Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitoa hundi ya Mkopo uliotolewa
na SIDO kwa mjasiriamali Sarah Isaya kutoka Singida katika hafla fupi ya
kukabidhi mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali mkoani hapa.
Mkurugenzi Mtendaji SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji
akitoa nasaha zake kwenye hafla ya utoaji wa hundi za mikopo kwa
wajasiriamali mbalimbali mkoani Singida uliofanyika kwenye viwanja vya
SIDO mjini hapa. Wa kwanza kushoto (aliyekaa) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt Rehema Nchimbi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitazama ubora wa mafuta ya
alizeti na kupata maelezo ya mafuta hayo yanayosindikwa katika viwanda
vya Mkoa wa Singida kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kuzalishaji
Mafuta ya alizeti ya Sunshiwe Oil Mill, Salum Khalifan.
Meneja
wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende akitoa taarifa ya Viwanda Vidogo
vidogo na ujasiriamali Mkoa wa Singida kwenye hafla ya utoaji wa hundi
za mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali. Wa kwanza kushoto (waliokaa) ni
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Mkurugenzi Mtendaji SIDO
Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amelitaka shirika la Viwanda
Vidogo vidogo (SIDO) kuandaa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa
vyuo mbali mbali mkoani hapa ili wakihitimu waweze kujiajiri
Dkt.
Nchimbi ametoa wito huo wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa
mikopo ya SIDO kwa wajasiriamali iliyofanyika kwenye viwanja vya SIDO
ambapo amesema mafunzo hayo yatawajengea mazingira mazuri wahitimu
kujiajiri.
Amesema
Mkoa wa Singida una fursa nyingi za kujiajiri pamoja na kuwa na vijana
wengi hasa walipo katika vyuo mbalimbali lakini hawawekezi katika fursa
hizo kwa kutokujua au kukosa elimu ya kutosha juu ya ujasiriamali, na
hata waliopo vyuoni wakihitimu wanasubiri kuajiriwa badala ya kujiajiri.
Dkt.
Nchimbi amesema ili wananchi wakiwemo vijana waweze kuzitambua fursa
hizo, SIDO Mkoa na wadau wengine wanapaswa kuongeza juhudi zaidi katika
utoaji mafunzo ya ujasiriamali ambapo amewataka wajielekeze kwenye vyuo
mbalimbali.
“Singida
ina kila aina ya fursa ambazo zinaweza kumkomboa mwananchi kiuchumi.
Kwa hiyo hakuna sababu vijana au watu wengine kuukimbia mkoa wao na
kwenda kutafuta maisha katika mikoa mingine. Ni suala la kujipanga na
kupata fursa ya mafunzo kutoka SIDO mkoa”, amefafanua.
Aidha
ameziagiza halmashauri zote na manispaa Mkoani hapa kutangaza fursa,
bidhaa, mazao, na huduma zinazopatikana katika maeneo yao ili kuwasaidia
wajasiriamali kupata soko la uhakika.
“
Halmashauri zote tumieni fedha mnazopata kwenye vyanzo vya mapato ya
ndani muwasaidie wajasiriamali wenu kutangaza kwenye vyombo vya habari,
nina imani na uhakika kuwa mkitangaza bidhaa na mazao yao yatapata soko
na nyinyi halmashauri mtapata mapato yenu”, amesema Dk.Nchimbi.
Awali
Mkurugenzi Mtendaji wa SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji
amesema SIDO imekuwa tegemeo kubwa kwa wajasiriamali hasa katika kutoa
mafunzo na kusaidia teknolojia ya kuongeza thamani ya mazao na
malighafi.
“Mikopo
ya SIDO imeweza kuwasaidia wajasiriamali kuthubutu na kuanzisha miradi
ya usindikaji mara tu baada ya kupata mafunzo. Kundi hili limekuwa na
changamoto ya mitaji kwa kuwa halikidhi na halijaweza kuthubutu
kuzifikia benki kutokana na woga na gharama za mikopo”, amesema.
Mhandisi
Profesa Mpanduji amesema kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 SIDO imeweza
kutoa mikopo 4,464 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7.2.
Mikopo hiyo imetengeneza ajira 11,861 kati ya ajira hizo asilimia 51 ni
wanawake.
Kwa
upande wake Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende amesema kwa
Mkoa wa Singida wametoa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 724.6 kwa
wajasiriamali 693 na vikundi 47. Hali ya urejeshaji wa mikopo hiyo ni
asilimia 98.
Kibende
amesema SIDO wameweza kutoa mafunzo ya wajasiriamali mbalimbali 37 kwa
wajasiriamali 996 ambao kati yao wanawake walikuwa 536 na wanaume 460.
Amesema
baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa wafanyakazi na
ukosefu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango waliyojiwekea ikiwemo
kuendeleza na kuboresha mtaa wa viwanda.
Naye
Mjasiriamali kutoka Kampuni ya Singida Super Quality Oil and Rice mills
Simon Kitundu amezishauri halmashauri na manispaa kutenga maeneo maalum
ya kufanyia biashara wajasiriamali waweze kuondokana na adha mbalimbali
ikiwemo ya kuuza bidhaa zao kwenye madirisha ya mabasi.
No comments:
Post a Comment