Saturday, December 23, 2017

SERIKALI YATOA SIKU SABA MKANDARASI WA BWAWA LA RUNGWA-ITIGI, KULETA VIFAA MUHIMU VA UJENZI

Mhandisi wa Maji Mkoa wa Singida Lydia Joseph (aliyevaa kofia nyeupe) akiendelea na ukaguzi wa bwawa la Rungwa-Itigi, nyuma yake ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Serikali za Mitaa Mwajabu Nyamkomola.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Serikali za Mitaa Mwajabu Nyamkomola akiwa na watendaji wa serikali na wawakilishi wa Mkandarasi wa bwawa la Rungwa wakitembelea eneo la Bwawa hilo mapema jana.
Baadhi ya vibarua wakiendelea na zoezi la kuchanganya zege kwa ajili ya ujenzi wa ukuta katika bwawa la Rungwa – Itigi, Serikali Mkoani Singida imeagiza kazi hio ifanywe na mashine ili kuleta ufanisi na kasi huku vibarua hao wakitakiwa kuendelea na kazi nyingine katika bwawa hilo.
Sehemu ya Bwawa la Rungwa –Itigi linalojengwa na serikali kwa zaidi ya shilingi milioni mia saba ili kutatua kero kubwa ya maji katika kijiji cha Rungwa.


Mkandarasi anayejenga bwawa la Rungwa katika Halmashauri ya Itigi amepewa siku saba na Serikali Mkoani Singida kuhakikisha anapeleka vifaa muhimu vitakavyoongeza kasi na ufanisi wa ujenzi wa bwawa hilo.

Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Serikali za Mitaa Mwajabu Nyamkomola ametoa agizo hilo mapema jana mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo na kukuta ukiwa katika asilimia 35 wakati ulitakiwa kuwa asilimia 60 huku baadhi ya vifaa muhimu vikikosekana.

Nyamkomola amemueleza Mhandisi mwakilishi wa kampuni ya Proactive Independent Group Ltd Elias Gamba kuwa wananchi wa Rungwa hawana maji na juhudi za serikali kuwapatia maji kupitia mradi huo wenye thamani ya zaidi ya milioni mia saba unatakiwa kufanyika kwa kasi na ufanisi wa hali ya juu.

Ameeleza kuwa baada ya kufanya ukaguzi katika bwawa hilo wamebaini kuwa baadhi ya kazi zimekuwa zikifanywa kwa kasi ndogo kutokana na kutokuwepo kwa mashine na badala yake kazi hizo kufanywa na vibarua huku vifaa vingine vikiwa pungufu tofauti na makubaliano katika mkataba.

“Kuna kazi ya kutengeneza zege kwa ajili ya kujenga ukuta katika bwawa hili, ile zege tumeona inachanganywa na vibarua badala ya mashine tuliyokubaliana, mkandarasi unapunguza ubora na kasi inakuwa ndogo, unatuchelewesha kuwapa wananchi maji, hata huu mchanga unaotumika haufai uache kutumika mara moja”, amesisitiza Nyamkomola na kuongeza kuwa,

“Sasa hivi mlitakuwa kuwa mmeshachimba mtaro wa bomba la kusafirisha maji kwenye matenki kwahiyo ndani ya siku saba hakikisheni kijiko cha kuchimba mtaro huo, mabomba na vifaa vyote vitakavyotumika katika kujengea viwe vimewasili hapa Rungwa”, amefafanua.

Naye Mhandisi wa Maji Mkoa wa Singida Lydia Joseph amesema ujenzi wa bwawa hilo unatakiwa kukamilika kabla ya mwezi Februari mwakani ili serikali na Mkandarasi wapate muda wa matazamio na kurekebisha dosari endapo zitajitokeza pamoja na kuwahi msimu wa mvua ili kuvuna maji hayo.

Mhandisi Lydia amemueleza mhandisi mwakilishi wa Mkandarasi kuwa anatakiwa kuzingatia makubaliano ya mkataba ikiwemo ubora wa vifaa vya kujengea pamoja na kuleta mashine zote zinazotakiwa ili kazi ifanyike kwa ubora uliokusudiwa.

Kwa upande wa Mhandisi mwakilishi wa kampuni ya Proactive Independent Group Ltd Elias Gamba amekiri kutumia vibarua kuchanganya zege pamoja na kutumia mchanga tofauti na makubaliano kutokana na mvua zilizonyesha huku akiahidi kurekebisha dosari hizo.

Mhandisi Gamba amesema kampuni hiyo italeta vifaa hivyo kama walivyoelekezwa na serikali ili kuharakisha kazi hiyo na kuifanya iwe na ubora wa juu kwa kuwa na wao wangependa kuona bwawa linakamilika ndani ya muda waliopewa na likiwa na ubora mzuri.

Ameeleza kuwa wamekuwa na changamoto ndogondogo ambapo hakuna ambazo zimesababishwa na serikali na kueleza kuwa changamoto hizo ni pamoja na mvua kunyesha na kusababisha kazi kusimama huku mchanga na mawe vikipatikana mbali kutoka eneo la bwawa na huku vibarua wengi wakipungua kutokana na kuanza msimu wa kilimo.

Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Rungwa Mashaka Juma ameishukuru serikali kwa kufanya jitihada za kutatua kero ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakinunua maji shilingi mia tano kwa dumu au ndoo yenye ujazo wa lita ishirini.

“Wananchi wana hamu kubwa kuona bwawa hili linakamilika, maji ni ya shida sana sio wananchi wote wenye uwezo wa kununua maji kwa shilingi mia tano kwa lita ishirini, ndio maana utaona wananchi wengi wanakuja huku bwawani mara kwa mara kuangalia hali ikoje hivvyo tunaomba huyu mkandarasi aongeze kasi”, amesisitiza Juma.

Mhandisi wa Maji halmashauri ya Itigi Evaristo Mgaya ameeleza kuwa ujenzi wa bwawa la Rungwa lenye mita za ujazo milioni 1.7 umeanza mwezi Septemba 2017 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2018 kwa fedha za serikali zaidi ya milioni mia saba na bwawa hilo linajengwa na kampuni ya Proactive Independent Group Ltd kwa kushirikiana na Bahati Investment and Supply.

Mgaya amesema maji kutoka katika bwawa hilo yatasafirishwa katika matenki matatu ya kuhifadhia maji ambapo matenki mawili yenye ujazo wa lita laki moja na nusu yatatumiwa na wanakijiji wa Rungwa na tenki moja lene ujazo wa lita elfu 22 litatumika katika hifadhi ya wanyamapori ya Rungwa.

No comments: