Thursday, October 26, 2017

WIZARA YA MALIASILI, ARDHI NA TAMISEMI KUMALIZA MGOGORO WA MPAKA WA HIFADHI YA NORTH UGALA NA VIJIJI JIRANI

Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kangeme kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo

NA HAMZA TEMBA- WMU- URAMBO, TABORA

Naibu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema Wizara yake itashirikiana na Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa pamoja wa kumaliza mgogoro wa mpaka baina ya Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja wilayani Urambo .

Naibu Waziri Hasunga amesema hayo mkoani Tabora jana wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Akiwa mkoani humo alitembelea eneo lenye mgogoro, akafanya mkutano wa hadhara na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa ajili ya kutafuta majibu ya kutatua mgogoro huo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme, Mkazi wa Kijiji hicho, Ramadhan Rashid alisema wananchi wa vijiji hivyo wanailalamika Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu kwa kusogeza mpaka wa hifadhi hiyo hadi ndani ya ardhi ya vijiji wakati wa uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka. Alisema eneo hilo ni la vijiji hivyo tangu mwaka 1988.

Naye, Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Peter Maiga alisema hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1956 ikiwa na hekta 165,282 huku mipaka yake halisi ikiwa haijabadilishwa. Alisema zoezi la uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka lilizingatia mipaka halisi kwa kutumia mfumo wa GPS.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta akizungumza kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo kwenye mkutano huo, alisema idadi ya wananchi inaongezeka huku maeneo yakiwa hayaongezeki hivyo akaiomba Serikali ione uwezekano wa kuwaongezea wananchi maeneo ya kulima na kuendeshea maisha yao.

Akijibu malalamiko na maombi ya wananchi hao wa Urambo, Naibu Waziri Hasunga alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutatua kero za wananchi sambamba na kuwaletea maendeleo.

“Baada ya kukagua eneo hili na kusikiliza pande zote, tunaenda kukaa pamoja na Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi tuangalie ramani zote zilizopo, Matangazo ya Serikali (GN) na taarifa mbalimbali ili tujiridhishe ni ipi mipaka halali tufikie ufumbuzi wa mwisho, migogoro ya namna hii haiwezi kuisha bila kushirikisha wizara hizi.

“Nawaagiza watendaji wangu kwenye taasisi mshirikiane na wananchi muwaelimishe na mzuie wasiendelee na uharibifu hadi hapo tutakapopata suluhu ya mgogoro huu”. alisema Naibu Waziri Hasunga.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kujiepusha na vitendo vya kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. “Mkiingiza mifugo tukaikuta tutaitaifisha kwa mujibu wa sheria” alisema Naibu Waziri Hasunga.  

Aidha aliwataka wananchi hao kujikita kwenye shughuli za ufugaji nyuki kibiashara kwa kutumia mizinga ya kisasa ambayo huongeza uzalishaji. “Asali ina soko zuri duniani kwa sasa, bei yake ni nzuri, kila mtu afuge tuchangie uchumi wa taifa letu” alisema Hasunga.

Naibu Waziri Hasunga ataendelea na ziara yake ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi katika mikoa wa Katavi, Rukwa na Songwe.
 Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kulia) akijibu kero mbalimbali za wananchi wa kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (katikati) akisikiliza maelezo ya Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kigwa (kushoto) kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (katikati) akiteta jambo Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kigwa (kulia) na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Urambo, Mussa Mohammed (kushoto) kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akikagua ramani ya eneo lenye  mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja alipokagua eneo hilo katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo
 Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta akizungumza katika mkutano huo.
 Mmoja ya wananchi akitoa kero yake katika mkutano huo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kangeme wakimpongeza kwa kumpigia makofi, Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayuko pichani) baada ya kutoa ahadi ya kutatua mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja kwa kushirikisha Wizara ya TAMISEMI na Ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana.

Mkutano ukiwa unaendelea.

No comments: