NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Taifa, Gaudencia Kabaka amewataka wanawake wa umoja huo kuvunja makundi ya ngazi zote yaliyojengeka wakati wa uchaguzi na badala yake wafanye kazi za kuwatumikia kwa ufanisi wapiga kura waliowapa ridhaa ya kuongoza.
Pia, amesema UWT kupitia uongozi wake mpya ulioingia kwa sasa ni lazima irejeshe heshima yake ya kuwa chombo cha kuwaunganisha wanawake wote wa mijini na vijijini Tanzania ili wapate maendeleo.Wito huo ameutoa katika hafla ya mapokezi ya uongozi huo yalioandaliwa na UWT Mkoa wa Dodoma katika viwanja vya White house Makao Makuu ya CCM Dodoma.
Amesema bila kuvunja makundi Umoja huo hautopata maendeleo na watatumia muda mwingi kulaumiana, kuangaishana na hamaye kukosa muelekeo wa kutekeleza ahadi walizotoa kwa mamilioni ya wanawake wa Tanzania.Kabaka ameeleza kwamba Umoja wa Wanawake Tanzania ni chombo cha CCM kinachotakiwa kuwa nguzo na muhimili mkuu katika kusimamia na kulinda maslahi ya Chama kisiasa, kiuchumi na kijamii.
"Furaha yangu ni kwamba mlituchagua kihalali bila ya kutumia rushwa, hivyo nasi tuna deni la kuwalipa ambalo ni lazima tutimize utumishi bora na uliotukuka kwa miaka mitano ya uongozi wetu.Na nakuombeni tushirikiane kwa pamoja kupinga rushwa na ufisadi ndani ya UWT na Chama kwa ujumla kama tunavyopinga makundi ya kuhatarisha uhai wa Chama cha Mapinduzi", amesema Mama Kabaka.
Amesema jopo la viongozi wa ngazi mbali mbali wa UWT waliochaguliwa hivi karibuni ndio jeshi la kisiasa la Akina Mama wanaotakiwa kuongoza mapambano ili CCM ishinde na kubaki madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.Kupitia hotuba yake Mwenyekiti huyo, ameagiza miradi yote ya UWT Tanzania iorodheshwe ndani ya miezi miwili kwa lengo la kuijua ipo mingapi na kuweka utaratibu rasmi ili iwanufaishe akina mama wote.
"Mbali na miradi ya kiuchumi iliyopo Makatibu wa ngazi mbali mbali tafuteni takwimu sahihi zinazohusu masuala ya huduma za kijamii hasa zinazowahusu wanawake." ameagiza Mwenyekiti huyo.
Pamoja na hayo ametoa shukrani zake kwa wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja huo kwa kuwaamini kisha kuwachagua kwa kura nyingi viongozi wote wa ngazi ya Taifa.“Natoa ahadi yangu tena kwenu kwamba mmeniamini nami nitatenda mema kwenu kwa kurejesha matumaini ya kutenda na kusimamia mambo yote yenye manufaa kwa wanawake wa Tanzania.
Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thwaiba Kisasi amesema dhamira ya UWT ni kuzitatua changamoto mbali mbali zinazowakabili Akina mama ili wanufaike na matunda ya kuwa mwanachama wa Umoja huo.Ameeleza kwamba viongozi hao hawatowaangusha kiutendaji bali watatumia uzoefu na taaluma zao kuleta maendeleo endelevu ndani UWT.
Akizungumza Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma, Neema Majule amesema Umoja huo umevuna wanachama wapya 5000 kupitia Chaguzi za ngazi mbali mbali zilizofanyika katika Mkoa huo.
Amesema UWT imejipanga kuanzisha miradi mikubwa ya kiuchumi kuanzia ngazi za Wilaya za Mkoa huo na mwanamke mmoja mmoja kwa lengo la kujikomboa kiuchumi.Mapema katika hafla hiyo jumla ya wanachama wapya 1700 wamekabidhiwa kadi za CCM kwa lengo la kuitumikia jumuiya na Chama kwa ujumla.
Viongozi mbali mbali walioudhuria katika hafla hiyo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Hakson, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Maulid Mwita na Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Amina Makilagi.
No comments:
Post a Comment