Thursday, October 5, 2017

Tumieni Wataalam wa Utafiti katika Ujenzi-NHBRA

Mmoja wa wafanyakazi katika Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) akitengeneza vigae vya kuezekea nyumba vilivyofanyiwa utafiti Jijini Dar es Salaam tayari kwa matumizi ya ujenzi wa nyumba.
Ukuta unaofanyiwa utafiti kwa ujenzi wa kutumia tofali mbichi kwa majengo makubwa na nyumba za makazi ulioko katika karakana ya Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) Jijini Dar es Salaam.
Mhandishi na fundi sanifu wa majengo Bw.Hussein Mataka akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani ) kuhusu mashine ya kufyatua tofali iliyoko katika karakana la ofisi hizo Mwenge Jijini Dar es Salaam.
Mhandisi wa ofisi za Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) Bw. Benedict Chilla akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu huduma zinazotolewa na ofisi hiyo mapema wiki hii Jiji Dar es Salaam.
Mashine ya kupima ubora na kiwango cha udongo kwa ujenzi wa nyumba ambayo ni moja ya vifaa bora vinavyopatikana Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) kama inavyoonekana kwenye picha.Picha na Paschal Dotto-MAELEZO


…………


Na. Paschal Dotto- MAELEZO.

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) imewashauri wananchi kufuata maelekezo katika ujenzi wa nyumba za makazi na majengo mbalimbali ili kupata nyumba bora.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mhandisi Benedict Chila alisema kuwa kuna uhitaji mkubwa sana wa utafiti kwa nyumba za makazi kuhusu matumizi bora ya vifaa vya ujenzi kama matofali, kokoto pomoja na mchanga uliobora katika ujenzi.

“kuna uhitaji mkubwa wa tafiti ambazo zitawawezesha watanzania kupata makazi bora yenye kudumu, kwani katika vifaa na huduma zinazopatikana kwetu zinajikita zaidi katika usanifu majengo pamoja na matumizi ya vifaa, kwa hiyo tafiti hizi ni muhimu kwa wananchi wenye mahitaji ya makazi bora”,.alisema Mhandisi Chila.

Aidha Mhandisi Chila alisema kuwa katika kutambua uhitaji wa wananchi NHBRA imetoa mlango kwa jamiii kupata huduma bora kwa kufanya tafiti katika sanifu ya majengo na vifaa vya kutumia katika ujenzi ili kupata makazi bora.

Kwa upande wake fundi sanifu wa Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba bora na vifaa vya ujenzi (NHBRA) Bw. Hussein Mataka alisema kuwa wamejidhatiti katika kutoa huduma bora kwa kufanya utafiti na kutoa bidhaa safi kwa ujenzi wa nyumba za makazi na majengo mengine.

“Tunahitaji watanzania waje kwa wingi na watambue uwepo wa bidhaa zetu kwani ni bora na zinatoa makazi bora kwa sababu zimefanyiwa tafiti za kutosha na kutengenezwa katika kiwango kizuri zaidi kwa matumizi ya muda mrefu”, .alisema Bw. Mataka

Akibainisha baadhi ya bidhaa hizo Mataka alisema vifaa vinavyopatikana NHBRA ni matofali ya kufungamana yanayotengenezwa kwa udongo na kiasi kidogo cha saruji, mashine za kutengeneza matofai hayo, vigae vya kuezekea nyumba na mashine ya kutengeneza vigae hivyo.

Mataka aliongeza kuwa tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanywa na NHBRA zina lengo la kupunguza gharama za ujenzi wa makazi na majengo mengine ya biashara, alieleza baadhi ya tafiti hizo ni utafiti wa kutengeneza frem za milango kwa kutumia zege, utafiti kuhusu matofali yanayofungamana na kuchoma pamoja na vigae vya kuchoma vya kuezekea.

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) ulianzishwa mwaka 2001chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kutoa huduma na kupunguza gharama kwa vifaa vya ujenzi kwa makazi bora.

No comments: