Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akitafakari jambo mara baada ya kuzungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Lenny Mjini Geita
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba (katikati) akisisitiza jambo Wakati wa Mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Lenny Mjini Geita, Mwingine ni Naibu Waziri wa wizara ya kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa (Kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe.
Waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo Wakati wa Mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Lenny Mjini Geita
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba (katikati) akisisitiza jambo Wakati wa Mkutano na
waandishi wa habari katika Ukumbi wa Lenny Mjini Geita, Mwingine ni Naibu Waziri wa wizara ya kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa (Kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe.
…………………………………………………………………………………
Na Mathias Canal, Geita
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe kuwafukuza kazi maafisa watatu wa idara ya Maendeleo ya Mazao katika sehemu ya pembejeo ambao wamebainika kuhusika moja kwa moja na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa.
Akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Lenny Mjini Geita Mhe Tizeba alisema kuwa kufukuzwa kazi kunajili kutokana na ukosefu wa umakini na usimamizi mzuri wa sheria ya ununuzi wa Umma ikiwemo kusababisha kuchapishwa kwa vocha za pembejeo zenye thamani ya Tshs 78,054,970,000 ambazo ni zaidi ya bajeti halisi iliyotengwa kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo kwa kiasi cha Tshs 42,587,419,200
Watumishi waliofukuzwa kazi ni Bw Shenal S. Nyoni aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kitengo cha pembejeo, Aliyekuwa Afisa kilimo Daraja la I Bw Michael G. Mayabu na Bw Franks F. Kamhabwa.
Waziri Tizeba ametumia mamlaka hayo mara baada ya kupitia taarifa ya waraka wa mkakati wa utekelezaji na Usimamizi wa utoaji wa Ruzuku za pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa kutumia vocha wa mwaka 2015/2016 ambapo pamoja na mambo mengine uliainisha utaratibu wa usimamizi wa zoezi la utopaji wa ruzuku ambao ulilenga kuleta ufanisi katika utekelezaji wake.
Wakati wa utekelezaji wa zoezi la usimamizi wa mpango wa Ruzuku za Pembejeo katika Msimu wa mwaka 2014/2015-2015/2016 kulijitokeza tuhuma mbalimbali zilizohusu ukiukwaji wa taratibu uliofanywa na watumishi wa serikali Za Mitaa zilizohusika kwenye Mpango wa Ruzuku, watumishi hao walituhumiwa kushirikiana na Mawakala waliokuwa wamepewa dhamana ya kusambaza pembejeo katika kuhujumu mpango huo serikalini.
Ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo pamoja na uhakiki uliofanywa na wizara ya fedha na Mipango kuthibitisha uhalali wa madeni ya mawakala, Mwezi Aprili, 2017 Wizara ya Kilimo ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwasimamisha kazi watumishi watano wa idara ya maendeleo ya mazao, Sehemu ya pembejeo waliohusika kusimamia mpango wa Ruzuku za pembejeo za kilimo.
Aidha, Mwezi Mei, 2017 wizara ya kilimo iliunda kamati ya uchunguzi ili kuchunguza tuhuma zilizowahusu watumishi hao waliosimamishwa kazi.Katika hatua nyingine Mhe Dkt Tizeba amemuagiza katibu mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe kuwasimamisha kazi watumishi wengine watatu ambao ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya mazao Bw Twahir S. Nzallawahe, Mkurugenzi wa Kitengo cha ununuzi na Ugavi Bw Burhan A. Shaban, na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa kitengo cha pembejeo Bw Canuth Komba.
Zaidi ya shilingi 29,977,114,700 zingepotea kama umakini usingekuwa mkubwa katika uhakiki kwani katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 serikali ilitenga kiasi cha shilingi 35,467,550,800 kwa ajili ya pembejeo za kilimo na mara baada ya zoezi la utoaji ruzuku ilibainika kuwa deni lililowasilishwa serikalini na mawakala ilikuwa ni kiasi cha shilingi 65,444,665,500.
Sambamba na hayo Mhe Waziri Tizeba aliviomba vyombo vya dola kuchunguza zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya watumishi na watu wote waliohusika katika ngazi za halmashauri na mawakala wote waliofanya udanganyifu kwa lengo la kuisababishia serikali hasara.
No comments:
Post a Comment