Friday, November 3, 2017

WAKULIMA WILAYA YA BUKOMBE WALILIA MBEGU ZA MAHINDI YA WEMA 2109 YANAYOSTAHIMILI UKAME

Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akimkabidhi mbegu ya mahindi ya Wema 2109,  Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya kwa ajili ya kupanda katika shamba darasa katika Kijiji cha Msasa kilichopo Kata ya Runzewe wilayani humo leo. Wengine kutoka kulia ni Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula na Mtafiti, Dk. Beatrice Lyimo  kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)
Maofisa Ugani wakiandaa shamba darasa la mahindi ya Wema  katika Kijiji cha Kabagole kilichopo Kata ya Busonzo litakalosimamiwa na Kikundi cha Igembensabho.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya, akizungumza na wakulima wa Kikundi cha Igembensabho.
Wanakikundi cha Igembensabho wakiwa wameshosha mikono ikiwa ni ishara ya mshikamano.
Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akimkabidhi mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya kwa ajili ya kupanda katika shamba darasa katika Kijiji cha Msasa kilichopo Kata ya Runzewe wilayani humo leo. Wengine kutoka kulia ni Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula na Mtafiti, Dk. Beatrice Lyimo  kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya akikmabishi mbegu ya Wema Ofisa Ugani wa Kijiji cha Kabagole, Ponsian Pancras.
Mtafiti wa Kilimo kutoka Kituo cha Utafiti wa Ilonga mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda, akiwafundisha wakulima wa Kijiji cha Kabagole namna ya kupanda mahindi ya Wema. Kulia ni Ofisa Ugani, David Makabila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Katibu wa Kikundi cha Igembensabho, Jacob Nsunzu akizungumza na waandishi wa habari.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya akikmabishi mbegu ya Wema Ofisa Ugani wa Kijiji cha Msasa, Mohamed Mwangeni. Katikati ni Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange.
Mtafiti wa Kilimo kutoka Kituo cha Utafiti  Ilonga mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda, akiwafundisha wakulima wa Kijiji cha Msasa, namna ya kupanda mahindi ya Wema.

Na Dotto Mwaibale, Bukombe Geita

WAKULIMA wilayani Bukombe Mkoani Geita wameiomba Serikali na wasambazaji wa mbegu bora za mahindi ya WEMA 2109 yanayostahimli ukame kufikisha mbegu hizo wilayani humo ili kuweza kutatua changamoto ya  mavuno kidogo wanayoyapata kila mwaka kutokana na mabadiriko ya tabia nchi na wadudu.

Ombi hilo limetolewa na wana Kikundi cha Igembensabho kwenye Kijiji cha Kabagole Kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani Geita wakati wakipokea mbegu bora za mahindi  yaliyozalishwa na Mradi wa WEMA kwa ajili ya kupanda kwenye shamba darasa la kikundi hicho ili waweze kuyalinganisha na aina za mahindi wanayolima kila mwaka na mahindi hayo yenye sifa ya kustahimili ukame yaliyotolewa na  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)

Akizungumza  kwa niaba ya wanakikundi hicho, Adam Kasalamsigwa alisema kuwa kutokana na sifa walizoambiwa na wataalamu kwenye mahindi hayo yatakuwa mkombozi kwa wakulima wengi kutokana na aina zingine za mahindi waliyozoea kupanda kushindwa kutoa matokeo waliyokuwa wakiyatarajia baada ya mvua kukata mapema kabla mahindi hayajazaa.

“Tunashukuru mmetuletea mbegu hizi ili tufanye majaribio na kuona jinsi mahindi haya yanavyostahimili ukame lakini mmetuambia tayari mmeshayafanyia majaribio kwenye maeneo mengine ya Tanzania na kuonyesha mafanikio makubwa hivyo hatuna sababu ya kusubiri hadi msimu ujao tuleteeni mbegu hizo tununue na kupanda” alisisitiza Kasalamsigwa.

Aidha wakulima hao wameiomba Serikali kuona sababu ya kuziingiza mbegu hizo kwenye ruzuku ya pembejeo ili ziweze kuwafikia hadi vijijini kwa bei nafuu ili ziweze kukinzana na mabadiliko ya taba nchi ambayo yamekithiri sana kwenye wilaya hiyo na maeneo mengine.

Akitoa maelekezo ya namna ya kupanda mahindi hayo Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda aliwaambia mahindi hayo baada ya kufanyiwa utafiti kupitia mradi wa mahindi yanayotumia maji kwa ufanisi (WEMA) waliyajaribu kwenye maeneo mbalimbali kwenye mikoa ya Morogoro na Tanga na kuonyesha kufanya vizuri kuliko aina nyingine za mahindi wanayolima wakulima.

Ngolinda aliwasisitiza kuwa pamoja na wao kupata mbegu hizo zinazostahimili ukame lakini ni lazima wazingatie kanuni bora za kilimo cha mahindi ikiwemo matumizi ya mbolea za kupandia na kukuzia ,kupanda kwa mistari na nafasi  na kufanya Palizi lakini wasipofanya hivyo hawawezi kupata mavuno yanayostahili badala yake watapata hasara kama mahindi mengine.

Aliwataka kuzingatia suwala la kupanda kwa mistari na nafasi ili kuweza kumshakikishia mkulima anatumia shamba lake vizuri badala ya kupanda holela na kujikuta amepanda miche michache kwenye shamba akidhani ni ekari moja kumbe ni miche inayoenea kwenye nusu ekari iliyopandwa vizuri.

Ngolinda aliwashauri wakulima kulima ekari moja kitaalamu na kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili apate mavuno makubwa badala ya kulima ekari tano ambazo anatumia nguvu nyingi na gharama kubwa lakini mwishoni anapata mavuno sawa na mtu mwenye ekari moja.

“ Unalima ekari tano bila kufuata kanuni bora za kilimo alafu unapta magunia 25 ya mahindi wakati mwenzako analima ekari moja tuu kwa kufuata kanuni bora za kilimo na anapata hadi gunia 30 hii ni tofauti kubwa sana kwa hiyo wakulima naomba mbadilike” alisistiza Ngolinda.

Aidha Mtafiti huyo wa zao la mahindi aliwaambia kuwa kufanya majaribio hayo kupitia mashamba darasa kwenye mkoa mzima wa Geita ni kutaka kuwaonyesha wakulima hao mbinu za kisasa za kilimo na matumizi ya mbegu bora yanavyoweza kumsaidia mkulima kuzalisha kwa tija ili aachane na kilimo cha mazoea ambacho hamkimsaidii mkulima kuondokana na umasikini lakini kupata chakula cha kutosha.

Awali akizungumza na watafiti hao kutoka COSTECH, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru Mwanza na Maruku mkoani Kagera kabla ya kwenda kutembelea mashamba darasa na kufanya uzinduzi huo kwenye wilaya hiyo ,Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo,  Dionis Myinga ameishukuru COSTECH na OFAB kwa kusaidia kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wakulima kwa kuwapelekea mbegu hizo bora ambazo zinajibu changamoto mbalimbali sugu za wakulima.

Myinga alisema sio wataalamu hao wametembea umbali mrefu kutoka Dar es salaamu hadi Geita ili kufikisha matunda ya utafiti kwa wakulima hivyo wilaya yake itafanya kazi bega kwa bega katika kuhakikisha malengo ya mpango huo yanafikiwa ili kuchochea uzalishaji wa mazao hayo kupiti mashamba darasa hayo.

“Tafiti zipo nyingi sana kwenye vituo vya utafiti na vyuo vikuu lakini zinabaki kwenye makabati tuu na hazitumiwi kwenye kutatua tatizo lililokusudiwa lakini kila utafiti ungefika kwa mlengwa naamini Tanzania tungekuwa mbali sana kwenye mambo mbalimbali hususani kilimo” alisema Myinga.

Katika kuonyesha kuridhika kwake na maelezo ya mbegu za mahindi na mihogo iliyoletwa kwenye wilaya yake akaomba  mbegu za kununua za mihogo hiyo aina ya Mkombozi za kutosha kupanda shamba la ekari kumi ili iwe mfano kwa wakulima wilayani humo pamoja na kuwa chanzo cha kusambaza mbegu nyingi kwa wakulima wengi zaidi.

Vijiji vilivyonufaika na uanzishwaji wa mashamba darasa katika wilaya hiyo ni Kijiji cha Msasa na Kabagole ambapo mashamba hayo yatasimamiwa na vikundi.

Watafiti hao kesho siku ya Ijumaa wanatarajia kwenda Halmshauri ya Mji wa Buchosa Sengerema kwa ajili ya kazi ya kuanzisha mashamba darasa na kisha wiki ijayo kwenda kumalizia  kazi ya kusambaza mbegu hizo Mkoa wa Tabora.



No comments: