Thursday, November 2, 2017

DC WILAYA YA NYANG'WALE ASEMA BILA YA KUWEPO USALAMA WA CHAKULA NCHINI HAKUNA KITAKACHOWEZA KUFANYIKA

 Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'wale mkoani Geita
 Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita,  Hamim Buzohera Gwiyama (katikati), akizungumza na watafiti wa kilimo kutoka  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Ukiriguru Mwanza, Ilonga mkoani Morogoro na Waandishi wa Habari kabla ya kukabidhiwa mbegu bora za mahindi na mhogo kwa ajili ya kuzipanda kwenye mashamba darasa katika vijiji vinne wilayani humo leo hii. Kulia ni Diwani wa Kata ya Nyugwa, Ndozi Manual na kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fabian Sospeter ambaye alikabidhiwa mbegu hizo na kuhutubia wananchi kwa niaba ya mkuu huyo wa wilaya.
 Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa upandaji wa mbegu katika mashamba darasa uliofanyika Kata ya Nyugwa wilayani humo.
 Diwani wa Kata ya Nyugwa, Ndozi Manual, akizungumza katika uzinduzi huo.
 Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fabian Sospeter, akihutubia wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi, akimkabidhi mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.
 Mtaalamu wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, akiwaelekeza wananchi wa Kata ya Nyugwa jinsi ya upandaji wa mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi kwenye shamba darasa.
 Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter akipanda mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.
 Mtafiti kutoka  Kituo cha Utafiti wa Kilimo  cha Ilonga, mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda akitoa maelekezo kwa wakulima wa Kijiji cha Kakora  jinsi ya upandaji wa mbegu ya mahindi aina ya Wema 2109 yanayostahimili ukame. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Wilaya ya Nyang'wale,Gudala Kija Tabu na katikati ni mkulima wa kijiji hicho.
 Wananchi wa kijiji cha Kakora wakiwa wamesimama mbele ya shamba la mahindi ambalo mahindi yake ni duni kutokana na mimea yake kushambuliwa na wadudu.
 Mkulima Pendo Sangoma akishiriki kupanda mbegu ya Wema katika shamba darasa katika Kijiji cha Kakora wilaya humo. Kushoto ni Ofisa Ugani, David Makabila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
 Watoto, Michael  na Getruda Bundala wa Kijiji cha Kakora wakiwa wamebeba mbegu ya mahindi aina ya Wema wakati wa uzinduzi wa shamba darasa katika kijiji hicho.
 Ofisa Ugani wa Kijiji cha Nyang'wale, akitoa maelekezo kwa watafiti wa kilimo kuhusu masuala ya kilimo.
Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange, akizungumza na viongozi wa Kijiji cha Kanegele, maofisa ugani na watafiti kabla ya kupanda mbegu ya mhogo katika shamba darasa kwenye kijiji hicho. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, Makoye Malikwisha.

Na Dotto Mwaibale, Nyang'wale, Geita

MKUU wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita Hamim Buzohera Gwiyama amesema bila ya kuwepo kwa usalama wa chakula nchini bado kutaendelea kuwepo na changamoto nyingi za maendeleo na kuwa pasipo chakula hakuna kitakachoweza kufanyika.

Hayo yalisema na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter  kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Hamim Gwiyana wilayani humo jana wakati akipokea mbegu bora za mahindi aina ya Wema na mhogo aina ya Mkombozi kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa ya mbegu katika vijiji vya Kakora, Nyang'wale, Kanegele na Nyugwa.

"Bila ya kuwepo kwa chakula cha kutosha hakuna kitu kitakachoweza kufanyika kwani shughuli zote zitasimama hivyo ni muhimu kuhimizana katika kilimo chenye tija kama tunavyo himizwa na wataalamu wetu kutoka COSTECH, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru Mwanza na Maruku mkoani Kagera" alisema Gwiyama.

Alisema usalama wa kujilinda na adui hauna shida kwani mtu anaweza kuandaa jeshi lake la kukabiliana na adui huku akiwa na silaha nzito lakini sio usalama wa chakula ambao unahitaji maandalizi ya kutosha na watu kujituma na kufanya kazi kwa bidii hasa za kilimo chenye tija.

Alisema kukosekana kwa chakula mara nyingi kunachangiwa na tabia za baadhi ya watu kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo hivyo kusababisha mvua kushindwa kunyesha  na maeneo mengi kuwa na ukame.

Alisema katika wilaya yake njaa imechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kuwa watoro na kushindwa kumaliza shule na kuwa kukosekana kwa chakula kwa watu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.


Diwani wa Kata Nyugwa, Ndozi Manual akizungumza kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo aliwata wananchi kuyatunza mashamba darasa hayo kwa kuwa ni mali yao baada ya kuletewa na COSTECH na OFAB na kuwa baada ya kupata mbegu bora wanatarajia kupata mavuno mengi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, alisema kuwa kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha matunda ya tafiti hizo yanawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi ikiwamo ya mahindi yanayostahimili ukame ya Wema 2109 na mhogo zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa. 

Dk. Bakari aliwataka wakulima na maofisa ugani kuyatunza mashamba darasa hayo ili kazi kubwa iliyofanyika isipotee bure na baada ya muda mfupi watarudi kuangalia maendeleo yake.

No comments: