Sunday, October 22, 2017

Namba maalumu yazinduliwa kuchangia Mfuko wa Ukimwi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa namba maalumu ya kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi. Wanaoshuhudia kulia kwake ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Godfrey Simbeye. Kushoto kwa Mhagama ni Waziri wa TAMISEMI, Suleiman Jafo na anayemfuatia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Khamis Mwinyimvua.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (katikati) akifurahia pamoja na viongozi wenzake mara baada ya uzinduzi huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akimkabidhi hundi ya sh. milioni 660 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jafo akimkabidhi hundi ya sh. milioni 200 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera ( kulia) kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mererani. 
Mwenyekiti wa bodi wa mfuko, Godfrey Simbeye akizungumza kabla ya uzinduzi wa namba hizo. 
Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk Leonard Maboko akizungumza kwenye tukio hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akitoa hotuba katika tukio hilo.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera akisisitiza jambo baada ya kukabidhiwa hundi yake.
Washiriki wakifuatilia mkutano huo.
Mawaziri wakiangalia namna ya kutuma fedha kwa kutumia namba 0684909090 kwa ajili ya kuchangia mfuko wa udhamini wa kudhibiti Ukimwi. Aliyesimama ni Mkuu wa kitengo cha sheria wa TACAIDS, Elizabeth Kaganda.
Waziri Mhagama (katikati) akiwa katika picha na viongozi wengine.
Mawaziri wakiagana mara baada ya kumaliza uzinduzi wa tukio hilo. Picha na Philemon Solomon
.....

Na Julian Msacky-Nchi yangu Blog.

TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), imezindua rasmi namba maalumu ya kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi. Uzinduzi huo umefanyika Dar es Salaam Oktoba 21, 2017 na kuzinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.

Mhagama alitaja namba ya uchangiaji wa mfuko huo kuwa ni 0684909090 na kwamba kila mwananchi anahimizwa kuchangia ili fedha itakayopatikana isaidie watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi. 

"Leo ni siku maalumu kwa nchi yetu...inaonesha tumeanza kujitegemea kupitia mfuko huu wa udhamini katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi," alisema.

Waziri alisema mfuko huo umeanzishwa kwa Sheria Namba 6 ya Mwaka 2015 na utakuwa unachangiwa na Watanzania wenyewe. 

"Huu ni mfuko wa umma na tunabeba jukumu hilo kama Serikali na lengo kuu ni kuwahudumia Watu wenye maambukizi," alibainisha.

Alisema fedha za mfuko huo zitatumika kununua dawa za septrine ambazo ni maalumu kwa ajili ya kufubaza Virusi Vya Ukimwi na zitatolewa bure. Mhagama alisema takwimu zinaonesha kuna Watanzania milioni 1.4 wanaoishi na VVU na watu 48,000 huambukizwa virusi hivyo kila mwaka nchini.

"Kati ya WAVIU milioni 1.4 wanaotumia dawa ni laki 8, Watanzania kati ya laki 4 hadi 5 hawatumii dawa, hivyo tupunguze utegemezi angalau kwa asilimia 40 ili kudhibiti Ukimwi," alifafanua.

Pamoja na hali kuwa hivyo, Waziri alisema asilimia 94.7 ya Watanzania hawana VVU na Ukimwi na wanahitaji kulindwa ili waendelee kubaki salama. Alisema kulingana na Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (2013/14-2017/18) uliothaminishwa, mahitaji ya taifa ya kugharimia mwitikio wa Ukimwi katika kipindi cha miaka mitano yanakadiriwa kufikia sh. trilioni 6.

"Asilimia 93 ya fedha hizi zinatarajiwa kutoka kwa wafadhili na asilimia 7 kutoka vyanzo vya ndani. Sehemu kubwa asilimia 56 ya fedha zote katika miaka hiyo ni kwa ajili ya kununua dawa," alisisitiza. 

Katika hatua nyingine, Mhagama alikabidhi hundi ya sh. milioni 660 kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa ajili ya kununua dawa aina ya cotrimoxazole za watu wanaoishi na VVU.

Pia alikabidhi hundi ya sh. milioni 200 kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera ili kujenga kituo cha afya Mererani ikiwa ni kuunga mkono ahadi ya Rais John Magufuli kusaidia ujenzi wa kituo hicho.

Viongozi wengine walioshiriki tukio hilo la uzinduzi ni Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, DK Leonard Maboko na Mwenyekiti wa bodi wa mfuko huo, Godfrey Simbeye. 

No comments: