Thursday, November 16, 2017

Wakulima 206 Wapata Mafunzo Ya kilimo Cha Chai kutoka NOSC

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Njombe Bwana Lameck Noah(wapili kushoto) akikabidhi cheti bwana Thiemo Msewa(kulia) katika hafla ya kufunga mafunzo kwa wakulima wa chai(farmer field school) mkoani humo yaliyoratibiwa na Kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe(NOSC). Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wakulima katika kilimo cha chai na mazao mengine. Wapili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NOSC, Bwana Filbert Kavia. Watatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi.Ruth Msafiri 
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Njombe Bwana Lameck Noah akizungumza jambo wakati wa hafla hafla ya kufunga mafunzo kwa wakulima wa chai(farmer field school) mkoani humo yaliyoratibiwa na Kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe(NOSC). Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wakulima katika kilimo cha chai na mazao mengine. 
Operation Director wa Wood foundation Tanzania Bwana Mathew Ng’enda(watatu kushoto) akishangilia mara baada ya wakulima kuwasilisha mada mbalimbali juu ya elimu ya kilimo cha chai (farmer field school) waliyoipata kutoka Kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe(NOSC). Kulia ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Njombe Bwana Lameck Noah. na watatu kulia ni Mkurugenzi mkuu wa NOSC Bwana Filbert Kavia. 


KUTOKANA na ushirikishwaji wa wakulima wadogo katika zao la chai kupitia Kampuni ya Kuhudumia Wakulima Wadogo Njombe (NOSC), viongozi wa Mkoa wa Njombe wanajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kilimo cha chai kilichosaidia kuinua kipato cha wakulima wadogo na kuongeza fedha za kigeni.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Njombe, Bwana Lameck Noah kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Bw. Christopher Ole Sendeka mkoani hapa jana katika mahafali ya mwaka mmoja kuhusiana na mafunzo ya kilimo cha chai kilichohusisha wakulima zaidi ya 206.

“Katika mkoa wetu tulijiwekea utaratibu kuwa kila mkulima alime mazao ya aina mbili ya chakula na biashara, kwa upande wa chai tatizo lilikuwa ni aina ya miche, ilikua inachukua muda mrefu kukua lakini tunaishukuru NOSC imetuletea mice inayokua kwa miezi 12 mkulima anaanza kupata majani mabichi ya chai,” alisema Bw. Noah.

Alibainisha kuwa elimu hiyo ina maana kubwa kwa mkoa wake kwa sababu itawasaidia kulima kisasa na kuwaongezea kipato wananchi wa mkoa huo, lakini pia viwanda vitapata malighafi hiyo muhimu kwa ajili ya soko la ndani na nje.

“Tunafahamu chai inapendwa na mataifa ya magharibi, zao hili lina fedha nyingi za kigeni. Soko la chai lipo na tunawahakikishia wakulima serikali inahangaika kupata mnada wa chai katika ukanda huu badala ya kufanyika Mombasa nchini Kenya.

“Elimu kwa wakulima kupitia huu mfumo ni suala zuri kwa kuwa wakulima watakua na kilimo endelevu waliofundishwa watawafundisha wenzao ili kupata mafuno mazuri na mazao yenye ubora, tunafahamu katika eneo hili kuna kiwanda cha Uniliver kinakaribia kukamilika maana yake watahitaji majani mengi ya chai ili kulisha kiwanda. Wakiendelea kulima zaidi tutawavuta wawekezaji wengi zaidi katika mkoa wetu ili kufikia azama ya serikali ya viwanda,” alisema Bw. Noah.

Mkurugenzi Mtendaji wa NOSC, Bwana Filbert Kavia alisema utaratibu wa kuwafundisha wakulima shambani watajitahidi kuusambaza katika maeneo mengine ya nchi ili wafundishwe wakulima wa mazao mbalimbali kwa lengo la kupunguza tatizo la maofisa ugani.

“Tulianza na vikundi vinane na tutaendelea na vikundi vingine mwakani, huu utaratibu ni mzuri kwa sababu unampa fursa mkulima kujifunza kwa vitendo, kwa kawaida wakulima huelewa zaidi kwa kuona shambani.

“Vilevile nchi yetu ina uhaba wa maofisa ugani, hawa wakulima watawafundisha wakulima wenzao, kama eneo linahitaji maofisa ugani 20 wanaweza kutumika chini ya hapo. Tunaamini kwa sasa tutapata mavuno mengi na yenye ubora kwenye chai baada ya mafunzo haya,” alisema Bw. Kavia.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzie Bw. Thiemo Msemwa alisema: “nashukuru kwa kupewa cheti cha mklulima bora wa chai, nimefurahia mafunzo haya ya kilimo endelevu na kanuni kumi za kilimo endelevu na hata wananvu ninapowaambia waje kwenye shamba la chai wanafurahi kuja shambani kwa sababu kuna mambo mengi ninawafunza.”

Mafunzo hayo yamedhaminiwa na mpango wa Chai Project kwa lengo la kusaidia viwanda vya chai nchini kwa msaada kutoka The Wood Foundation Africa (TWFA), Gatsby Cheritable Foundation (Gatsby) na UKAID ambapo NOSC imedhamiria kulima chai katika eneo lenye ukubwa wa jhekta 3,800 na kufikia wakulima 4,000.

No comments: