Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
KIKOSI cha Yanga kimeendelea na mazoezi yake leo katika Uwanja wa Uhuru kujiandaa na mchezo wa raundi ya 11 ya ligi kuu Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons ya Jijini Mbeya.
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Chamazi kutokana na mabadiliko yaliyofanya na bodi ya ligi baada ya Uwanja wa Uhuru kuwa na shughuli za kijamii.
Katika mazoezi hayo, mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe aliyekosekana uwanjani kwa kipindi kirefu toka kuanza kwa ligi msimu huu leo amejumuika na wenzake na kufanya mazoezi kikamilifu kwa mara ya kwanza pamoja na wenzake ikiwa ni baada ya muda mrefu.
Kurejea kwa Tambwe katika mazoezi ya pamoja chini ya Kocha George Lwandamina kuna uwezekano kwenye mchezo wa wiki hii akajumuishwa kwenye mchezo dhidi ya TZ Prisons siku ya Jumamosi.
Kocha wa Yanga, Mzambia George ‘ Lwandamina amesema kwamba kati ya majeruhi wake wanne, wengine ni Tambwe pekee amefanya mazoezi ukiachilia kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji, Donald Ngoma nna kiungo Papy Kabamba "Tshishimbi" ambapo alikosa mchezo wa wiki iliyopita dhidi ya Mbeya City.
Lwandamina amesema kwamba inaonekana Tambwe amerudi imara kabisa na leo alionyesha yuko fiti kwa kucheza kwa nguvu na kupiga mashuti ya kusisimua. Tambwe alifanya mazoezi mepesi ya kukimbia peke yake juzi na jana Uwanja wa Uhuru, kabla ya leo kuungana na wenzake kwa program kamili ya mazoezi.
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itaendelea Ijumaa, wenyeji Ndanda FC wakiwakaribisha Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Jumamosi, Yanga wataikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Singida.
Mechi nyingine za jumamosi, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Jumapili Simba SC watakuwa wenyeji wa Lipuli ya Iringa Uwanja wa Azam, Complex na mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment