NA ESTOM SANGA- DODOMA
Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Huruma Mkuchika amesema serikali itaendelea kuunga mkono mchango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF katika kutatua kero zinazowakabili wananchi katika kupambana na umasikini ili vita hiyo iwe endelevu .
Mheshimiwa Mkuchika amesema jambo muhimu kwa TASAF ni kuhakikisha kuwa walengwa wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wanafikiwa na kunufaika na huduma za mfuko huo huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili mema katika utendaji kazi wa wadau wote wanaohusika na utekelezaji wa Mpango huo .
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF zilizowasilishwa kwake na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga mjini Dodoma, Waziri Mkuchika ameuagiza uongozi wa TASAF kuhakikisha kuwa unawatumia kikamilifu Maafisa maendeleo ya Jamii walioko katika maeneo mbalimbali nchini kuhamasisha shughuli za maendeleo na kupambana na umasikini.
“tunao maafisa maaendeleo ya Jamii nchini kote,lakini nina wasiwasi na namna wanavyotumiwa katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi,naagiza TASAF mtumie vizuri hazina hiyo ya wataalamu katika utendaji kazi wenu” ameagiza Waziri Mkuchika.
Aidha Waziri huyo ameitaka menejimenti ya TASAF kuhakikisha kuwa inaandaa mipango thabiti katika utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kipindi kirefu huku akisisitiza kuwa walengwa wa Mpango huo wanapaswa kuwekewa mazingira yatakayowawezesha kujitegemea hata baada ya kuondolewa kwenye shughuli za Mpango.
Akitoa taarifa ya utekelezaji,Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga amesema mfuko huo umeendelea kuwajengea msingi wa kujitegemea walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya Masikini nchini kote,kazi ambayo amesema imefanyika kwa mafanikio makubwa.
Walengwa wengi hivi sasa wameweza kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi kwenye maeneo yao huku akitaja mafanikio makubwa katika utekelezaji wa masharti ya elimu na afya kwa walengwa jambo ambalo amesema linaendelea kusaidia juhudi za serikali za kupambana na adua ujinga na maradhi.
“Kumekuwa na mwitikio mkubwa katika kuwapeleka watoto kutoka kaya masikini kupata elimu na huduma za afya, kwani hayo ni miongoni mwa masharti ya Mpango, na hyo kwetu ni mafanikio makubwa” amesisitiza Bwana Mwamanga.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amesema mfuko huo kwa sasa unakabiliwa na changamoto ya kufikia takribani asilimia 30 ya vijiji ambavyo havikufikiwa katika awamu inayokaribia kukamilika, hivyo jitihada zaidi zinafanywa ili kupata fedha za kukamilisha vijiji hivyo katika awamu itakayofuata.
Mheshimiwa Mckuchika akitazama nakala za vipeperushi,taarifa na majarida yenye taarifa za utekelezaji wa shughuli za TASAF,Ofisi kwake mjini Dodoma.
Waziri Mkuchika (aliyevaa suti nyeusi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa TASAF na Utumishi wa Umma ,baada ya kupata taarifa za utekelezaji wa shughuli za TASAF ofisini kwake mjini Dodoma, aliyevaa Kaunda suti ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,Mhe. George Mkuchika (aliyevaa tai nyeusi) akipata maelezo kutoka kwa mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislau Mwamanga,ofisi kwa Waziri mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment