Tuesday, November 14, 2017

SERIKALI YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA WADAU WA MCHEZO WA GOLF NCHINI

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Katikati) akiwa amewasili katika Viwanja vya Kili Golf Jumapili Mkoani Arusha  kwa ajili ya kufunga mashindano ya Wazi ya Tanzania Kili Golf Kulia ni Katibu Wake Bw. Andrew Magombana na kushoto ni Bw. Chris Martin Makamu wa Rais wa Umoja wa Golf Tanzania(Tanzania Golf Union).
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kili Golf Bw. Bastiaan Bruins (Kushoto) baada ya kuwasili katika viwanja hivyo kwa  ajili ya kufunga mashindano ya Wazi ya Tanzania Kili Golf katikati ni  Makamu wa Rais wa Umoja wa Golf Tanzania(Tanzania Golf Union) Bw. Chris Martin.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ( wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na waandaji wa mashindano ya Wazi ya Kili Golf Mkoani Arusha.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe  akitoa risala kwa washiriki wa mashindano ya Wazi ya Tanzania Kili Golf katika halfa ya kufunga mashindano hayo jana Mkoani Arusha.
 Mshiriki kutoka Kenya Bw. Edwin Mudanyi  akijiandaa kupiga mpira wakati wa fainali wa mashindano ya Wazi ya Tanzania Kili Golf jana Mkoani Arusha ambapo  jumla ya washiriki 250 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Afrika ya Kusini na Tanzania walishiriki.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe  akimpa mkono wa hongera mmoja wa washindi wa kwanza Bw. Victor Joseph kutoka Tanzania baada ya kumalizika kwa mashindano ya Wazi ya Tanzania Kili Golf jana Mkoani Arusha.(Picha na Lorietha Laurence-WHUSM).

Na Lorietha Laurence- WHUSM, Arusha.
Serikali imeahidi kushirikiana kwa ukaribu na wadau wa mchezo wa Golf nchini katika kuhakikisha mchezo huo unafundishwa kuanzia ngazi ya chini ili kuandaa wachezaji bora wa kimataifa wataoiwakilisha nchi katika mashindano hayo duniani.
 Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akifunga mashindano ya Kili Golf Mkoani Arusha ambapo ameeleza kuwa mchezo huo ni wa muhimu  ukazingatiwa katika kukuza sekta ya michezo.
“Mchezo huu wa Golf ni mzuri sana kwa kuwa unakusanya watu wa tamaduni mbalimbali na kuwaleta pamoja nami naahidi kuwa Wizara yangu itahakikisha inashirikiana kwa karibu na wadau wa Golf nchini ili kuukuza zaidi” amesema Mhe. Dkt. Mwakyembe.
Mhe. Dkt. Mwakyembe ameongoza kwa kuwataka washiriki wa mchezo huo kuwa mabalozi wazuri katika kuutangaza mchezo huo ndani na nje ya nchi na kuhamasisha vijana wengine kuwa na moyo wa kujifunza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kili Golf Arusha Bw.Bastiaan Bruins amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuhakikisha mchezo huo unafahamika kwa watu wengi na kuondoa dhana iliyojengeka kuwa ni mchezo wa kitajiri.
“Mashindano haya ni kuwapa hamasa watanzania kuupenda,kujifunza na kuelewa mchezo huu wa Golf ambao ni mchezo rahisi sana na unachangamasha akili huku ukiwaleta watu kutoka sehemu mbalimbali kuwa kitu kimoja” amesema Bw.Bruins.
 Kwa upande wa washiriki wa mashindano hayo hususani kutoka nje ya Tanzania wamewashukuru waandaaji na watanzania kwa ukarimu, upendo,ushirikiano  na umoja waliouonyesha huku wakiahidi kushiriki tena mashindano mwakani.
Mashindano ya Wazi ya Kili Golf Tanzania yalifunguliwa rasmi Novemba 10 mwaka huu yakiwa na jumla ya washiriki 250 kutoka nchi za Malawi,Zambia, Afrika ya Kusini, Uganda , Kenya na wenyeji wao Tanzania huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na washindi wawili baada ya kutoka sare katika mchezo wa mwisho ambao ni Bw. Edwin Mudanyi kutoka Kenya na Bw. Victor Joseph kutoka Tanzania.

No comments: