Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Mpina (mwenye miwani) akiangalia maboksi ya samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 yaliyokamatwa katika kituo kikuu cha basi cha mjini Kagera hapo jana.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Mpina(mwenye miwani ) akitoa tamko la kumsimamisha kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Ayoub Ngoma kwa tuhuma za kushiriki katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.
. Moja ya boti inayotumika kwenye doria katika ziwa Viktoria na Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera.
……………………………………………………………………………………..
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yohana Budeba kumsimamisha kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Ayoub Ngoma kwa tuhuma za kushiriki katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.
Akizungumza katika ofisi ya Kitengo hicho iliyopo mjini Kagera, Mpina alisema mnamo tarehe 03/12/2017 majira ya Saa 03:00 asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter likiwa limepakia samaki zenye uzito wa kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara.
“Katika kipindi cha uongozi wangu, tayari nimesha waagiza Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu kutembea na barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi watumishi wote wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa hatuna hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara moja.” Alisisitiza Mpina
Aidha, Waziri alisema Afisa huyo na Dereva wa gari hilo bwana Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio hilo, na kuongeza kwamba samaki hawa walikuwa wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya Uvuvi Na 22 ya 2003 na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.
Afisa Mfawidhi wa Kanda wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Gabrieli Mageni alimweleza Waziri Mpina baadhi ya taratibu zilizokiukwa kuwa ni pamoja na samaki hao kutopaswa kuvuliwa kwa kuwa walikuwa wakubwa zaidi ya sentimeta 85 na wadogo chini ya sentimeta 50, msafirishaji kutokuwa na kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi, kutolipia ushuru na mrabaha wa Serikali, kutokuwa na cheti cha afya pamoja na leseni ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi.
Waziri Mpina alisema samaki hao walitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi wa Murusagamba, Kiteule cha Jeshi la Wananchi la Tanzania Murusagamba, Kituo cha Polisi Murusagamba pamoja na Shule ya Sekondari Murusagamba baada ya kupata kibali cha Mahakama.
Alisema kazi hiyo ilifanyika chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngara. Luteni kanali,Michael Mtenjele. Aliongeza kuwa, uchunguzi wa awali ilibaini kuwa samaki hao walitokea kwenye kijiji cha Izigo wilayani Muleba.
Ametaja baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni kuwa ni pamoja na kukamatwa kwa furu kilo 9100 zilizokuwa zinatoroshwa kwenda nchini Uganda ambapo zilitaifishwa na kuuzwa kwa amri ya mahakama na watuhumiwa wawili kufikishwa mahakamani kwa kosa hilo.
Kukamatwa kwa uduvi kilo 5000 ambazo zililipiwa mrabaha na mtuhumiwa kulipa faini ya shilingi 100,000/=,kukamatwa kwa mafurushi 6 ya Samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 katika kituo cha Basi cha Bukoba zilizokuwa zikitoka mkoani Kigoma kwenda Uganda ambapo mtuhumiwa alikimbia na samaki hao kutaifishwa.
Katika tukio jingine jumla ya kilo 100 za mabondo mabichi ya samaki yamekamatwa kwenye doria mpakani Mtukula na mtuhumiwa amefikishwa polisi kwa hatua za kisheria.
Waziri Mpina amewaomba wavuvi kuzingatia Sheria na taratibu mbalimbali za uvuvi nchini ili sekta hiyo iwe na tija na kuchangia katika uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.
Wakichangia kwa nyakati tofauti watumishi wa kituo hicho waliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mpina kuangalia namna ya kuongeza nguvu kazi na vitendea kazi mbalimbali vitakavyosaidia kudhibiti uvuvi haramu.
Nahodha Mkuu wa kituo hicho, bwana Ernest Maguzu alisema kazi ya doria katika ziwa Viktoria imekuwa ngumu kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano kwa kuwa wavuvi wamekuwa wakiwasiliana mara moja kutumia simu za mikononi pindi wanapoziona boti za doria zinaingia ziwani na kufanikiwa kukimbia.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora na Masoko bi, Theresia Temu aliiomba kuongeza udhibiti wa usafirishaji wa bidaa zitokanazo na mazao ya uvuvi nje ya nchi kwa kuwa hivi sasa Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na wafanyabiashara kutorosha mazao hayo mipakani bila kulipa ushuru.
Bi Temu alisema kuwa inakadiriwa kuwa zaidi ya tani mia moja ya mazao ya uvuvi yanatoroshwa kila mwezi katika mipaka ya nchi jirani hivyo jitihada za pamoja baina ya wadau mbalimbali zinahitajika ili kupambana na tatizo hili
“Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo kubwa tunaomba Serikali kuliangalia kwa jicho la tatu namna nyingine tutaendelea kuibiwa” alisisitiza bi Temu
Waziri Mpina alisema Halimashauri zote nchini zinatakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinza raslimali za majini na baharini kwa kuwa licha ya raslimali hizo kutoa mchango mkubwa wa uchumi kwa taifa pia manufaa yake ni kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Nataka suala la uvuvi wa mabomu na nyavu za kukokota liwe historia katika nchi yetu. Tutaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakaje tuhujumu” alisisitiza Mpina
No comments:
Post a Comment