Sunday, October 15, 2017

WASHIRIKI ZAIDI YA 150 WAJITOKEZA KWENYE MAONYESHO YA KIMATAIFA YA UTALII

Na Jumia Travel 

TAKRIBANI wadau 150 wa sekta ya utalii wa ndani na nje ya Tanzania wameshiriki kwenye Maonyesho ya tatu ya Kimataifa ya Utalii (SITE – Swahili International Tourism Expo) yaliyofanyika kuanzia Oktoba 13 mpaka 15 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Maonyesho hayo ambayo yameandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) yamefanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake kwa mara ya kwanza mwaka 2014 ambapo idadi ya washiriki imeonekana kuongezeka kwa kiasi kikubwa na kuvutia mataifa zaidi ya 13 kama vile Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi, Mauritius na Shelisheli.

Maonyesho hayo yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa akiwemo waziri mpya kwenye sekta ya utalii na maliasili nchini, Mh. Dkt. Hamisi Kigwangala.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa maonyesho hayo Makamu wa Rais alibainisha kwamba sekta ya utalii nchini imekuwa na mchango mkubwa kwenye pato la taifa kwani inachangia jumla ya asilimia 17 na hivyo kuifanya mojawapo ya sekta muhimu katika kukuza uchumi wa nchi. Mbali na hapo sekta hiyo inatarajia kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka milioni 1.2 mpaka kufikia milioni 2 kufikia mwaka 2020.

Akitoa ushuhuda wake baada ya kutembelea Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro siku chache zilizopita, ambapo kihistoria sehemu hiyo ndimo yanapatikana mabaki ya binadamu wa kwanza kuwahi kuishi duniani, alisema kuwa Tanzania imebarikiwa kwa kuwa na vivutio vya kitalii vya kila aina ambavyo ni nadra kupatikana sehemu zingine duniani. Kuwepo kwa vivutio vingi kumepelekea kutajwa na taasisi, mitandao na majarida mbalimbali duniani ikiwemo mtandao wa SafariBookings ambao umeitaja Tanzania kuwa ni kinara kwa kutembelewa zaidi na watalii barani Afrika.
Kwa upande wake akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangala alibainisha kuwa ili sekta hiyo iendelee kukuwa na kufikia malengo iliyojiwekea ni lazima kufanyiwa marekebisho, yakiwemo kufungiwa mfumo wa kieletroniki utakaofanikisha uongezaji kasi ya mapato huku akiwatoa hofu watalii juu ya upatikanaji wa vibali vya viza ambapo amesema vitakuwa vikitolewa kwa muda wa nusu saa.

“Kuna changamoto kidogo ya upatikanaji wa viza kwa watalii wanaowasili hususani muda wanaochukua pale wanapofika uwanja wa ndege kusubiria mpaka kuipata. Na hili ni eneo ambalo tunakusudia kuwekeza zaidi na kupitia huu mfumo jumuishi wa mtandao wa mawasiliano wa serikali tutaweza kupunguza muda wa kusubiria kupata viza mara watalii wanapowasili uwanja wa ndege,” alisema na kuhitimisha Waziri huyo mpya wa Maliasili na Utalii, “Na ni eneo ambalo kwa kweli ili kufanikiwa tunakusudia kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kufanya maboresho.”
Jumia Travel ni miongoni mwa wadau wa sekta ya utalii walioshiriki kwenye maonyesho hayo ya kimataifa ya utalii kwa mara ya kwanza ambayo kwa kiasi kikubwa huwakutanisha washiriki wa ndani na kimataifa pamoja.

Akizungumzia juu umuhimu wa maonyesho kama hayo nchini, Meneja Uhusiano wa Umma wa kampuni hiyo inayojihusisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao barani Afrika na duniani, Bw. Kijanga Geofrey amesema kuwa ni fursa kubwa kwa wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kukutanishwa kwa pamoja na kushirikishana shughuli wanazozifanya na namna ya kusonga mbele zaidi.
“Ni mara ya kwanza sisi kushiriki kwenye maonyesho haya ya kimataifa ya utalii na yametupatia fursa kubwa ya kukutana na wadau wengine ambao kwa namna moja ama nyingine shughuli zetu zinahusiana kwa kiasi kikubwa. Sekta ya utalii ina mlolongo wa shughuli nyingi na mojawapo wa shughuli hizo ni malazi, na hapo ndipo Jumia Travel tunapoingia na kurahisisha huduma hiyo kupatikana wakati na muda wowote ili mradi kuwepo na mtandao wa intaneti, aidha kwa kutumia kompyuta, tabiti au simu ya mkononi,” alisema Bw. Geofrey.
“Uwepo wetu hapa umetupatia fursa ya kukutana na wadau ambao tunafanya nao kazi, tunaotamani kufanya nao kazi na wengine ambao wanatusikia lakini hawakuwa wanafahamu namna ya kutufikia. Hivyo basi tumepata fursa ya kukutana nao na kubadilishana mawazo ya namna ya kukuza ushirikiano zaidi ili kuifanya sekta ya utalii ni ya kuvutia zaidi nchini Tanzania hususani huduma za malazi. 

Kwa sababu miongoni mwa jambo ambalo huwakwamisha watanzania wengi kusafiri na kutalii sehemu mbalimbali nchini ni gharama za juu za malazi. Lakini sisi tunataka kuwaaminisha kwamba suala hilo siyo la kweli kwani malazi yapo ya kila aina kukidhi kipato cha kila mtu na siyo kama wao wanavyodhani,” alihitimisha Meneja huyo wa Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel Tanzania.

No comments: