Wednesday, November 15, 2017

WATU 10 WAFIKISHWA MAHAKAMA YA KISUTU KUJIBU MASHTAKA 13 LIKIWEMO LA KUSAFIRISHA BINADAMU KWA NJIA HARAMU

Watu 10 wanaosadikiwa kuwa wachezaji wa Judo nchini, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka 13, likiwamo la kusafirisha binadamu kwa njia haramu, kughushi na kutoa taarifa za uongo katika Ubalozi wa Italia nchini Tanzania.

Washtakiwa wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga aliyekuwa akisaidiana na Pamela Shinyambala na Mwanaamina Kombakono.

Washtakiwa hao walitajwa kuwa ni, Kashinde Bundala, Said Ally, Mafunda Ali, Abdulrazak Baus, Mwamba Mungia, Hafidhi Said, Abubakari Nzige, Athumani Ngondo, Endrew Mlugu na Ahmed Magogo.

Mbele ya Hakimu Mwandamizi, Godfrey Mwambapa imedaiwa kati ya Oktoba Mosi na Novemba 3/2017 jijini Dar es Salaam mshtakiwa Bundala 

chini ya kisingizio cha kuhudhuria mashindano ya Sankuku Judo na mafunzo  aliajiri na kuwasafirisha watu tisa, Kwenda Milan nchini Italia kwa ajili ya kufanya kazi kwa nguvu.

Watu hao ni, Ally, Ali, Baus,Mungia Said, Nzige, Nyondo Mlugu na Magogo.

Katuga amedai Oktoba 5/ 2017 huko Mwananyamala, mshtakiwa Bundala alighushi barua ya Oktoba 5,2017 akionyesha kuwa Umoja Judo Klabu umeomba ushiriki wa timu ya Judo ya Tanzania katika mashindano ya 28 ya Sankuku Judo wakati akijua si kweli.

Aidha katika shtaka la tatu, mshtakiwa Mafunda Alli anadaiwa, kati ya Julai Mosi na Agosti 15/2017, katika ofisi za Hati ya Kusafiria Zanzibar alitoa taarifa ya uongo ili aweze kupatia hati ya kusafiria.

Washtakiwa hao waliosafirishwa pia wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba na Novemba 2,2017 katika Ubalozi wa Italia nchini Tanzania walitoa taarifa za uongo kwa nia ya kujipatia VISA ili waweze kusafiri kwenda nchini Italia.

Washtakiwa wamekana mashtaka

Wanne kati yao wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mdhamini angesaini bondi ya Sh 500,000/.

Mshtakiwa Bundala yeye amerudishwa rumande kwani kosa la kusafirisha binadamu halina dhamana mpaka mahakama kuu.

Washtakiwa wengine walipelekwa rumande hadi Novemba 29/2017 kesi itakapotajwa.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi bado wa kesi hiyo bado haujakamilika, bado wanasubiri taarifa kutoka sehemu husika

No comments: