Jonas Kamaleki-MAELEZO
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa Kampuni ya Accaso International Limited, William Kafipa katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii.
Kafipa amesema mkaa wa mawe wa kupikia unatumika kwa kiasi kidogo na unawaka kwa muda wa saa nne mfululizo hivyo kuwezesha mtumiaji kupika vitu vingi kwa mkaa kidogo ukilinganisha na mkaa unaotokana na miti.
“Mkaa huu ni bora sana na watu wengi wakiutumia wataachana na kukata miti ovyo hivyo kutunza mazingira na kuepusha nchi kuwa jangwa,”alisema Kafipa.
Aliongeza kuwa badala ya kutumia gunia moja la mkaa wa kuni ambalo gharama yake ni kati ya shilingi 60,000/= na 85,000/=, unaweza kutumia boksi mbili hadi tatu za mkaa wa mawe kwa matumizi sawa na gunia hilo ambayo jumla yake ni shilingi 36,000/=. Kwa kufanya hivyo mtumiaji ataokoa fedha yake na pia atatunza mazingira kwani hatalazimika kukata miti ili kupata mkaa.
Kwa upande wake, Afisa Masoko na Mauzo wa Accaso, Monica Cornelius amesema mkaa wa mawe utampunguzia mwanamke adha ya kutembea mwendo mrefu kutafuta kuni endapo atatumia mkaa huo ambao bei yake ni nafuu hata kwa mtu wa kipato cha chini.
“Mkaa huu hautoi moshi jambo ambalo ni zuri kwa mazingira na kwa kwa afya ya mtumiaji, hii itaepusha pia mauaji ya vikongwe ambao walikuwa na macho mekundu kutokana na kupikia samadi au kuni mbichi,” alisema Monica.Monica ameongeza kuwa akina mama na watu wengine waipokee teknolojia hii mpya ya mkaa wa mawe wa kupikia ili iweze kubadilisha maisha yao.
Naye Afisa masoko na Mauzo wa kampuni hiyo, Abdullatif Ramadhani amesema mkaa huo wa mawe umeboreshwa na unafaa kwa matumizi ya nyumbani kwa kupikia hata kwenye taasisi kubwa kama shule, vyuo na magereza kwani upo kwa viwango tofauti.
“Kwa sasa soko letu lipo Dar es Salaam ambapo tumeanzia lakini tunalenga na mikoa ya jirani kama vile Pwani, Morogoro, Tanga na mikoa mingine hadi kuifikia mikoa yote ya Tanzania,”alisema Ramadhani.
Akizungumzia changamoto kampuni yake inazokumbana nazo, Ramadhani amasema ni watu kutobadilika na kupokea teknolojia mpya. Ameongeza kuwa baadhi wana dhana potofu kuwa mkaa wa mawe unaweza kutoboa sufuria zao, jambo ambalo si kweli kwani mkaa huo umetafitiwa kwa kina, na joto lake ni la wastani ambalo haliwezi kuharibu sufuria au chombo chochote cha kupikia.
Mkaa huu unaotokana na vumbi la makaa ya mawe unaweza kutumika kwenye majiko ya kawaida ya mkaa na unawaka kwa muda mrefu, pia ni rafiki wa mazingira na hauna madhara kwa binadamu.
Hivyo watanzania wengi wautumie ili kuepuka ukataji miti kwa wingi unaoharibu mazingira. Mazingira yakiharibika, ukame unatokea na kusababisha upungufu au ukosefu wa chakula.
3 comments:
Nawezaje kuupata aina hii ya mkaa wa mawe???
Nahitaji kuwa wakala. Vigezo ni nini?
Nahitaji kuwa wakala. Vigezo ni nini?
Post a Comment