Saturday, December 2, 2017

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA WA CHINA AKUTANA NA JAJI MKUU WA TANZANIA

Mhe. Jaji Mkuu akifurahia zawadi ya picha aliyopatiwa na Mgeni wake.
Picha ya pamoja baada ya Majadiliano: wa nne kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, katikati ni Naibu Waziri wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Zhao Dacheng, wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga pamoja na Wajumbe waliombatana na Naibu Waziri.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akimkaribisha Naibu Waziri wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Zhao Dacheng pindi alipowasili katika Ofisi ya Jaji Mkuu-Mahakama Kuu Zanzibar.
Naibu Waziri wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Zhao Dacheng (katikati) akiongea jambo na Mhe. Jaji Mkuu pindi alipomtembelea Desemba 01, 2017.
Majadiliano yakiendelea; pichani ni baadhi ya Wajumbe walioambatana na Naibu Waziri huyo, mbali na Wajumbe hao pia kuna Wajumbe kutoka Mahakama ya Tanzania na Wizara ya Katiba na Sheria, wa pili kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga na wa kwanza kushoto ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria-Tanzania.
Naibu Waziri wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Zhao Dacheng akipitia nakala ya Kitabu cha Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/2016-2019/2020) alichozawadiwa na Mhe.Jaji Mkuu wa Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akichangia jambo katika majadiliano baina yake na Naibu wa Waziri wa Katiba na Sheria wa China.


Na Mary Gwera, Zanzibar

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim H. Juma ashauri juu ya uwezekano wa kuwa na Kanuni za pamoja za Sheria ya Biashara na Uwekezaji ‘Trade Investment Regulations’ kati ya Tanzania na China zitakazowezesha ukuaji wa uchumi ambao utasaidia kuleta maendeleo baina ya nchi hizi mbili.

Aliyasema hayo, Desemba 1, katika maongezi maalum na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng, pindi alipotembelewa na Naibu Waziri huyo Mahakama Kuu-Zanzibar ambapo Mhe Jaji Mkuu anaendelea na Vikao maalum vya Mahakama ya Rufani ‘court session’

Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa; China ni nchi ambayo tayari imeshapiga hatua kubwa kiuchumi na kimaendeleo, hivyo kuwepo kwa Kanuni wezeshi za Biashara Uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (2) utasaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania pia.

“Ni vyema kuangalia juu ya uwezekano wa nchi zetu; Tanzania na China kuwa na kanuni zinazofanana zitakazotoa muelekeo wa jinsi ya kuwekeza kwa manufaa ya pande zote mbili,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng aliafiki ushauri huo uliotolewa na Mhe. Jaji Mkuu na kumtaka kuendelea na hatua za awali za uwasilishaji wa pendekezo hilo kwa taratibu zinazotakiwa kufanyika ili kufanikisha utekelezaji wa ushauri uliotolewa.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu pia alimueleza Naibu Waziri huyo juu ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati unaoendelea kufanyika ndani ya Mahakama kwa kutaja baadhi ya vipaumbele ambavyo Mahakama imejiwekea ikiwa ni pamoja na utoaji wa Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama, Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kadhalika.

Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania inakusudia pia kuwafikishia huduma ya Mahakama Watanzania wote kwa ngazi ya Kata.“Kwa sasa changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni jinsi ya kuwafikishia huduma ya Mahakama wananchi wote, tuna zaidi ya Kata 3000, lakini Mahakama ya Tanzania ina majengo ya Mahakama za Mwanzo yasiyozidi 900, hivyo Mpango uliopo ni kufikisha huduma za Mahakama kwa wananchi wote ili kuwaondolea aza za umbali pindi wanapotafuta haki zao,” alifafanua Mhe. Jaji Mkuu.

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama katika uendeshaji wa shughuli zake.“China ni nchi inayoendelea kukua kiuchumi hivyo tunapaswa kutoa mchango kwa Tanzania pia ili kuendelea kukua kimaendeleo,” alisema Mhe. Zhao Dacheng.

Naibu Waziri huyo aliyeambatana na Ujumbe wa Wakurugenzi na Maafia sita (6) kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Watu wa China walionana na Mhe. Jaji Mkuu lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili; Tanzania na China.

No comments: