Waziri
wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy
Mwalimu akimkabidhi kadi ya bima ya afya, Irene Paul kwa niaba ya watoto
wenzanke 139 ambao wanaishi katika mazingira magumu. Kadi hizo
zimetolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na mfuko wa
Abbott na benki ya ABC. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja
Binafsi, Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati wa benki ya ABC, Joyce Malai,
Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Kurasini, Rabikira Mushi na
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru. Kutoka kulia
ni Mkurugenzi wa Miradi Endelevu wa Mfuko wa Abbott, Dkt. Festo
Kayandabila na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali wa
hospitali hiyo, Dkt. Juma Mfinanga.
Baadhi
ya walezi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakishuhudia
jinsi watoto hao wanavyokabidhiwa kadi za bima ya afya leo katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili leo.
Waziri
wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy
Mwalimu akizungumza kabla ya kukabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto
wanaoishi katika mazingira magumu.
Baadhi
ya watoto waliokabidhiwa kadi za bima ya afya na Waziri wa Afya
wakionyesha kadi hizo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
Muhimbili leo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru
akizungumza faida za watoto hao kupatiwa kadi hizo.
Baadhi ya wataalamu wa afya wa Muhimbili wakiwa kwenye mkutano huo leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya ABC wakishuhudia shughuli ya kukabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto hao leo
……………
Serikali
ameipa siku 60 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuandaa mpango
utakaowawezesha wateja wa hiari kulipia fedha kidogo kidogo kwa ajili ya
kupata kadi ya bima ya afya.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kabla ya kukabidhi kadi za bima ya afya
kwa watoto 139 wanaoishi katika mazingira magumu. Kazi hizo zimetolewa
na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Mfuko wa
Abbott na Benki ABC.
Waziri
Ummy Mwalimu ameuagiza mfuko wa NHIF kuhakikisha ndani ya siku 60
inaweka utaratibu ambao utasaidia wateja wa hiari wanapata kadi za bima
ya afya ndani ya muda mfupi kwa kuwa wengi wao hawana fedha taslimu Sh
50,400 za kulipia kwa wakati mmoja.
“Natoa
siku 60 kwa NHIF kuhakikisha inaweka utaratibu wa kuwawezesha watu
kupata kadi ya bima ya afya kwa kulipa fedha kidogo, kidogo kwa mfano
mteja wa hiari anaweza kulipia Sh 5,000 au Sh 10,000 hadi atakapokuwa
amefikisha Sh50,400 ambayo inatakiwa na NHIF,” alisema waziri huyo.
Katika
hatua nyingine, serikali imeipongeza Muhimbili kutokana na juhudi za
kuwawezesha wananchi kupata huduma bora ikiwamo kuwapatia kadi za bima
ya afya watoto 139 wanaoishi katika mazingira magumu.Waziri huyo
amesema uamuzi wa Muhimbili kutoa kadi kwa watoto hao ni mfano wa kuigwa
na kwamba unapaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini.
“Naamini
mpango huu, utawaamsha wazazi, walezi na wadau wengine wa afya ili
kuhakikisha kwamba watoto wa Taifa hili wanakuwa na bima za Afya mara tu
baada ya kuzaliwa,” amesema.
Naye
Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema Muhimbili kwa
kushirikiana mfuko wa Abbot na Benki ABC imewezesha watoto hao kupata
kadi ya bima ya afya ili waweze kupata matibabu popote pale
watakapokwenda nchini.“Muhimbili imekuwa ikitekeleza jukumu lake
kikamilifu la kutoa huduma bure kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa
kuchangia huduma kwa kiasi Sh milioni 500 hadi 600 kwa mwezi sawa na Sh.
bilioni 6 hadi 7.2 kwa mwaka,” amesema Profesa Museru.
Profesa
Museru amesema kadi hizo zitapunguza mzigo mzito kwa vituo vya kutunzia
watoto ambavyo vimekuwa vikigharamia huduma za Afya kwa kutumia fedha
taslimu pale watoto hao wanapougua.
“Mheshimiwa
Waziri, nitoe rai kwa wenzetu NHIF kuangalia namna ambavyo huduma kwa
kundi hili la watoto itaendelea kuwafikiaw ahitaji wengi ili kuhakikisha
watoto wetu wanakuwa na uhakika wa kuzifikia huduma za afya popote
pale,” amesema mkurugenzi huyo.
Katika
hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt.
Juma Mfinanga amesema kutokana na uboreshaji uliofanywa na idara hiyo
hivi sasa wanapokea wastani wa wagonjwa mahututi wapatao 200 hadi 250
kwa siku na kuwapatia huduma ya afya.
“Utafiti
uliofanyika Muhimbili na kuchapishwa katika majarida mbalimbali ya
kimataifa unaonyesha kuwa idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali
imepunguza vifo MNH kwa zaidi ya asilimia 5 kutoka asilimia 13 kabla ya
kuanzishwa kwa idara hiyo hadi asilimia 8 baada kunzishwa,” amesema Dkt
Juma.
No comments:
Post a Comment