Monday, October 9, 2017

MUHIMBILI YAPOKEA WATAALAMU 16 KUTOKA CUBA.


Na; Agness Moshi na Pascal Dotto-MAELEZO.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imepokea wataalamu 16 kutoka nchini Cuba kama moja ya mikakati yake ya kuboresha utoaji huduma za Afya ikiwemo kutoa huduma za kibingwa hapa nchini.

Akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dk.Mpoki Ulisubisya alisema kuwa Serikali imepokea madaktari bingwa 6, madaktari bingwa wa usingizi 2, madaktari wa wodi za wagonjwa mahututi 2, Daktari bingwa wa  upasuaji wa macho 1, mtaalamu mmoja wa radiolojia pamoja na wauguzi 10 wa vyumba vya wagonjwa mahututi.

“Wataalam hawa mamekuja wakati muafaka, kwasababu kwa kipindi hiki hospitali ya Muhimbili inafanya maboresho ya utoaji huduma , hivyo nina amini uwepo wao hapa kwa miaka miwili, hautakuwa kwa ajili ya  kuboresha huduma au kusaidia wagonjwa tu , bali ni nafasi nzuri ya  kuwapa ujuzi na mafunzo  wataalamu wetu “,alisema Dk.Ulisubisya.

Dk. Ulisubisya amesema kuwa uwepo wa wataalamu hao utaongeza nguvu kazi hususani kwenye utoaji huduma kwa wagonjwa mahututi kwani hospitali hiyo imeongeza vitanda vya wagonjwa mahututi kutoka vitanda 21 hadi 88.

Dk. Ulisubisya ameongeza kuwa wataalamu hao watasaidia kupunguza msongamano kwenye wodi za wagonjwa mahututi pia kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda nje kwa ajili ya matibabu kwani huduma za matibabu zitapatikana hapa nchini.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Prof.Lawrence Museru  amesema kuwa, kutokana na uhaba wa wataalamu kwa kipindi hiki cha maboresho,Hospitali imetafuta wataalamu kutoka Cuba ili kuziba pengo hilo.

Prof.Museru alisema kuwa kwa kipindi chote cha miaka miwili,wataalamu hao watatoa mafunzo kwa wataalamu wa hapa nchini ambao utawapa ujuzi na kuwasaidia katika maeneo ya utoaji huduma kama vile huduma za upasuaji macho,wagonjwa mahututi ,radiolojia ,na usingizi.

Aidha,Dkt.Ulisubisya ametoa wito kwa Taasisi nyingine za Afya nchini,kuiga mfumo unaofanywa na hospitali ya taifa Muhimbili ili kusaidia kupunguza utegemezi serikalini katika kuboresha huduma za Afya.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha  utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kuongeza wodi za wagonjwa mahututi,Ununuzi wa vifaa tiba,kukarabati na kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 13 hadi kufikia 20, pamoja na kukabiliana na changamoto ya rasilimali watu kwa kupelekeka wataalamu nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo.
Katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya(katikati) akieleza jambo wakati wa kuwakaribisha wataalamu 16 kutoka nchni Cuba wakiwemo Madaktari Bingwa 6 pamoja na Wauguzi wa Chumba cha uangalizi maalumu kwa wagonjwa mahutiti mapema leo Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam kushoto ni kiongizi mkuu wa matibabu nchini Tanzania Dkt. Maylen Lopezi na kulia ni Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya taifa Muhimbili Profesa Lawrence Museru.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka Cuba katika hafla ya kuwakaribisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili leo Jijini Dar es Salaam.

No comments: