Monday, November 13, 2017

Lulu kutumikia miaka miwili jela


 Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

Leo Novemba 13, 2017 Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam, imemuhukumu msanii maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya bila kukusudia ya msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba.

Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Sam Rumanyika ambaye amesema, ameridhika na ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashitaka na wazee wa baraza waliotoa maoni yao kuwa kweli mshtakiwa Lulu aliuwa bila ya kukusudia.

Alisema  Aprili 12, 2012 ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa Lulu kufikishwa Mahakamani ambapo alifikishwa katika mahakama ya mkoa wa Dar es Salaam, ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kujibu tuhuma za mauaji ya marehemu Kanumba. Lakini baadae baada ya kusota rumande kwa takribani miezi kumi, Lulu alibadilishiwa mashitaka na kushitakiwa kwa mauaji ya bila kukusudia, shtaka lililomuwezesha kuwa nje kwa dhamana hadi leo.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Rumanyika amesema, kesi hiyo imejikita katika ushahidi wa mazingira na kwamba mshtakiwa mwenyewe alikubali kwamba yeye ndio alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemeu Kanumba ambaye alikuwa ni mpenzi wake kwa miezi minne . Alisema ili kuthibitisha kesi hii ni watu wawili pekee ndio wenye uwezo huo ambao ni mshitakiwa na marehemu.

‘’Kwa sababu hiyo, mshitakiwa anatakiwa kutoa maelezo ya kina yanayojitosheleza na akishindwa kufanya hivyo ataonekana kwamba yeye ndiye muuaji. Ushahidi wa mazingira unaweza kutumika kama msingi pekee endapo utaendelea kumnyooshea kidole mshitakiwa,’’ alisema Jaji Rumanyika.
Alisema maelezo aliyoyatoa mshitakiwa yanakidhi viwango na vigezo kwa kuwa alikubali kwamba walikuwa na mzozo na kupigwa. Alisema ‘’kwa maoni yangu kuanguka au kudondoka kwa mtu mmojawapo katika ugomvi atakuwa amesukumwa au kumkaba mwenzake.’’
Alisisitiza  kuwa mshitakiwa anajukumu la kutoa maelezo ya kutosha kuhusu tukio lililotokea na kwamba alijikanganya wakati akitoa utetezi wake.

 Alieleza  kuwa Lulu aliiambia mahakama marehemu Kanumba  alikuwa amelewa na desturi ya mlevi mara nyingine huanguka, lakini yeye alieleza kuwa aliburuzwa na kurudishwa chumbani hivyo kama alikuwa mlevi hakueleza kama wakati wanakimbizana alianguka.

Pia alisema maelezo yaliyotolewa na Josephine Mushumbuzi yanaacha maswali mengi kwa sababu hayana hadhi ya cheti cha daktari na kwamba Daktari Paplas Kagaiga ndiye aliyethibitishwa na mshitakiwa mwenyewe pamoja na mdogo wa marehemu, Seth kuwa ndiye daktari  wa familia na kwamba ndiye aliyepaswa kujua historia ya marehemu ikiwemo afya na maradhi. Hata hivyo, mshitakiwa kwa kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi alitazamiwa  ajue maradhi ya marehemu lakini kwenye utetezi wake hajaeleza.

‘’Maelezo yake yanakinzana na hekima ya kawaida kwa sababu hata pale marehemu alipokuwa akimpiga na kumtishia kumuua kwa panga hakuthubutu kufanya chochote, kumsukuma wala kumrudishia bali alichukua taratibu zile za kibiblia kwamba akupigae shavu la kulia mgeuzie na la kushoto,’’ alisema na kuongeza;
‘’Akiwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu hakutoa maelezo ya kina na ya kutosheleza ni kitu gani kilitokea hadi kukutwa na mauti,’’alisema.

Jaji Rumanyika alisema wakati tukio linatokea mshitakiwa alikuwa mtoto wa miaka 17, lakini alikubali kuitwa mke. Alisema mtoto wa umri kama wake ambaye ameweza kuyafanya ya watu wazima sio mmoja wa wale watoto waliolengwa kulindwa na sheria ya watoto hivyo kwa maoni yake, kuwa mtoto wa umri na kuweza kufanya kama alichofanya Lulu halafu akakingwa na sheria ya watoto basi, tutegemee watoto wengi kufanya hayo na kujikinga na mwamvuli wa utoto.

Alifafanua kuwa watunzi wa sheria ya watoto walikuwa na maana ya umri na sio ukomavu kama amesherehekea sikukuu za kuzaliwa ngapi,kukua na kuzeeka ni jambo moja na ukomavu ni jambo lingine.

‘’Kama wanasheria na majaji wataendelea kuwa na fikra na mawazo yaliyosimama huku jamii ikiwa inaendelea kwa kasi, basi watashindwa kuonesha kwa vitendo utawala wa sheria nami sitaki kuwa wa kwanza,’’ alisema.

Pia alisema mahakama ikiacha kufanya yale ambayo sheria hazijaruhusu, lazima jamii isiyokuwa na maendeleo kisheria.

‘’Hivyo ninajiridhisha kuwa kifo cha marehemu kimetokana na ugomvi ndio maana mshitakiwa alishitakiwa kwa kosa la mauaji bila kukusudia. Mshitakiwa alisema marehemu alikuwa na wivu uliozidi mipaka ambao haukuwa na maana lakini hakuna mchezo usiokuwa na kanuni na katika mapenzi wivu ni moja ya kanuni zake,’’ alisisitiza Jaji Rumanyika.

Alieleza kuwa kama Lulu alishajiingiza katika mapenzi huku akifahamu kwamba marehemu alikuwa na wivu kumbe hata alivyoanza kumshuku kwa simu, alitakiwa aachane nayo ili kuepusha ugomvi lakini yeye aliamua liwalo na liwe.

Alisema, kuna wivu wa maendeleo ambao huzaa maendeleo lakini wivu wa mapenzi huleta maangamizi. Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali, Faraja George alidai hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya Lulu, lakini kwa vile mashitaka hayo yamehusisha uhai wa mtu, mahakama itoe adhabu stahiki dhidi ya mshitakiwa.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai mshitakiwa anategemewa na familia yake ambao ni mama na mdogo wake, pia ni balozi wataasisi mbalimbali ambazo zinamuwezesha kiuchumi.
Pia alisema ataangaliwa kwa macho dhihaka na jamii inayomzunguka na kwamba Lulu amebadilika tangu tukio lilipotokea hivyo anaamini ataendelea kubadilika endapo atapata kifungo cha nje, hivyo aliomba asipewe adhabu kali.

Katika kesi hiyo, ambayo Lulu anadaiwa kumuua Kanumba Aprili 7, 2012 maeneo ya Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, upande wa serikali uliwakilishwa na Mawakili, Faraja, Yusuph Abood na Batilda Mushi huku upande wa utetezi uliwakilishwa na Kibatala na Omary Msemo.

No comments: