Friday, October 6, 2017

MFANYABIASHARA MANJI AACHIWA HURU NA MAHAKAMA BAADA YA KUKOSEKANA UTHIBITISHO ANATUMIA DAWA ZA KULEVYA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji jijini Dar es Salaam leo mara baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake yaliyokuwa yakimkabili.Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha amesema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo dhidi yake.
Mfanyabiashara maarufu,Yusuf Manji aliyekuwa anakabiliwa na matumizi ya Dawa za Kulevya akiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akisubiri kusomewa shtaka lake.
 Mfanyabiashara maarufu,Yusuf Manji aliyekuwa anakabiliwa na matumizi ya Dawa za Kulevya akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kusomewa hukumu na kujulikana kuwa upande wa mashtaka hawakuweza kuthibitisha kama kweli alikuwa anatumia dawa za kulevya.
.
 Mfanyabiashara maarufu,Yusuf Manji aliyekuwa anakabiliwa na matumizi ya Dawa za Kulevya akielekea kwenye gari kwaajili ya kuondoka huku akiwa hana kosa mara baada ya kusomewa hukumu  na kuonekana kuwa hakuwa akitumia dawa za kulevya.

 Mfanyabiashara maarufu,Yusuf Manji aliyekuwa anakabiliwa na matumizi ya Dawa za Kulevya akipanda gari akipanda gari mara baada ya kusomewa hukumu ya kesi iliyokuwa ikimkabiri ya kutumia dawa za kulevya ikiwa upande wa mastaka walishindwa kuthibitisha shtaka hilo.
Wakili wa Manji Bi. Hajra Mungula akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu mara baada ya mteja wake kuonekana hana kosa la matumizi ya dawa za kulevya.
Picha na Avila Kakingo,Globu ya Jamii.



Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya kesi yake iliyokuwa ikimkabili ya matumizi ya dawa za kukevya aina ya heroine. Mshtakiwa Manji ameachiwa chini ya kifungu cha sheria Namba 235 cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Hukumu hiyo imesomwa leo mchana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha ambaye amesema ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha makosa kwa mshtakiwa bila ya kuacha shaka.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkeha amesema, kuna baadhi ya kesi zinahitaji zaidi utaalamu kutoka kwenye fizikia na madawa zaidi ya sheria. Amesema kwa utetezi ulivyotolewa unaonyesha kuwa polisi walimsaidia mshtakiwa kupata dawa zake alipokuwa kituoni na hata gerezani.

Manji ni miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watu wanaodaiwa kujihusisha na kutumia dawa za kulevya February 6 mwaka huu na kuwataka walipoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO).

Awali kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulisema ungeleta mashahidi kumi lakini wakaishia kuleta watatu na Manji alisema angeleta mashahidi kumi na tano lakini walileta mashahidi saba tu ambao kupitia hoja za pande zote mbili mahakama imejiridhisha pasi na shaka ya kwamba mshtakiwa huyo hana hatia baada ya upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha kosa lake.

Amesema, ushahidi uliotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo wa Jakaya Kikwete (JKCI),Profesa Mohammed Janabi, daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili na dawa za kulevya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Fransic Benedict na Daktari Mkuu wa Gereza Keko Eliud Mwakawanga umeweza kuisaidia mahakama kwani kesi hiyo iko kitaalamu zaidi ya sheria.

“Madakatari hawa ambao ni wafanyakazi wa serikali, hawakuwa na sababu yoyote ya kutoa utetezi mbaya walifika hapa kwa ajili ya kusaidia kama wataalamu dhidi ya tuhuma hizi na kutokana na utetezi uliotolewa na uoande wa mshtakiwa na ule ushahidi was upande wa jamuhuri namuachia huru mshtakiwa chini ya kifungu cha 235 cha mwenendo wa makosa ya jinai (CPA).” amesema Mkeha.

Akichambua ushahidi wa upande wa utetezi, Hakimu Mkeha amese,a katika ushahidi wa Dk Janabi aliiambia mahakama kuwa alimpokea Manji katika hospitali hiyo na kulazwa kwenye Taasisi ya moyo mwezi February na Julai.na katika uchunguzi wao waligundua moyo wake haujakaa vizuri. 
Ambapo alitibiwa na kuruhusiwa kabla ya kuplekwa tena hospitalini hapo ambapo alirudishwa tena mwezi wa saba akiwa na matitizo ya kupata maumivu upande wa kushoto ndio akaanzishiwa tiba ambapo alipewa dawa zikiwemo Corvedolo, Lasix na Ascard pamoja na dawa nyingine.

Mbali na hayo alisema Manji pia alikua akisumbuliwa na matatizo ya kutokulala vizuri na maumivu ya mgongo

Daktari Mfawidhi wa Gereza la Keko, Inspekta Eliud Mwakawanga yeye katika ushahidi wake alisema, Manji alipokuwa gerezani, alikuwa akitumia vidonge kati ya 25 mpaka 30 kwa siku na alikuwa akipatiwa dawa hizo alipokuwa akisikia maumivu hasa ya mgongo kwani kuna kipindi alikuwa akiamka akiwa anatetemeka au kuchanganyikiwa.

Pia alidai kuna wakati alikuwa anaamka anashindwa hata kushindwa kutembea na wakati mwingine alikuwa akitumia mkanda wa kufunga mgongo na kuongeza pia mbali na dawa alizokuwa akipewa gerezani kulingana na hali yake kiafya siku hiyo, pia alikuwa na dawa zake za aina sita kutoka Muhimbili na kuongeza, wao hawakuwa wanatoa dawa za kulevya kwa mgonjwa ila wanatoa dawa. 


Naye, Daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili na dawa za kulevya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Francis Benedict aliiambia mahakama kuwa ili mtu aweze kupimwa kama anatumia dawa za kulevya lazima aache dawa anazotumia ndani ya wiki mbili alafu ndio apimwe la sivyo akipimwa lazima akutwe na Heron kutokana na dawa anazotumia.

Aidha Dk Francis aliiambia mahakama kuwa ripoti ya mkemia haikuonyesha ni kiasi gani cha heroin kwenye mkojo wa mshtakiwa bali ilikuwa imeonyesha heroin pekee. Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16, 2017 akidaiwa kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View wilayani Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroin. mwisho

No comments: