Friday, October 13, 2017

WIZARA YA AFYA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA MAMA NA MTOTO KUFIKIA 2020

 Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu katikati akiongea na wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali  hawapo pichani wa Wizara ya afya kuhusiana na kuimarisha huduma bora za afya nchini  leo jijini Dar es salaam, wa kwanza kushoto ni Naibu wa wizara hiyo Dkt. Faustine Ndungulile na wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya. Wakati wa kikao chake na wakuu hao.


NA WAMJW-DAR ES SALAAM
WIZARA ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imejidhatiti kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto mpaka kufikia 2020 ili kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto wachanga .

Hayo yamesemwa na Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipokutana na Wakuu wa Idara na vitengo Mbalimbali kwa ajili ya utambulisho wa Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndungulile  katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam.

“Vifo vya wajawazito vimekua tishio nchini hivyo ni lazima tuimarishe huduma za afya ya mama na mtoto ili tufikie malengo ya kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi mpaka kufikia 2020 ili kujenga taifa lenye watu wenye afya bora” alisema Waziri ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa katika kuboresha hilo amewaagiza wakuu wa idara wizara ya afya kushirikiana na mfuko wa bima ya afya nchini(NHIF) kuona kama kuna uwezekano wa kuanzisha bima ya afya kwa wajawazito kwa bei nafuu hadi kufikia Julai mosi 2018.

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa wanamipangilio ya kutokomeza kabisa tatizo la dawa nchini kwa kuweka mpango mkakati kati ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na vituo  vitoavyo huduma za afya  ili kuepuka tatizo hilo lisijirudie mara kwa mara .

Kwa upande wake Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndungulile amesema kuwa ameshukuru kwa kupewa dhamana hiyo na atashirikiana vyema na Waziri pamoja na watendaji wa Wizara hiyo ili kuleta ufanisi na Huduma bora za afya nchini.

“Nitashirikiana na Waziri wangu pamoja na nyinyi watendaji wenzangu katika kusimamia na kutekeleza sera ya afya ili kuweza kutoa huduma bora za afya kwa watanzania wote bila ya kujali rika,jinsia wala umri” alisema Dkt. Ndungulile.


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa wamepokea maagizo hayo amabayo baadhi  wameanza kuyatekeleza na mengine  atawahimiza watendaji wake kuendana na kasi ya awamu ya tano ya HAPA KAZI TU ili kuifikisha nchi katika afya bora.
 Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto Dkt.  Faustine Ndungulile wa kwanza kushoto akiongea na wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali wa Wizara ya afya hawapo pichani kuhusiana na kuimarisha huduma bora za afya nchini  leo jijini Dar es salaam, katikati ni Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu na kulia ni Katibu Mkuu Wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya. Alipokutana na wakuu hao.
 Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali wa Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na watoto wakifuatilia kwa makini maelezo kutoka kwa Waziri mwenye dhamani hiyo  Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake Dkt. Faustine Ndungulile hawapo pichani wakati wa kikao na wakuu wa idara hizo leo jijini Dar es salaam.
 Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali wa Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na watoto wakimpongeza Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndungulile hayupo pichani mara baada ya kuwapa maelezo wakati wa kikao na wakuu wa idara hizo leo katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es salaam.
 Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali wa Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na watoto wakifuatilia kwa makini maelezo kutoka kwa Waziri mwenye dhamani hiyo  Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake Dkt. Faustine Ndungulile hawapo pichani wakati wa kikao na wakuu wa idara hizo leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wa kwanza kulia akiteta jambo na Naibu wake Dkt. Faustine Ndungulile kushoto mara baada ya  kikao na wakuu wa idara hizo leo jijini Dar es salaam.

No comments: