Tuesday, December 5, 2017

MADEREVA WAACHE KUENDESHA VYOMBO VYA MOTO BILA YA TAALUMA WALA LESENI - RC NDIKILO

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani Mkoani hapo, iliyozinduliwa na kufanyika viwanja vya Mailmoja, Kibaha.
Kaimu kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Mkoani Pwani, Salum Morimori akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani Mkoani hapo, iliyofanyika viwanja vya Mailmoja, Kibaha. (picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, amewaasa baadhi ya madereva kuacha kujiingiza kwenye biashara ya usafiri wa vyombo vya moto ikiwemo bodaboda bila kwenda kwenye mafunzo ya udereva na kupata leseni kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria za usalama barabarani. Amesema wapo baadhi ya madereva wanaoendesha vyombo hivyo kwa kujifunza kwa wenzao kwa masaa kisha kuingia barabarani suala ambalo ni kuhatarisha maisha ya abiria wanaowabeba.

Akizindua wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani humo katika viwanja vya Mailmoja, mhandisi Ndikilo alisema ajali nyingi husababishwa na makosa ya kibinadamu. Alisema kati ya makosa hayo ni pamoja na yanayosababishwa kwa makusudi na madereva hao ikiwemo kuendesha huku wakiwa hawana leseni. Mhandisi Ndikilo alieleza kuwa, pia kuendesha wakiwa wametumia vileo ,kupishana pasipo tahadhali (overtaking),uchovu wa kuendesha masafa marefu na kuendesha vyombo vibovu.

"Abiria nao waache ushabiki kuwaambia madereva wazidishe mwendo ,uvukaji wa barabara kwa watembea kwa miguu wakiwa wamelewa ." alifafanua.

Mhandisi Ndikilo alielezea lakini kutokana na kutekeleza kwa vitendo mikakati waliyojiwekea wameweza kupata mafanikio katika kupunguza ajali na vifo vinavyosababishwa na ajali. Anaamini kuwa tatizo lililokuwepo hasa waendesha bodaboda kuendesha bila leseni litapatiwa ufumbuzi wa kudumu ikizingatiwa bodaboda umekuwa usafiri rasmi na unatumiwa na wananchi wengi.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya crane kwa ajili ya kuvutia na kunyanyulia magari yaliyoharibika barabarani ama yanayopata ajali mhandisi Ndikilo,alieleza mwaka jana aliahidi kulishughulikia kwa kuwashirikisha wadau wa barabara "!'na kudai kutokana na kuongezeka kwa wawekezaji wakubwa mkoani hapa,kero hiyo inaenda kupata ufumbuzi. Alisema ataendelea kulifuatilia ili kupata huduma hiyo muhimu ambayo itakuwa tiba ya kudumu kwa barabara za Dar es salaam -Chalinze - Morogoro na Chalinze -Segera.

Nae kaimu kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Pwani,Salum Morimori,alisema vifo vinavyosababishwa kutokana na  ajali za barabarani mkoani Pwani vimepungua kutoka  174 mwaka jana hadi kufikia  watu 89 mwaka  huu. Morimori ambae pia ni katibu wa kamati ya usalama barabarani ya mkoa huo ,  alisema twakwimu hizo ni za kuanzia kipindi cha  januari hadi oktoba mwaka 2016 na mwaka huu kipindi kama hicho.

Alisema  idadi ya watu waliojeruhiwa katika kipindi hicho pia ilipungua kutoka watu 402 mwaka jana hadi kufikia 142. Hata hivyo alisema, jumla ya aina zote za ajali katika kipindi hicho nazo zilipungua   kutoka ajali 383 mwaka jana hadi kufikia ajali 86 sawa na asilimia 77.54 katika kipindi hicho.

Morimori alielezea kupungua kwa ajali kwa kiwango hicho kikubwa ni kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani na kamati ya usalama barabarani ya mkoa wa Pwani ambapo wamekuwa wakifanya kazi za kudhibiti ajali usiku na mchana,kuimarisha doria, misako na operesheni mbalimbali za barabara. Alieleza licha ya kufanikiwa kupunguza ajali lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni sanjali na ufinyu wa barabara ya Morogoro usioendana na ongezeko la vyombo vya moto kwa sasa.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa gari la kufanyia doria na operesheni za kupambana na madereva wazembe.

“Pia kuna ukosefu wa crane kwa ajili ya kuvutia na kunyanyulia magari yaliyoharibika barabarani ama yanayopata ajali ambapo ajali inapotekea mara nyingi barabara hufunga  na kusababisha msongamano mkubwa wa magari barabarani”, alisema Morimori.

Lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kutoa elimu ya usalama barabarani kwa umma na makundi yote yanayotumia barabara.

No comments: