WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wana-Lindi na wana-Ruangwa watumie fursa zilizopo ili kufanikisha maandalizi ya sherehe za Maulid na Baraza la Maulid Kitaifa mwaka huu.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
Waziri Mkuu amesema sherehe hizo zitafanyika Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, saa 3 asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.
Aliwataka wana-Ruangwa waharakishe kujenga nyumba za kulala wageni na sehemu za kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa. “Kila mmoja anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,” alisisitiza.
“Kwa niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mheshimiwa Mufti na Baraza la Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa wilayani kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika sherehe hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” alisema.
Alisema uamuzi huo wa BAKWATA ulitangazwa kwenye Baraza la Maulid lililofanyika Singida, mwaka jana ya kwamba wameamua kuadhimisha sherehe hizo kwenye ngazi ya wilaya badala ya kuwa inafanyika makao makuu kila mwaka.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaarifu viongozi hao kwamba maandalizi yanaendelea na kwamba vifaa mbalimbali kama mchele, vitoweo, unga wa ngano, sukari, maji, juisi, mahema, mikeka na mazulia vimekwishapatikana.
“Ninaomba Kamati ya Uhamasishaji iifanye kazi hii kwa kutambua kuwa jambo hili si la kwenu peke yenu, bali linaungwa mkono na Serikali, na hii ni kwa sababu Serikali yenu inafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa dini,” alisema.
Alisema misingi ya amani katika nchi hii imejengwa na mahubiri ya viongozi wa dini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji, Sheikh Ali Mohammed Mtopa alisema Ruagwa iko tayari na imepokea wito huo wa kitaifa. “Tunakuhakikishia wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wawakilishi wa Mufti waliopo hapa kwamba tumepokea hiyo heshima,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Itifaki kutoka BAKWATA Makao Makuu na Msimamizi wa Malidi za Kitaifa, Sheikh Mohammad Nassir ambaye alisema wana Ruangwa an wana Lindi wanalo jukumu la kuhamasisha watu washiriki sherehe hizo.
“Hamasa haitatoka Morogoro au Dar es Salaam bali hapahapa Lindi. Tunataraji watu wasiopungua 10,000 watahudhuria sherehe hizi za Maulid kutoka wilaya zote za mkoa wa Lindi na hii ni mbali wawakilishi kutoka kila mkoa wapatao 100 -150,” alisema.
Waziri Mkuu anatembelea vijiji vya jimboni mwake ambako atahutubia wananchi.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, NOVEMBA 5, 2017.
No comments:
Post a Comment