Tuesday, October 17, 2017

MADIWANI NA WATENDAJI KATA HALMASHAURI YA HANDENI WASHUARIWA KUHAKIKISHA WANASIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO INAYOFADHILIWA NA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI (NGOS)

Madiwani na Watendaji wa kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga,wameshauriwa kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi ya maendeleo hususani inayofadhiliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kujengwa kwa kiwango kinachohitajika.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hamlamashuri ya wilaya ya Handeni William Makufwe kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Oktoba 16 na kueleza kuwa kuna umuhimu wa viongozi wa Kata kuwa karibu na wafadhili wanaojenga miradi kwenye maeneo yao kwani wao ndio wasimamizi.

Makufwe alisema ofisi ya Mkurugenzi inakuwa na imani kwamba Madiwani na Watendaji wa Kata ndio wasimamizi wakuu wa miradi iliyopo kwenye kata zao hivyo ikitokea miradi haina kiwango ina maana viongozi ngazi ya Kata hawakutimiza wajibu wao.

Aliongeza Kuwa ni kweli Serikali inahitaji kufadhiliwa lakini sio kwa kujengewa miradi ambayo ipo chini ya kiwango hali inayopelekea kuharibika Kwa muda mfupi na kutokufikia malengo yaliyokusudiwa.

" Waheshimiwa mnaopata miradi hii ya ufadhili hakikisheni inaleta tija kwa kusimamia hususani wanaopewa tenda ya kujenga kuepuka madhara yanayoweza kuepukika kwa kuisimamia tu" alisema Makufwe. 

Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni,Ramadhan Diliwa alisema kuwa kuna baadhi ya miradi ni kweli mapungufu yapo na yamesababishwa na kutokuwepo uangalizi wa karibu na kusisitiza Madiwani kusimamia vyema miradi kwa manufaa ya wananchi wao. 

Alitolea mfano eneo la Kata ya Kabuku mjini kuwa kuna madarasa yaliojengwa na wafadhili miaka iliyopita lakini ipo chini ya kiwango hali iliyopelekea wanafunzi kutolewa ndani ya madarasa hayo na kutafutiwa mengine kutokana na kuwa hatarishi kwao.

Aidha Sharifa Abebe diwani kata ya Kwamgwe alisema ni kweli awali hali kama hiyo ilikuwa ikitokea ila kwasasa wanasimamia vizuri miradi iliyopo kwenye maeneo yao ambapo kwake ipo miradi inayofadhiliwa na inajegwa katika ubora unaohitajika kutokana na usimamizi uliopo Kwa kushirikiana na watendaji ngazi ya Kata.

Imetolewa na 

Kitengo cha Habari
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni akizungumza kwenye kikao cha baraza na kutoa ushauri kwa viongozi.
Diwani Kata ya Kwamgwe Mh Sharifa abebe akizungumza kwenye kikao hicho cha baraza
Wataalamu wa Halmashauri na Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza
Mwenyekiti wa Halmashauri MH Ramadhani Diliwa katikati akizungumza na wataalamu na Madiwani, kulia ni kaimu Mkurugenzi kwa Muda Fatuma Kalovya , kushoto ni Makamu mwenyekiti Mh. Abdalla Pendeza.

No comments: