Monday, October 16, 2017

SERIKALI KUWATOA SADAKA WATENDAJI WATAKAOZEMBEA UVAMIZI WA MIFUGO TOKA NCHI JIRANI YA KENYA - MPINA NA MWANDISHI MAALUM – KILIMANJARO

Serikali haitaweza kuwavumilia watendaji wazembe katika suala zima la uvamizi wa mifugo hususan ng’ombe kutoka katika nchi jirani ya Kenya.

Hayo yamebainishwa wilayani Mwanga na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina alipozindua rasmi oparesheni maalum ya uvamizi na utambuzi wa mifugo hiyo tokea angani.

Mpina alisema kuwa uvamizi wa mifugo hiyo tokea nchi jirani ya Kenya unaleta changamoto kubwa ya malisho ya mifugo ya ndani ya nchi unaopelekea migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji na husababisha mmomonyoko wa udongo na uharibifu wa mazingira.

Baada ya kupokea taarifa ya timu ya wataalam iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara Mifugo na Uvuvi Dkt Maria Mashingo, iliyofanya oparesheni hiyo maalum kwa kutumia ndege ya shirika la taifa la hifadhi ya wanyamapori, (TANAPA) taarifa iliyobaini kuwepo kwa makundi makubwa ya ng’ombe waliokuwa wakihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kuwepo kwa idadi kubwa ya Maboma, Waziri Mpina alisema ,

“ Haiwezekani ng’ombe wanaingia kwa makundi makubwa hivi nchini na watendaji wa serikali wapo, lazima kutakuwa na shida katika utendaji, Oparesheni hii itakuwa ni ya mwisho, kwa ng’ombe watakaoingia tena watendaji watatolewa sadaka.” Alibainisha Mpina.

“Yawezekana ng’ombe wote 4000 ambao inasemekana walitoroshwa hapo awali wapo, hivyo Oparesheni ianze rasmi tuwakamate ng’ombe wote, tuheshimu sana sheria, na nchi jirani tushirikiane katika mambo tuliyokubaliana kisheria na lolote litakalotokea katika suala hili la uvamizi wa mifugo sheria itachukua mkondo wake na tusilaumiane” Alisisitiza Mpina.

Awali wataalam waliyokuwepo katika oparesheni hiyo maalum waliezeza kuwa mifugo mingi iliyoonekana kutokea angani ilikuwa zaidi katika maeneo ya malisho na maji ya vijiji vya kiti cha Mungu,njiapanda,kirya na kitongoi cha Mangulai.

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilya ya Mwanga imeingia kazini tayari kwa kuanza oparesheni hiyo maalum. 

 Katika picha kikosi kazi maalum cha oparesheni ya angani ya ukaguzi wa uvamizi wa mifugo katika Wilaya ya Mwanga inayotokea katika nchi jirani ya Kenya , mbele ni rubani wa ndege hiyo maalum ya TANAPA Bw. Mark Athumani akiongoza ujumbe huo kupanda ndege katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Kilimanjaro (KIA).

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina akiongea na kikosi kazi maalum kikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Maria Mashingo na Rubani wa ndege hiyo  maalum ya TANAPA Bw. Mark Athumani walipokuwa wakijiandaa kwenda kwenye oparesheni maalum ya angani ya ukaguzi wa uvamizi wa mifugo katika wilaya ya Mwanga wanaotokea katika Nchi jirani ya Kenya.
Waziri Mpina akimpungia mkono Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvivi Dkt Maria Mashingo akiwa na baadhi ya wajumbe wakiingia  kupanda ndege maalum kuanza oparesheni ya ukaguzi wa uvamizi wa mifugo katika Wilaya ya Mwanga wakitokea Kenya.

No comments: