Serikali Mtandao ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika taasisi za umma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa haraka, zilizo za gharama nafuu, zinazofikiwa kwa urahisi, zinazopatikana wakati wote (24/7) na kwa wakati mwafaka. Huduma za Serikali Mtandao zimegawanyika katika maeneo makuu manne: kati ya Serikali na Watumishi wake (G2E), Serikali na Sekta ya Biashara (G2B), Serikali na Wananchi (G2C) na Kati ya Taasisi moja na Taasisi nyingine ya Serikali (G2G).
2.0 Wakala ya Serikali Mtandao
Wakala ya Serikali Mtandao ilianzishwa 2012 kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na.30 ya Mwaka 1997 Sura ya 245 na Kanuni zake. Wakala hii ina jukumu na mamlaka ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa Taasisi za umma. Lengo ni kuziwezesha Taasisi hizo kutumia TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
3.0 Malengo ya Wakala ya Serikali Mtandao
Malengo ya Wakala ya Serikali Mtandao ni pamoja na Kuboresha uwezo wa Taasisi za umma kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao, kuwezesha upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma, Kuboresha mifumo shirikishi ya TEHAMA, Kuimarisha uratibu, usimamizi na uzingatiaji wa viwango vya Serikali Mtandao katika utoaji wa huduma kwa umma, Kuboresha huduma za ushauri wa kitaalam na msaada wa kiufundi na Kushirikiana na Wadau wa Serikali Mtandao.
4.0 Mafanikio ya Utekelezaji wa Serikali Mtandao yenye Umuhimu wa kipekee.
Ndani ya miaka mitano, Serikali imeijengea uwezo Wakala ulioiwezesha kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao kama ifuatavyo:
4.1 Kusimamia utekelezaji wa Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma ili kuwezesha utekelezaji wa serikali mtandao, zaidi ya hayo, Wakala inatumia viwango na miongozo hiyo kutoa maelekezo ya namna sahihi ya kutekeleza jitihada za serikali mtandao na kupunguza urudufu.
4.2 Kuendesha vituo vya Kuhifadhi Mifumo na Data za Serikali vinavyotoa huduma za kuhifadhi tovuti, mifumo tumizi, utunzaji katika sehemu zaidi ya moja, “co-location” na usajili na uhifadhi wa majina miliki.
4.3 Kutengeneza na kuendesha Mtandao wa Mawasiliano Serikalini(GovNet) ulio salama na nafuu ambao Taasisi za umma 150 zikiwemo Wizara na Idara za Serikali,Hospitali za Mikoa na baadhi ya Ofisi za halmashauri.
4.4 Kutoa huduma za ushauri kwa taasisi za umma 299 na huduma za msaada wa kiufundi 2947 katika maeneo ya Uhakiki wa Mifumo ya TEHAMA, Tathmini ya Usalama wa TEHAMA, Utengenezaji wa Mpango wa Kukabili Majanga, Utayarishaji wa Mkakati wa TEHAMA, Utayarishaji wa Sera ya TEHAMA, na Utayarishaji na Usanifishaji wa Shughuli na Uhakiki wa Miradi ya TEHAMA.
4.5 Kutoa mafunzo ya kiufundi ya serikali mtandao katika maeneo ya; usimamizi wa mtandao kwa taasisi 240, Mfumo wa Baruapepe Serikalini kwa taasisi 359, utekelezaji wa huduma mtandao kwa taasisi 76 na usimamizi wa tovuti kwa taasisi 411.
4.6 Kuhuisha na kusanifu upya Tovuti ya Serikali kuwa Tovuti Kuu (www.tanzania.go.tz ) ambayo ni kituo kimoja cha kutolea taarifa na huduma mtandao kwa wananchi kwa kupitia sehemu ya huduma za simu za mkononi na wavuti ya tovuti hii.
4.7 Kutengeneza na kuendesha Mfumo wa Huduma za Serikali kwa
kutumia Simu za Mkononi (mGOV) kama kituo kimoja cha huduma zote za Serikali kwa simu za mkononi, ambapo jumla ya taasisi za umma 117 zinatumia mfumo huo na zaidi ya miamala 15 milioni imefanywa.
4.8 Mfumo wa Ofisi Mtandao (GeOS) ulisanifiwa, kutengenezwa na kutumika kuwezesha shughuli za kila siku za utawala za ofisi Serikalini ndani na miongoni mwa taasisi za umma. Kwa sasa taasisi za umma 28 zimeunganishwa na kutumia mfumo huu.
4.9 Mfumo wa Serikali wa Baruapepe (GMS) ulisanifiwa, kutengenezwa na kutumika, kuwezesha mawasiliano ya ofisi ambapo jumla ya taasisi za umma 359 zikiwemo ofisi za Ubalozi zimeunganishwa na zinatumia mfumo huu.
4.10 Tumewezesha usanifu na utengenezaji wa mifumo mbalimbali inayowesesha utendaji kazi katika Taasisi za Umma ikiwemo Mfumo wa wa kutoa taarifa za ruswa (TAKUKURU kupitia namba 113), Mfumo wa Taarifa na shughuli za Bunge, Mfumo wa Ajira unaorahisisha mchakato wa ajira za Serikali na Mfumo wa Malipo ya Serikali kielektroni(GePG) unaowezesha udhibiti wa ukusanyaji wa Maduhuli kielektroni Serikalini.
5.0 Hitimisho
Pamoja na mafanikio hayo kwa kipindi hicho, hivi sasa Wakala imejizatiti vyema kuanza kipindi kingine cha utekelezaji ili kufanya matumizi ya TEHAMA yawe na manufaa zaidi katika utendaji wa taasisi za umma. Huduma ya serikali mtandao ndio mwelekeo wa miaka ijayo katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha Wakala itaendelea kushirikiana na wadau wa serikali mtandao na kujiimarisha zaidi katika kusimamia utekelezaji wa serikali mtandao kwa ufanisi zaidi.
Pia itaongeza jitihada muhimu kuziwezesha taasisi za umma kuwasiliana na kuweza kukabiliana na matishio ya mtandao yanayozidi kuibuka kila uchao.
Imetolewa Na:
Suzan Mshakangoto
MENEJA WA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO WAKALA YA SERIKALI MTANDAO
21.12.2017
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao, Dk. Jabir Kuwe, akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari ambapo alielezea kuhusu miaka mitano tangu ulipoanzishwa na namna walivyoweza kuhakikisha taasisi za serikali kuingia katika serkali mtandao.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo.
No comments:
Post a Comment