Tuesday, October 24, 2017

TTCL yazindua huduma ya 4G mkoani Shinyanga

Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Zainab Telack amezindua rasmi huduma ya TTCL 4G mkoani Shinyanga, na kuitaka kampuni kutoa huduma bora za uhakika na zenye gharama nafuu ambazo Wananchi wa kawaida watamudu.

Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika jana katika ofisi za TTCL, mkoani Shinyanga na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulu, Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba, viongozi wa vyombo vya usalama, viongozi wa Mkoa na Wafanyakazi wa TTCL.

Akizungumza katika hafla hiyo, Telack ameitaka TTCL kuongeza ubunifu na juhudi katika kutoa huduma ili iweze kupambana na ushindani uliopo kwenye soko la mawasiliano. “Soko la huduma za Mawasiliano limepanuka sana hapa Nchini, Watoa huduma wapo wengi, ushindani mkali ambapo kila Kampuni inabuni mbinu za kujitanga ili kuvutia Wateja kwa ofa na zawadi mbalimbali.

"Tunataka TTCL yetu nayo ifanye hivyo, ishindane sokoni, iongoze kwa kuwajali Wateja na kutoa huduma bora za uhakika, zenye gharama nafuu ambazo Wananchi wa kawaida watamudu. Tunahitaji kuona sababu ya msingi ya kutoka huku tulipo na kurejea nyumbani TTCL” amesema Mkuu wa Mkoa Shinyanga.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba amesema kuwa TTCL imekuja Shinyanga kuwapa suluhisho bora la Mawasiliano, huduma bora, gharama nafuu na za uhakika. 

“Tumewafuata Wafanyabiashara wa Madini na Vito vya thamani, tumewafuata Wafugaji wa mifugo aina zote, Wakulima wa Mazao yote ya chakula na biashara, Wafanyabiashara na Wajasiriamali wa ngazi zote” amesema Bw. Waziri Waziri Kindamba.

Ameongeza kuwa TTCL imeleta huduma ya mawasiliano katika Mkoa wa Shinyanga ili kuongeza ufanisi washughuli za Viwanda, Elimu, Ulinzi na Usalama wa Wananchi kwa ujumla. “Tunataka tuyafikie Makundi yote haya na kuyawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi ili waweze kufikia ndoto na malengo yao pamoja na kuchangia Maendeleo ya Nchi yetu kupitia shughuli zao za kila siku hasa katika kupata taarifa za Masoko na Bei nzuri ya mazao yao. Amesema Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akitoa hotuba katika uzinduzi wa huduma ya TTCL 4G Mkoani humo katika hafla iliyofanyika Oktoba 23, 2017 katika ofisi za TTCL.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu, Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba pamoja na Meneja wa Mkoa wa Shinyanga-TTCL, Abdalah Lugage wakishika bango kuashiria uzinduzi wa huduma ya TTCL 4G Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa TTCL katika uzinduzi wa huduma ya 4G Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akitumia huduma ya TTCL 4G mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu, Afisa na Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba, katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya 4G, mkoani Shinyanga.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya TTCL 4G Mkoani Shinyanga katika hafla iliyofanyika katika ofisi za TTCL, Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu, Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba na Meneja wa Mkoa wa Shinyanga-TTCL wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Mkoa wa Shinyanga.

No comments: