Tuesday, December 19, 2017

MKURUGENZI MTENDAJI WA TASAF AWATAKA WATUMISHI WA TAASISI HIYO KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMM KWA VITENDO.

Estom Sanga- TASAF

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF- bwana Ladislaus Mwamanga amefungua kikao kazi cha Watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es salaam na kuwaagiza wazingatie misingi ya Utumishi wa Umma ili kufanikisha jukumu la kuwahudumia wananchi na hivyo kusaidia jitihada za serikali za kupambana na umaskini kwa vitendo.

Bwana Mwamanga amesema Watumishi wa taasisi hiyo wanalo jukumu kubwa mbele yao katika kutekeleza mkakati wa kuwaondolea wananchi kero ya umaskini kazi ambayo amesema mafanikio yake yatapimwa kulingana na mabadiliko ya maisha ya wananchi wanaohudumiwa na Mfuko huo kupitia Mpango wake wa Kunusuru Kaya Masikini-PSSN.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amewakumbusha wajibu wa watumishi wa taasisi hiyo kuzingatia maadili bora ya utumishi wa umma na kutumia waledi walionao katika kutoa huduma bora kwa walengwa na wananchi wanaotegemea huduma zake kote nchini.

Akizungumzia mafanikio ya PSSN, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amesema tangu kuanza kwa Mpango huo, Walengwa wake wameonyesha nia ya dhati ya kuondokana na umaskini kwa kuanzisha miradi midogo midogo huku wengine waboresha makazi yao na kuzingatia masharti ya Mpango katika sekta za elimu, afya na lishe.

Amesema kinachosisitizwa kwa sasa ni kuhakikisha kuwa walengwa hao wanaweka misingi imara ya kujitegemea kwa kufanya kazi za kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao, kama ambavyo maelekezo ya serikali yanavyosisitiza.

Bwana Mwamanga pia amezungumzia namna taasisi yake ilivyoweka mkazo katika ushirikishwaji wa sekta nyingine zikiwemo za maendeleo ya jamii,mifugo na kilimo katika kiuboresha shughuli za walengwa za kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao.TASAF hivi sasa inahudumia kaya za walengwa zipatazo MILIONI MOJA NA LAKI MOJA nchini kote.

Kikao kazi hicho kinachowajumusha watumishi wa taasisi hiyo kutoka mikoa yote nchini pamoja na mambo mengine kitapitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Maandalizi sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya maskini na kupata taarifa ya Maafisa Ufuatiliaji juu ya kazi wanazozifanya kwenye maeneo yao ya kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga (aliyeshika kipaza sauti) akifungua kikao kazi cha watumishi wa taasisi hiyo(hawapo pichani ) kinachofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyi mjini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa fedha Bi. Chiku Thabiti, na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Miradi bw. Amadeus Kamagenge. 

Watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF wakisimama kwa dakika moja kuwakumbuka baadhi ya watumishi waliopoteza maisha au kupoteza ndugu na jamii zao katika kipindi cha mwaka huu kabla ya ufunguzi rasmi wa kikao kazi chao kinachofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo jijini Dar es salaam.
 


Baadhi ya Watumishi wa TASAF wakiwa katika kikao kazi chao cha kufunga Mwaka katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo,bwana Ladislaus Mwamanga (hayupo pichani) alipofungua kikao hicho.
Watumishi wa TASAF wakifuatialia kwa makini hotuba ya ufunguzi wa kikao kazi chao kilichoanza leo ,kilichofunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Bwana Ladislau Mwamanga (hayupo pichani.

No comments: