Wednesday, November 1, 2017

EASTAFAB Kibwebwe kinachopigia chapuo Sanaa EAC

KADRI siku zinavyokwenda mbele, wadau wanaoguswa na sanaa hapa nchini wanasaka namna ya kusaidia tasnia hiyo ambayo ni eneo adhimu kwa jamii duniani. Mara nyingi wasanii wamekuwa wakilalamika kwamba wanafanywa kama yatima ambao wanakosa msaada wa kuwasogeza katika njia ya maendeleo baada ya kufanya kazi zao kwa ufanisi. Wasanii hulalamika katika matukio mbalimbali ya kazi zao, hali ambayo husababisha kuonekana kwamba tasnia hiyo sio eneo la kukimbilia kwa sababu ya malalamiko kutoka kwa baadhi ya wasanii.

Wasomi wa Sanaa hapa nchini wanaguswa kwa kiasi kikubwa na sanaa za Tanzania ambao wanatekeleza kwa vitendo kazi hizo, Asasi ya East Africa Art Biennale (EASTAFAB) inaguswa na malalamiko, vilio vinavyotolewa na baadhi ya wasanii katika matukio yanayoandaliwa na baadhi ya wadau  wanaoguswa na mdororo wa maendeleo ya kazi za sanaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa EASTAFAB, Dr. Kiagho Kilonzo anasema mguso huo umejikita kwenye kupromoti sanaa za Ufundi  ambazo zina idadi kubwa ya wasanii ambao wakiwemo Wachongaji, Wachoraji, Wasusi, Wafinyanzi na wengineo ambao wanaingia kwenye Sanaa za Ufundi.       

Dr. Kilonzo anasema promosheni hiyo hufanyika kupitia Maonesho ya Sanaa ambayo yalianza tangu mwaka 2003 ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili. Anasema mara zote 7, maonesho hayo ya Afrika Mashariki yamekua yakifanyika jijini Dar es Salaam ambayo pia hushirikisha wasanii wengine kutoka nje ya Afrika Mashariki na kushirikisha wasanii wa Afrika, Ulaya na Amerika lakini mwaka huu limepanua wigo kwa kufanyika katika majiji ya Afrika Mashariki.

Anasema pamoja na kufanyika katika majiji ya Afrika Mashariki pia kutakuwa na semina ya wasanii na matukio mengi yanayoendana na mwenendo wa hali ya sanaa pamoja na masoko ya sanaa.Dr. Kilonzo anasema katika semina hiyo itakayofanyika Novemba 3, kutakuwa na wawasilishaji mada wa nchi za Tanzania (kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania), Revocatus Kundy, Kenya (kutoka Taasisi ya Elimu Kenya), Dr. Jennifer Wambugu na Uganda (kutoka Kituo cha Maendeleo ya Mitaala), Christopher Muganga.


Katika semina hiyo mbali ya watoa mada  kuchanganua mipangilio mbalimbali ya sanaa pia wasanii watajadili hoja mbalimbali zitakazowasilishwa mezani na watoa mada. Dr. Kilonzo anasema pamoja nao katika semina hiyo kutakuwa na wahusika wa masoko ya sanaa hapa nchini ambao ni pamoja na Origenes Uiso (Karibu Art Gallery), Abel Shuma (Alliance Francaise), Tim Amstrong kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Franciscar Shirima-Frankoo Design.


Anasema semina hiyo itafanyika nyumbani kwa Balozi wa Uswiss,  Arthur Mattli Masaki mtaa wa Kenyata Drive jijini Dar es Salaam ambaye pia atazindua maonesho hayo Novemba 4 katika kituo cha Nafasi Art Mikocheni jijini Dar es Salaam huku ufunguzi wa kwanza utafanyika Novemba 2 ambao utafanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Olle Gabriel.

Dk. Kilonzo anasema mgeni rasmi Novemba 3 atakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu, Habib Fent.
Dr. Kilonzo anasema miaka 7, maonesho yalikuwa yakifanyika Nafasi Arts Space, Alliance Francaise, Goeth Institut na Russian Culture Centre.Aidha Dr. Kilonzo ambaye ni mhadhiri wa Sanaa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema maonesho ya mwaka huu  yataanza Novemba 2-22 ambayo yatashirikisha wasanii 100 wa sanaa za Ufundi.
Dr. Kilonzo anasema kuanzia Novemba 28-Desemba 4, maonesho hayo  yatafanyika kwenye ukumbi wa Afrika Mashariki jijini Arusha ambako wasanii wataonesha kazi zao katika ukumbi huo wa Kimataifa.

Anasema baada ya maonesho ya jijini Arusha, yatahamia jijini Nairobi kuanzia Januari 22-28 mwakani huku kuanzia Februari 2-8 yatafanyika jijini Kampala wakati kuanzia Februari 12-18 yatafanyika jijini Kigali na kumalizia jijini Bujumbura kuanzia Februari 22-28. Dr. Kilonzo anawataja wafadhili waMaonyesho haya yamefadhiliwa na GIZ kupitia Asasi ya Incubator for Integration for Development in East Africa (IIDEA) iliyopo Arusha, pamoja na Balozi za Uswizi, Ujerumani, Denmark na Ubeligiji. Wengine ni pamoja na vituo vya utamaduni wa kifaransa (Alliance Francaises) vya Dar es Salaam, Nairobi na Kampala, Taasisi za kifaransa (French Institutes) za Kigali na Bujumbura, kituo cha Nafasi Art Space (Dar es Slaam), Kuona Art Trust (Nairobi), ghala za GoDown na Banana Hill zilizoko Nairobi, pamoja ghala la AKA Gallery lililoko Kampala, Goeth Institut, Swiss Airline na Dow ELEF International ya jijini Dar es Salaam.

Dr. Kilonzo anaweka bayana taratibu za ushiriki  hufanyika kwa mtindo wa kufanya matangazo kwa wasanii wa sanaa za Ufundi na Kamati ya maandalizi ya maonesho hayo wanapitia majina na kuyapitisha majina 100 ya wasanii  watakaoshiriki.
Pamoja na maonesho hayo kushirikisha wasanii wa Afrika Mashriki pia wamefungua milango  na nchi nyingine nje ya Afrika Mashariki ambazo zilishiriki maonesho ya mwaka 2015 ni pamoja na Ghana, Ujerumani, Namibia, Burundi, Msumbiji, Ufaransa, Ubelgiji na Marekani.

Mwaka huu nchi shiriki ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ujerumani, Norway, Ghana, Nigeria, Ubelgiji  na India.
Anasema pamoja na hayo wasanii washiriki wa maonesho hayo wanapata nafasi ya kutangaza kazi zao katika jarida lao ambalo litasambazwa duniani kote.

“Kwa mipangilio hiyo tutakuwa tumewasaidia kwa kiasi kikubwa wasanii wa  Sanaa za Ufundi ambao masoko yao yatafanyika moja kwa moja na wateja katika nchi mbalimbali duniani, hivyo wasanii wajiandae kwa hilo,” alisema Dr. Kilonzo.
Anaeleza kwamba maonesho ya mwaka huu ni tofauti na maonesho yaliyopita kwani mwaka huu wamefanikiwa kupata wadhamini ambao wamewasaidia kufanikisha matukio yote muhimu, tofauti na mwaka 2015 walikuwa na matatizo ya fedha ndio maana walifanya eneo moja la Afrika Mashariki ambalo ni Dar es Salaam.

Dr. Kilonzo anasema katika maeonesho hayo katika kila jiji kutakuwa na makundi ya ngoma za asili yatakayosindikiza maonesho hayo ambayo yatafanikisha kazi zao katika ufunguzi wa maonesho hayo.

Dr. Kilonzo anaweka bayana uongozi unaounda taasisi ya EASTAFAB, ni pamoja na waasisi Profesa Elias Jengo ambaye ni Mwenyekiti  wa Kamati ya maandalizi, Yves Goscinny Mratibu wa Mambo ya Nje, mratibu wa mipango Stephen Ndibalema, Ofisa Habari na Mawasiliano, Boniphace Mkindi na Francisca Shirima Mjumbe wa Bodi.

No comments: