Na Greyson Mwase, Geita
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la
Madini la Taifa (STAMICO) kuwasilisha taarifa zote za gharama za uendeshaji wa
Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD – Biharamulo ili kujiridhisha
pamoja na kuchukua hatua za kisheria iwapo kama kuna taratibu za manunuzi
zimekiukwa.
Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 27 Oktoba, 2017 alipofanya ziara katika mgodi
huo uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera lengo likiwa ni kufahamu shughuli za
migodi ya serikali, binafsi na wachimbaji wadogo.
Alisema kuwa gharama za uendeshaji wa shughuli za mgodi huo zimekuwa ni
kubwa mno pamoja na madeni hali inayopelekea shirika hilo kujiendesha kwa
hasara badala ya kujiendesha kwa faida.
Aliendelea kusema kuwa STAMIGOLD imekuwa ikitumia gharama kubwa sana
katika uendeshaji wa shughuli zake kwa kutumia mashine za kukodi na kutaka
watendaji wa mgodi huo kuwa wabunifu kwa kuibua mikakati mipya kupunguza
matumizi na kuzalisha faida kubwa ili hatimaye waweze kutumia vifaa vyake badala
ya kukodi.
“ Ukiangalia gharama inayotumika kukodi mashine za uchorongaji na uchimbaji
madini na nyinginezo utabaini kubwa sana ambapo kama STAMIGOLD ingejipanga
ingekuwa na uwezo kabisa wa kununa mashine na mitambo yake yenyewe na
kuepuka gharama kubwa za kukodi.
Aidha, Waziri Kairuki alielekeza Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) kwa kushirikiana na menejimenti ya Mgodi wa STAMIGOLD
kuwasilisha mpango wa kibiashara wenye kuainisha gharama za uzalishaji, mapato
na faida.
“ Tunataka kuanzia sasa STAMIGOLD uwe ni mgodi wa mfano wenye kuzalisha kwa
faida Tanzania, badala ya kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Kairuki.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki aliutaka Mgodi wa STAMIGOLD kutumia
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwenye tafiti zake za madini kwa kuwa wakala
huo una wataalam na maabara za kutosha.
Alieleza kuwa kutokana na wakala huo kuwa na uzoefu katika utafiti wa madini ni
muhimu kwa Mgodi wa STAMIGOLD kushirikiana nao kwenye utafiti wa madini
kama njia mojawapo ya kuboresha tafiti zake.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliitaka STAMIGOLD kuwa
wabunifu kwa kufanya utafiti na kubaini maeneo yenye mashapo ya madini ya
dhahabu ili kuwa na miradi endelevu ya uchimbaji madini
Alisema kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini
inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, hivyo inaanza na usimamizi
wa karibu kwa migodi yote inayosimamiwa na serikali, binafsi na wachimbaji wadogo
na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
Balozi Alexander Muganda alipongeza ujio wa Waziri na Naibu Waziri wa Madini
katika mgodi huo na kuahidi kutekeleza kwa wakati maelekezo yaliyokuwa
yametolewa.
Alisema pamoja na mgodi kuwa na changamoto nyingi za kiuendeshaji kama bodi
watahakikisha wanasimamia masuala ya kiutendaji kwa karibu zaidi, kushauri na
kuwasilisha ripoti za mara kwa mara kwa Waziri na Naibu Waziri wa Madini.
Wakati huo huo Waziri Kairuki pamoja na Naibu wake Nyongo, walikutana na
wafanyakazi wa Mgodi wa STAMIGOLD Biharamulo ili kusikiliza kero mbalimbali na
kuzitatua.
Katika kikao hicho Waziri Kairuki ameelekeza Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la
STAMICO pamoja na uongozi wa Mgodi wa STAMIGOLD Biharamulo kuzingatia
maslahi ya watumishi ikiwa ni pamoja na kupata mishahara kwa wakati, kuwa na
bima za afya, kufuata utaratibu wa manunuzi na kuwepo kwa uwazi kwenye
uzalishaji.
Katika kikao hicho ameagiza bodi hiyo, kumsimamisha kazi aliyekuwa afisa
manunuzi, January Kinunda kwa kushindwa kusimamia mkataba wa ukodishaji wa
mashine kwa ajili uchorongaji.
Awali ilielezwa katika kikao hicho kuwa mashine hizo mbili zililetwa kwa dharura
huku zikiwa si mpya ambapo zimekuwa zikiharibika mara kwa mara na kufikia hatua
ya moja kufanya kazi mara moja kwa wiki na kukwamisha uzalishaji katika mgodi
huo.
Uchimbaji wa madini ya dhahabu ukiendelea katika moja ya mashimo
yanayomilikiwa na Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD – Biharamulo
mkoani Kagera.
Kaimu Meneja Uchimbaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD –
Biharamulo, Rashil Rulanga (kulia mbele) akielezea shughuli za uchimbaji
zinavyofanyika katika mgodi huo kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto
mbele) mara alipofanya ziara katika mgodi huo tarehe 27 Oktoba, 2017. Wa pili
kushoto mbele ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Shughuli za utafiti wa madini ya dhahabu zikiendelea katika Mgodi wa Uchimbaji
Dhahabu wa STAMIGOLD – Biharamulo uliopo mkoani Kagera.
Kutoka kushoto mbele ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini
la Taifa (STAMICO), Balozi Alexander Muganda, Waziri wa Madini, Angellah
Kairuki, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya
Biharamulo, Saada Malunde wakiendelea na ziara katika eneo la Mgodi wa
Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD – Biharamulo.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja
Uchenjuaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD – Biharamulo,
Joseph Kamishina (kulia mbele) katika ziara hiyo. Kushoto ni Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akifafanua jambo katika ziara
hiyo.
Kaimu Meneja Uchenjuaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD –
Biharamulo, Joseph Kamishina (katikati mbele) akimwongoza Waziri wa Madini,
Angellah Kairuki ( wa pili kulia) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa
tatu kulia) kuelekea kwenye eneo la uchenjuaji katika mgodi huo.
Kaimu Meneja Uchenjuaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD –
Biharamulo, Joseph Kamishina(katikati) akielezea shughuli za uchenjuaji madini
zinavyofanyika kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) katika ziara hiyo.
Kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Mmoja wa wafanyakazi katika Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD –
Biharamulo, Sara Mkama akiwasilisha kero yake kwa Waziri wa Madini, Angellah
Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ( hawapo pichani) mara
Mawaziri hao walipokutana na watumishi wa mgodi huo kwenye ziara hiyo lengo
likiwa ni kusikiliza na kutatua kero zao.
Sehemu ya watumishi wa Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD –
Biharamulo, wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Madini,
Angellah Kairuki (hayupo pichani).
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo (kulia) wakisikiliza kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na watumishi
mbalimbali wa Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD – Biharamulo
(hawapo pichani).
No comments:
Post a Comment