Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu akimkaribisha Mhe Waziri wa Katiba na Sheria kuzindua Baraza la Wafanyakazi na katika salamu zake alisema ni muhumu kwa Serikali kuendelea kuiimarisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya nchi, kiuchumi, kiusalama, katika utawala wa sheria na katiba
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Profesa Paramagamba Kabudi akitabasamu mara baada ya kufungua Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali siku ya jumatatu. Baraza hilo linakutana kwa siku mbili katika ukumbi wa LAPF mkoani Dodoma.
Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiimba wimbo wa mshikamano wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo, wajumbe wa Baraza ni pamoja na Mawakili Wafawidhi wa Serikali, Wakuu wa Divisheni na Vitengo, Wajumbe wa TUGHE na mada mbalimbali zilitolewa wakati wa uzinduzi hao.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju amesema, kutokana na mchango mkubwa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika maendeleo ya kiuchumi, usalama, utawala wa sheria na utawala bora, Kuna umuhimu wa Serikali kuendelea kuiimarisha Ofisi hiyo.
Ameyasema hayo wakati akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Profesa Palamagamba Kabudi kuzindua Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Uzinduzi wa baraza hilo umefanyika siku ya jumatatu katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la LAPF Mkoani Dodoma.
Uzinduzi wa Baraza hilo, ulitanguliwa na uchaguzi wa Katibu na Katibu Msaidizi. Zoezi la uchaguzi lilisimamiwa na Katibu Mkuu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. John Mchenya, Naibu Katibu Mkuu TUGHE Taifa Bi. Jane Mbura na Afisa Kazi Bi. Razina Tuusa. Waliochaguliwa kwa kura za Siri ni Wakili wa Serikali Mkuu Monica Mbono ambaye anakuwa Katibu na Bw. Michael Masanja anakuwa Katibu msaidizi.
Mhe. Masaju akiwa ni Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi, ameyataja maeneo ambayo Serikali inatakiwa kuendelea kuyaimarisha katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni pamoja na, Raslimali fedha, mafunzo, makazi salama kwaajli ya mawakili wa serikali na miundombinu ya ofisi.
“Mhe. Waziri, yapo masuala ya kisera ambayo tunaomba Serikali inayashughulikie ipasavyo ili kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Maeneo hayo ni kuajiri Mawakili wa Serikali na Watumishi wa Kada zingine, kujenga majengo ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika Ofisi za Wilaya na Mikoa ili kuokoa fedha inayotumika kulipia pango”. Ameleza Mwanasheria Mkuu.
Kwa upande wa mafunzo, Mwanasheria Mkuu, ameishauri Serikali katika kuwajengea uwezo wa kitaalam Mawakili wa Serikali na watumishi wenzao katika maeneo ya kipaumbele na kuimarisha maslahi ya mawakili wa serikali na watumishi wote katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pamoja na kutaja changamoto mbalimbali ambazo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikikabiliana nazo katika utekelezaji wa Majukumu yake. Mwanasheria Mkuu ametaja mafanikio ambayo Ofisi imeyapata katika utekelezaji wa majukumu yake.
Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na kuokoa fedha nyingi na kuingiza serikalini mapato kupitia uendeshaji wa mashtaka na mashauri mbalimbali mahakamani na katika mabaraza ya usuluhishi, ushiriki katika majadiliano ya Mikataba na uhakiki wake na kudumisha utawala wa sheria na utengamano nchini.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuingiza serikalini kiazi cha shilingi 1.039 Bilioni iliyotokana na faini baada ya serikali kushinda kesi 110 zinazohusiana na makosa chini ya sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 2009.
Mafanikio mengine ni urejeshwaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu ambapo kesi 10 zilitolewa uamuzi na mali zenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2 zilitaifishwa. Vile vile Serikali ilishinda kesi 3 zinazohusiana na utakatishaji wa fedha haramu ambapo mbali na watuhumiwa kutiwa hatiani kiasi cha fedha kipatacho shilingi milioni 29,439,452 kilitaifishwa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akifafanua zaidi mafanikio yanayotokana na majukumu ya Ofisi yake kuwa ni yale yanayotokana na mashauri mawili yanayohusu kuingiza nchini magari mawili ya kifahari yaliyotolewa uamuzi kwa watuhumiwa kupatikana na hatia na magari hayo ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 1.7 yalitaifishwa kuwa mali ya serikali na fidia ya shilingi milioni 200 kulipwa serikalini.
Akizindua Baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Profesa Palamagamba Kabudi alipongeza uamuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuzindua Baraza lake na kukutana kwa siku mbili kujadili masuala mbalimbali.
Kwa mujibu wa Waziri Kabudi, Baraza la Wafanyakazi ni chombo cha kupanga mipango muhimu na kuhakikisha kuwa kinafanyika pia katika kutathmini ambacho Ofisi imepanga kukifanya na kimefanyika kwa kiwango gani.
Akasema “sote tu mashahidi kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani msisitizo umekuwa kwa kila taasisi kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yake. Awamu hii inasisitiza watumishi na taasisi kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kuhakikisha utendaji wao unaleta tija katika serikali” ameeleza Waziri
Na akalitaka Baraza hilo la wafanyakazi kutathimini ni jinsi gani linaishauri serikali na taasisi zake katika masuala yote kwa kuhakikisha kwamba ushauri unaotolewa unabeba maslahi mapaba ya taifa na kuzingatia vipaumbele vya serikali ya awamu ya tano
Akasisitiza pia kwamba tathmini hiyo inatakiwa kwenda mbali zaidi kwa kujiuliza kama m Miswada inayoadaliwa inakidhi vigezo vya kitaalam, je inabeba maslahi mapana ya nchi, au je jukumu la kuiwakilisha Serikali mahakamani liinatekelezwa kwa kiwango gani cha ufanini, je kesi na mashauri yote yanasimamiwa na kuendeshwa kwa weledi na uzalendo na ni kwa kiasi gani uratibu wa upelepezi na uendeshaji wa mashauri unafanyika kwa weledi na umakini.
Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali linahudhuriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza, naibu Mwanasheria Mkuu, Bw. Gerson Mdemu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti , Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Biswalo Maganga, Mawakili Wafadhiwi kutoka Mikoa yote na Wilaya ambako kuna Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakuu wa Divisheni na Vitengo na Na wajumbe wa TUGHE.
Aidha mada mbalimbali zinatolewa zikiwamo zinazohusu maadili katika utumishi wa umma na utunzaji wa siri za serikali.
No comments:
Post a Comment