Thursday, November 9, 2017

KIGAMBONI KINARA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akizungumza na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Mikoa na Halmashauri nchini kabla ya kutoa Tuzo kwa Mikoa na Halmashauri zilizofanya vizuri katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.
  Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga akizungumza na Maafisa maendeleo ya Jamii katika siku ya ufungaji wa Mkutano wa 12 wa Wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii  na kuwasisitiza kuwajibika na kujituma katika kuleta  maendeleo katika maeneo yao.
 Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni Bi. Mwajuma Magwiza akitoa neno la shukurani kwa mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) na kuahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa katika Mkutano huo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akimkabidhi tuzo kwa Afisa Maendeleo ya Jamii Kutoka Mkoa wa Dar es Salaam Bi.Esterine Sephania kwa niaba ya Halmashauri ya Kigamboni iliyoibuka kinara wa uwezeshaji wanawake kiuchumi kupitia mchango wa asilimia 5 katika mfuko wa maendeleo ya wanawake. 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo(katikati) na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na watoto Bibi. Sihaba Nkinga(wa tano kushoto mstari wa chini) wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Mikoa na Halmashauri nchini, mara baada ya kufungwa kwa Mkutano wa 12 wa Wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii ulioambatana na utoaji Tuzo kwa Mikoa na Halmashauri zilizofanya vizuri katika kuwawezesha wanawake kiuchumi. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
  

Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni imekuwa kinara wa kuwawezesha wanawake kiuchumi katika vikundi vya uzalishaji mali katika halmashauri zao.

Hayo yamebainika katika utoaji wa tuzo kwa Mikoa na Halmashauri zilizofanya vizuri katika kuwawezesha wanawake kiuchumi katika kwa kutenga asilimia tano (5) katika Bajeti ya mapato ya Halmashauri katika  Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kiuchumi fedha inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.

Akitoa tuzo hizo Mjini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewapongeza washindi wote waliofanikiwa kutekeleza mpango wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwatengea asilimia 5 katika Bajeti ya mapato ya halmashauri.

Ameongeza kuwa njia pekee ya kufikia maendeleo ya uchumi wa viwanda ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kwani wengi wao wanashiriki katika shughuli za kijasilia mali ambazo zinawapa uwezo wa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo. 

Mhe. Jafo amesisitiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kujituma katika maeneo yao na kuleta mabadiliko kwa kuamsha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo kufikia uchumi wa viwanda.

Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Bibi. Sihaba Nkinga amesema kuwa Serikali imedhamilia kuwawezesha wanawake kiuchumi na wao kama wasimamizi wa Sera watahakikisha wanafuatilia utekelezaji wake katika ngazi za Mikoa na Halmashauri.

“Tumejipanga kuwawezesha wanawake kiuchumi ambao watasaidia kuiwezesha jamii nzima kupitia shughuli zao za maendeleo kuelekea kufikia uchumi wa viwanda” alisema Bibi Sihaba.

Aidha Bibi Sihaba amewataka maafisa maendeleo kutumia weledi katika kusimamia uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika ngazi ya halmashauri kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu katika kushirikiana kuwezesha wanawake kiuchumi ili kusaidia taifa kufikia azam ya uchumi wa kati na viwanda .  


Kwa upande wake Mwakilishi wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Kinondoni Bi. Mwajuma  Mwagiza ameishukuru Serikali kwa kuwezesha wananchi kiuchumi na kuahidi kuendelea kuhamasisha wanawake kujiunga katika vikundi vya ujasiliamali ili kuwezesha kuleta maendeleo katika maeneo yao kufikia uchumi wa viwanda. 

Tuzo hizi za vinara wa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi zimetolewa kwa Mikoa na Halmashauri kumi zikiongozwa na vinara Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni itasaidia kuleta chachu ya mabadiliko katika kuwawezesha wanawake kiuchumi Tanzania.

No comments: