Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu sifa na taratibu za utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2017/2018. Taarifa hii inalenga kutoa ufafanuzi kufuatia maoni ya baadhi ya wadau kuwa baadhi ya waombaji mikopo wenye sifa wanakosa mikopo ya elimu ya juu.
i. Uyatima: Waombaji ambao wamefiwa na wazazi na hivyo kushindwa kumudu gharama za elimu ya juu. Kwa mwaka huu, waombaji yatima wanapaswa kuthibitisha uyatima wao kwa kuwasilisha vyeti vya vifo vya wazazi wao vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA);
ii. Wenye ulemavu: Waombaji wa mikopo wenye ulemavu wanapaswa kuambatisha barua kutoka kwa Mganga Mkuu wa Wilaya au Mkoa inayothibitisha ulemavu huo;
iii. Uduni wa kipato: Waombaji ambao wanatoka kwenye familia zenye vipato duni, miongoni mwao wakiwamo wale wenye barua za uthibitisho kuwa waliosomeshwa kwenye masomo yao kabla ya kujiunga na elimu ya juu;
Pamoja na sifa/vigezo hivi, kila mwombaji ni lazima awe amepata udahili au kuthibitisha udahili katika taasisi moja ya elimu ya juu ambayo atajiunga kwa ajili ya masomo na asiwe na umri wa zaidi ya miaka 30.Aidha, tunapenda kufafanua kuhusu takwimu za utoaji mikopo kwa mwaka 2017/2018 kama ifuatavyo:
i. Bajeti ya jumla ya mikopo kwa mwaka 2017/2018 ni TZS 427.54 bilioni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 122,623. Fedha hizi zinajumuisha malipo ya ada za wanafunzi wenye mikopo pamoja na fedha za chakula na malazi, vitabu n.k;
ii. Fedha zinazohitajika kwa malipo kwa ajili ya Robo ya Kwanza ya mwaka 2017/2018 ni TZS 147.06 bilioni ambazo tayari Bodi imeshapokea kutoka Serikalini;
iii. Hadi leo, Novemba 6, 2017, jumla ya wanafunzi 29,578 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 96.5 bilioni na fedha zao tayari zimeshatumwa vyuoni ili kuwawezesha kuanza masomo;
iv. Aidha, fedha za mikopo ya wanafunzi wote wanaoendelea na masomo zimetumwa vyuoni ili kuwawezesha kuendelea na masomo.
Kufunguliwa kwa dirisha la rufaa.
Tunapenda pia kuwajulisha waombaji wa mikopo wote kuwa dirisha la rufaa litafunguliwa Jumatatu, Novemba 13, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili. Maelezo ya kina yatatolewa kupitia tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).
Tunatoa wito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafuzi na kuwasilisha kwa Bodi ya Mikopo. Lengo ni kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa rufaa zao ifikapo Novemba 30, 2017.
Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Novemba 6, 2017
No comments:
Post a Comment