Wednesday, November 15, 2017

NAMTUMBO KUANZISHA TAMASHA LA MUZIKI KUCHANGIA UJENZI WA KITUO CHA REDIO YA JAMII NAMTUMBO

Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma katika harakati yake  ya kuhakikisha wanajenga kituo cha Redio ya jamii katika Halmashauri hiyo  imepanga kuanzisha Tamasha la muziki kwa lengo la kupata fedha kujenga kituo cha Redio.

Kamati ya uanzishwaji Redio katika Hamashauri hiyo imependekeza kuundwa kwa kamati ndogo itakayoratibu kuanzishwa kwa Tamasha la muziki kwa lengo la kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha Redio.

Aidha mwenyekiti wa kamati ya uanzishwaji Redio ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Bwana Gwakisa Mwasyeba ambaye ni Afisa mipango wa Halmashauri hiyo alipendekeza majina ya kamati hiyo kuwa ni James komba Afisa utamaduni wa wilaya hiyo , Afisa manunuzi Robert Mahili, Abbas Masawe katibu wa mikutano ya madiwani , na Afisa michezo John Ligoho na kuwataka kuanza mikakati ya kuanzishwa kwa Tamasha hilo la muziki.

Hata hivyo kamati ya uanzishwaji Redio ya Halmashauri hiyo ilipendekeza Hadidu Rejea kwa kamati hiyo ndogo ili zianze kushughulika nazo na kutoa taarifa kamili kwenye kamati kuu ya uanzishaji Redio .

Hadidu rejea ilizotoa kamati ya uanzishaji Redio kwa kamati ndogo ya uanzishwaji tamasha la muziki ni pamoja na kamati hiyo ifuatilie Gharama za kuwaleta wasanii mkoani Ruvuma na aina ya wasanii wanaokubalika kwa sasa katika jamii, wafuatilie pia upatikanaji wa muziki na jukwaa kwa ajili ya wasanii,Muda sahihi wa kufanya tamasha na namna ya kufanya matangazo kwa jamii ili jamii ijitokeze kwa wingi katika tamasha hilo pamoja na kuwasilisha mapendekezo ya uwanja wa kutumia.

Aidha mwenyekiti wa kamati ndogo ya Tamasha aliiambia kamati ya uanzishwaji Redio kuwa kamati yake itafanya ziara mjini songea nakufanya mahojiano na waliobobea na maswala ya matamasha mjini songea pamoja na wadau wengine wa muziki na kutoa taarifa katika kamati ya uanzishaji Redio ya Halmashauri hiyo.

Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo inahitaji kukusanya shilingi milioni 104 ili kukamilisha zoezi zima la uanzishwaji wa kituo cha Redio ikiwa ni gharama za uagizaji wa vifaa , ,utengenezaji wa studio,gharama zinginezo kama utengenezaji wa thamani za ofisi kama meza,kabati na viti vya ofisi ambapo kwa jumla yake inafikia kiasi cha shilingi milioni 104.

Pamoja na mikakati hiyo Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo itawaomba wadau kuweza kushiriki katika tamasha hilo kwa lengo la kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha Redio ambacho kitakuwa ukombozi mkubwa katika Halmashauri hiyo na wilaya kwa ujumla wakati utakapofika.

No comments: