibi Prisca amewashukuru watalaamu wote walioshiriki katika kumuhudumia na pia ametumia fursa huyo kumuomba Rais John Magufulu kuendelea kuisaidia MNH ili kuhakikisha huduma za kibingwa wa juu zinaendelea kutolewa katika hospitali hiyo.

“Kipekee namshukuru mwenyezi Mungu, madaktari , wauguzi, uongozi wa Hospitali ya Muhimbili pamoja na serikali kwa kufanisha matibabu yangu, nilisumbuliwa na ugonjwa wa figo takribani mwaka mzima na kuingia katika matibabu ya kuchuja damu, lakini hatimaye leo kaka yangu amejitolea figo yake moja na nimewekewa mimi kwa kweli namshukuru sana.

“Napenda kuwashauri wagonjwa wenye matatizo ya figo na wanaoendelea na huduma ya kuchuja damu wasikake tamaa kwani sasa matibabu yamepatikana na mimi ni shuhuda katika hili,’’ amesema Bibi Prisca.

Kwa upande wake, Bwan Bathelomayo Mwingira ambaye amemtolea figo dada yake, amesema anafuraha kwani amesaidia kufanikisha matibabu ya dada yake na anamuomba Mungu afya ya dada yake izidi kuimarika.

Pia, Baba mdogo wa Prisca , Ainhard Mwingira ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kufanikisha huduma za kibingwa kutolewa Muhimbili.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya figo, Dkt. Jackline Shoo wa Muhimbili amesema upasuaji wa kupandikiza figo ulitumia takribani saa nne na zoezi hilo limekamilika vizuri na mgonjwa anarejea nyumbani huku afya yake ikiwa salama.

“Mgonjwa anaondoka Hospitalini akiwa mzima salama kabisa , anaenda kujumuika na familia yake ataishi kama binadamu wengine ingawa kuna masharti atatakiwa kuyafuata kama alivyoshauriwa na wataalam,” amesema Dkt. Shoo.

Pia, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hudma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha amesema upasuaji huo umegharimu Shilingi Milioni 21 na endapo mgonjwa angepelekwa nchini India matibabu yake yangegharimu Shilingi Milioni 80 hadi Shilingi milioni 100.

“Kwa niaba ya uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili nawapongeza watalaam wote walioshiriki katika upasuaji huu mkubwa na wa kihistoria na pia naishukuru serikali kwa kufanikisha zoezi hili,’’ amesema.

No comments: