Thursday, October 12, 2017

Puma Energy yaendeleza udhamini wake Rock City Marathon

KAMPUNI ya mafuta ya Puma Energy leo imekabidhi hundi yenye thamani Tsh milioni 25 kwa waandaaji wa mbio za Rock City Marathon ikiwa ni mwendelezo wa kampuni hiyo kudhamini mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Octoba 29 mwaka huu, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akikabidhi hundi hiyo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo Bw Zenno Ngowi, Meneja Mkuu wa  kampuni ya Puma Energy Bw Phillipe Corsaletti alisema udhamini huo unalenga kuunga mkono juhudi za serikali kuhamasisha michezo na utalii wa ndani hapa nchini.

“Michezo huleta uimara wa afya na uimara huo ndio umetufikisha Puma Energy hapa tulipo kimafanikio. Ni wazi ushiriki wa Puma kwenye mbio hizi utawajaza nishati ya nguvu na ubora washiriki wote’’ alisema.

Aliahidi kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo katika kuboresha zaidi mbio hizo kwa miaka ijayo huku akitoa wito kwa  vijana wengi zaidi kutoka mikoa mbalimbali kujiandaa kwa ajili ya mbio hizo.

Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo, Ngowi alisema uwepo wa kampuni hiyo katika kufanisha Rock City Marathon utaongeza hadhi na ubora wa mbio hizo ili ziende sambamba na ubora wa huduma na bidhaa zinazoandaliwa na kampuni hiyo.

Naye, Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Bidan Lugoe  alisema pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 4 kila mmoja, Sh mil 2/-  kwa washindi wa pili na sh. Mil 1/- kwa washindi wa tatu.

Kwa upande wa mbio za  Kilomita 21, Bidan alisema pamoja na medali washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh.  Mil 2/- kila mmoja, sh. Mil 1/-  kwa washindi wa pili na sh. Laki 5/- kwa washindi wa tatu.

“Zaidi tunatarajia kwamba viongozi wa kiserikali pamoja na wadhamini wetu wakiwemo PUMA, Tiper, Precision Air, RedBull,  Bodi ya Utalii Tanzania(TTB), New Mwanza Hotel, EF Out door, CF Hospital, KK Security, Jambo Food, SDS,  watashiriki kikamilifu katika mbio za KM 5 sambamba na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino,’’ alitaja.

Akizungumzia usajili wa mbio hizo Bw. Bidan alisema kwa wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani wanaweza kujisajili kwa kuchukua fomu katika Ofisi za michezo wilaya zote za mkoa wa Mwanza, Ofisi za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga.

Sehemu nyingine ni pamoja na  Uwanja wa Nyamagana,  Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino  Mwanza, Kituo cha michezo  Malya, Shule ya Kimataifa ya Isamilo, New Mwanza  Hotel na Ofisi za EF Out door zilizopo jingo la Rock City Mall.

“Kwa upande wa Dar es Salaam Fomu za ushiriki pia zinapatikana katika ofisi za Kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya sita jengo la SHAMO Tower, Mbezi Beach , jijini Dar es, Salaam na EFM Jogging Club iliyopo Coco Beach  Dar es Salaam” alitaja.

Zaidi kuhusu usajili wa mbio hizo zinazoandaliwa kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA), Bidan alisema unaweza kufanyika kupitia tovuti ya kampuni hiyo ambayo ni www.capitalplus.co.tz

Alitoa wito kwa washiriki zaidi kujisajili ili kuthibitisha ushiriki wao kwenye mbio hizo ambazo mbali na kuibua vipaji vya mchezo wa riadha hapa nchini pia zinalenga kutangaza utalii katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Ziwa.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Puma Energy Bw Phillipe Corsaletti (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh milioni 25 kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio za Rock City Marathon Bw Zenno Ngowi (wa tatu kushoto) ikiwa ni udhamini wa mbio hizo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni pamoja na Meneja Masoko wa Kampuni ya Puma Energy Bw Machumani Shebe (wa tatu kulia) na Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Bidan Lugoe (kulia) 
Meneja Masoko wa Kampuni ya Puma Energy Bw Machumani Shebe (kushoto) akizungumza kwenye warsha hiyo. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio za Rock City Marathon Bw Zenno Ngowi (katikati) akizungumza kwenye warsha hiyo. Pamoja na mambo mengine Ngowi alisema uwepo wa kampuni ya Puma katika kufanisha Rock City Marathon utaongeza hadhi na ubora wa mbio hizo ili ziende sambamba na ubora wa huduma na bidhaa zinazoandaliwa na kampuni hiyo.
Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Bidan Lugoe akizungumza kuhusiana na maandalizi ya mbio hizo ambazo pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 4 kila mmoja, Sh mil 2/- kwa washindi wa pili na sh. Mil 1/- kwa washindi wa tatu.
 

No comments: