Friday, October 6, 2017

KATIBU MKUU SIHABA NKINGA AHIMIZA WANAWAKE KUJIUNGA NA VIKUNDI VYA KIUCHUMI WILAYANI MVOMERO


Na Kitengo cha Mawasiliano serikalini WAMJW

Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga amewahimiza wanawake nchini kujiunga na vikundi vya kiuchumi katika kujiletea maendeleo.Ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya majaribio ya kuhamisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi yaliyofanyika katika wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.

Bibi Sihaba amesema kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi ni moja ya jitihada za utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000; Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/2022); Mpango wa Taifa wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/2021); na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.

Ameongeza kuwa mwongozo wa uanzishaji wa vikoba utasaidia pia kuwa na takwimu za taarifa sahihi za vikundi kwa ajili ya uchambuzi na kujenga hoja kuhusu maamuzi ya ushiriki na uzingatiaji wa nafasi ya wanawake katika fursa mbalimbali.

“Nijukumu la kila Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha mwongozo huu unatekelezwa ipasavyo na kuleta matokeo yaliyotarajiwa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi ikiwemo kuboresha hali ya maisha yao” alisema Bibi Sihaba. Akiongea katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Bw. Julius Mbilinyi amefafanua kuwa vikundi vingi vimekuwa vikiendeshwa bila kuwa na mwongozo na pia ukosefu wa elimu ya uendeshaji.

Ameongeza kuwa hatua ya kuwepo mwongozo na elimu inayotolewa imetoa mbinu na kujenga uelewa ambao utatumika kuhamasisha wanawake kuunda vikundi na kuboresha vikundi mbalimbali vya kiuchumi kutegemea mazingira ya wanachama.Naye Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mvomero Bi. Sia Ngao amesema kuwa mafunzo ya mwongozo wa uundaji na uimarishaji wa vikundi vya kiuchumi ambayo yametolewa na Wizara mama yataimarisha usimamizi na uratibu wa vikundi kwa kuvifanya kuwa endelevu na kuwanufaisha wanawake wengi kutokana na waratibu kujengewa uwezo na upatikanaji wa elimu stahiki kwa walengwa mahususi.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Mvomero Janeth Shishila amebainisha kuwa awali walikuwa wakiunda vikundi kiholela bila kuwa na mwongozo wa Kitaifa ila baada ya mafunzo haya yatawawezesha Idara kufanya kazi zake kwa umahiri zaidi katika kujenga ubia wa wanawake wajasiriamali ili kukuza faida ya kiuchumi, kijamii na kielimu kwa manufaa ya wanawake, familia na Taifa.

Mwezeshaji kutoka Shirika la CARE Tanzania Bi Zenais Matemu ameeleza kuridhishwa na ushirikiano wanaopata kutoa Serikalini katika kuboresha hali za makundi yenye mahitaji maalum hapa nchini wakiwemo wanawake masikini. Dhumuni la mafunzo haya ya siku tatu yalikuwa yakifanyika kwa majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi, uzalishaji mali, viwanda vidogo vidogo, ili kukuza kipato na kutokomeza ukatili wa kijinsia unaotokana na umasiki wa kipato katika kaya.

Mbali na Halmashauri ya Mvomero, majaribio ya Mwongozo huu yatafanyika pia katika Halmashauri ya Rombo mkoani Kilimanjaro na kuzingatia uzoefu na maoni yatakayopatika kutoka kwa wadau kabla ya kuanza kutumika rasimi katika mikoa yote nchini.
Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga(katikati) akizungumza na washiriki wa mafunzo ya majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi yaliyofanyika wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi wakimsikiliza Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga( hayupo pichani) wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo yaliyofanyika wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Bw. Julius Mbilinyi akifafanua jambo katika mafunzo ya majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi yaliyofanyika wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Mwezeshaji kutoka Shirika la Care Tanzania Bi Zenais Matemu akitoa mada katika Mafunzo ya majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi yaliyofanyika wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Baadhi ya washirki wa mafunzo ya majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa katika mafunzo hayo yaliyofanyika wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Bw. Julius Mbilinyi(kulia) akijadiliana jambo na Mwezeshaji kutoka Shirika la Care Tanzania Bi Zenais Matemu mara baada ya kukamilika kwa mafunzo ya majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi yaliyofanyika wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya majaribio ya mwongozo wa kuhamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi yaliyofanyika Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

No comments: