Monday, October 9, 2017

WAENDESHA BODABODA WILAYANI TARIME WAFUNDWA KUSHIRIKI JUHUDI ZA KUTOKOMEZA MIMBA ZA UTOTONI KWA WANAFUNZI WA KIKE.

  Mwezeshaji kutoka ‘Shirika la Save the Children’ Bw. John Komba akitoa mada kwa madereva bodaboda wa Wilaya ya Tarime katika Semina shirikishi ya jamii katika kuwalinda watoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike itakayofanyika kitaifa Oktoba 11, 2017 Wilayani Tarime Mkoani Mara.
 Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la REPSSI Tanzania Bibi. Edwick Mapalala akizungumza na waendesha bodaboda wa wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara katika Semina ya kuelimisha jinsi ya kuwalinda watoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni kuelekea maadhimkisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike itakayofanyika kitaifa Oktoba 11, 2017 Wilayani Tarime Mkoani Mara.
Baadhi ya waendesha bodaboda kutoka Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolea katika Semina ya kuwaelimisha jinsi ya kuwalinda watoto wa kike na mimba za utotoni kuelekea maadhimkisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike itakayofanyika kitaifa Oktoba 11, 2017 Wilayani Tarime Mkoani Mara.


 Na Mwandishi Wetu- Tarime, Mara
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya watoto wa kike hapa nchini wameendesha mafunzo kwa  waendesha bodaboda walioko wilaya ya Tarime mkoani Mara  kuwahamasisha vijana hao  kuunga mkono juhudi za kitaifa za kutokomeza mimba za utotoni kwa wasichana walioko shule ya msingi na sekondari.  

Akieleza malengo ya mafunzo hayo, Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Jamii Bibi Anna Shengweli amebainisha kuwa madreva wa bodaboda ni kundi mahususi katika ulinzi wa watoto wa kike kwani kutokana na shughuli zao wanakutana mara nyingi na watoto wa kike wakiwa katika mazingira hatarishi. 

“Wakiwa katika kazi zao za kila siku bodaboda na wanapishana na watoto wa kike wakitekeleza majukumu yao mbalimbali ikiwemo kwenda na kurudi kutoka shule, kuteka maji visimani, kuchunga mifugo porini, sokoni, stendi ya basi na kadhalika’’ alisema Bibi Anna.

Kwa upande wake mwezeshaji kutoka ‘Shirika la Save the Childern’ Bw. John Komba  amesema kuwa ni muhimu kuwajengea uelewa waendesha bodaboda ili wawe tayari kutambua na kutekeleza wajibu wa kuwaelimisha na kuwalinda watoto wa kike waepukane na vitendo vya ngono wawapo nyumbani, shuleni, njiani, sokoni, mitaani, na katika shughuli za kijamii kwa ujumla.  

“Mafunzo haya yatawasidia waendesha bodaboda kuwa mabalozi wa usalama na ulinzi wa mtoto wa kike ili kupunguza idadi ya wasichana wanaoacha shule kutokana na changamoto ya mimba za utotoni na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao, pamoja na kuwashirikisha katika mtandao wa usalama wa mtoto katika ngazi ya kata na mitaa. Juhudi hizi zikifanyika zitachangia kupunguza tatizo la mimba za utotoni kutoka asilimia 27 hadi asilimia 8 ifikapo mwaka 2022 alisema Bw. Komba.

Naye Mkurugenzi Mkazi Shirika la REPPSI Bibi. Edwick Mapalala amefafanua kuwa mafunzo haya yatasaidia kumwezesha mtoto wa kike aweze kuwa na maisha bora yenye usalama maana atahakikishiwa ulinzi na ndugu wa karibu katika familia, watoa huduma wanaomzunguka mtoto, na jamii yote kwa ujumla.
  
“Mafunzo haya yataimarisha uaminifu wa madreva wa bodaboda kuzingatia umuhimu wa kuzuia na kupunguza matukio ya mimba za utotoni kwa watoto wa kike” alisema Bibi Edwick. 

Aidha Mwenyekiti wa madreva bodaboda wilayani Tarime Bw. Paschal Joseph, ameishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo pamoja na wadau mbalimbali na ameahidi kuwaheshimu, kuwalinda na kuwapa haki sawa watoto wa kike katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla. 

Semina hiyo ya siku moja iliyoandaliwa  na mashirika yautetezi haki za watoto nchini wakiwemo UNICEF, Save the Children, Plan International  Tanzania, REPSSI na CDF na jumla ya washiriki 40 wamehudhuria mafunzo hayo kati ya vijana 1600 wanaojihusisha na uendeshaji wa Bodaboda  wilayani Tarime. 



Mafunzo hayo yamefanyika ikiwa ni moja kati ya shughuli muhimu za maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike 2017 yenye kauli mbiu  inayosema “Tukomeza Mimba za Utotoni Tufikie Uchumi wa Viwanda’.  

No comments: