Sunday, October 15, 2017

BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA YAIPONGEZA TANZANIA KUHUSU USIMAMIZI WA RASILIMALI ZAKE

Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (wa tatu kushoto) wakiwa katika mkutano na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Benki hiyo Bw. Amadou Hott, (wa tatu kulia), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.


Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati, Bw. Amadou Hott (kushoto) akisikiliza kwa makini wakati wa mkutano na Waziri wa fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) mkoani Dodoma, kulia ni Mkurugenzi wa benki hiyo anayeshughulika masuala ya maendeleo ya mifumo ya umeme, Bw. Henry Baldeh.
Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wakiwa katika mkutano na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) mjini Dodoma.


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kushoto) akichukua kumbukumbu wakati wa mkutano na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) (hawapo pichani) kulia ni Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara hiyo Bw. John Rubuga, mjini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dorothy Mwanyika (kulia), akichukua kumbukumbu wakati wa mkutano na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) (hawapo pichani) kushoto ni Kamishna wa Bajeti wa Wizara hiyo Bi. Marry Maganga akisikiliza kwa makini wakati mkutano ukiendelea katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.


Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati, Bw. Amadou Hott (kushoto), akifurahia jambo wakati wa mkutano uliowahusisha viongozi mbalimbali wa Wizara ya Fedha na Mipango (hawapo pichani) wenginie ni sehemu ya ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) walioshiriki mkutano huo ulifanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (kulia), akiagana na mgeni wake Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati Bw. Amadou Hott baada ya kumaliza mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa nne kulia) na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati Bw. Amadou Hott (wa tano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara hiyo na ujumbe wa benki hiyo baada ya kumalizika kwa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kulia), akifurahia jambo na mmoja wa wajumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika baada ya kumalizika kwa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kushoto) na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati, Bw. Amadou Hott wakifurahia jambo baada ya kumalizika kwa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango


…………….

Benny Mwaipaja, Dodoma

MAKAMU wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, anayeshughulikia masuala ya nishati Bw. Amadou Hott amesema kuwa Tanzania iko katika njia sahihi kutaka iwe na asilimia 16 ya hisa kwenye miradi inayowekezwa katika sekta ya madini na mafuta ili rasilimali hizo ziweze kuwanufaisha wananchi na wawekezaji.

Makamu huyo wa Rais ametoa kauli hiyo mjini Dodoma alipofanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango kuhusu namna benki hiyo inavyoweza kusaidia kulikwamua Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) kutoka katika mzigo wa madeni unaolikabili ili liweze kujiendesha kibiashara bila kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.

Alisema kuwa nchi kadhaa duniani, zenyewe ama kwa kutumia kampuni ilizoziteua zina hisa ya kati ya asilimia 14 hadi 16 za hisa za bure katika miradi ya rasilimali za madini ili pande zote zinazohusika katika mikataba hiyo ziweze kunufaika na rasilimali za nchi.



Alitolea mfano wa baadhi ya nchi ikiwemo Senegal ambazo zinatekeleza sera kama hizo na hakuna matatizo yoyote kati ya nchi hizo na wawekezaji na kwamba anaona nia njema ya Tanzania katika kulinda rasilimali zake.

“Jambo la msingi linalotakiwa ni kuhakikisha kuwa makubaliano ya suala hili kati ya Serikali na Sekta binafsi yawe ya wazi, usawa na haki na ni muhimu wawekezaji wakakubaliana na utaratibu huo” aliongeza Bw. Hott.

Hivi karibuni kumekuwa na mjadala baada ya mwekezaji mkubwa, Bilionea Aliko Dangote kunukuliwa na vyombo vya habari nchini uingereza akiitahadharisha Serikali kuhusu uamuzi wake wa kuchukua hisa 16 za bure katika sekta ya madini na mafuta kwamba utawatisha wawekezaji.

Akizungumzia deni la TANESCO, Hott alisema kuwa Benki yake inakusudia kuipatia Tanzania kiasi cha dola milioni 200 za Marekani ili iweze kupunguza deni la dola zaidi ya milioni 370 ambazo Shirika hilo linadaiwa na taasisi mbalimbali ili liweze kujiendesha kibiashara.

Akizungumza yaliyojiri kwenye kikao na mgeni wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango ameishukuru Benki hiyo kwa misaada mbalimbali na mikopo yenye mashari nafuu inayoipatia Serikali, ambapo katika sekta ya nishati peke yake, kufikia mwaka 2019, itakuwa imetoa zaidi ya Dola bilioni 1.1.

“Tunaendelea kujadiliana namna bora zaidi ya kutekeleza masharti yaliyomo kwenye fedha hizo dola milioni 200 ambazo benki hiyo imeonesha nia ya kuipatia Serikali ili iweze kupunguza madeni ya TANESCO yanayofikia Dola milioni 370” alisema Dkt. Mpango

Dkt. Mpango alisema kuwa Benki hiyo pia imeionesha nia ya kusaidia utekelezi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Stieglers Gorge utakaozalisha megawati 2,100 ambao utakuwa mkombozi mkubwa wa mapinduzi ya viwanda.

“Lakini pia AfDB wamekubali kutupatia fedha za kujenga awamu ya kwanza ya miundombinu ya kusafirisha umeme wa ukanda wa Kaskazini Magharibi, unaoanzia Mbeya, Sumbawanga hadi Nyakanazi, kiasi cha Dola za Marekani milioni 123 na benki hiyo inajadiliana na Shirika la Maendeleo la Korea ili itupatie kiasi kingine cha Dola milioni 60 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo” Alisema Dkt. Mpango

Aidha, Benki hiyo itafadhili mradi wa umeme unaotumia joto ardhi (geothemo) kwenye ukanda wa Bonde la Ufa wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 91 lakini wao watatoa Dola milioni 65.

“Miradi mingine ya nishati itakayofadhiliwa na Benki hiyo ni ule ulioko Kakono, Mto Maragarasi wenye uwezo wa kuzalisha megawati 44.5, mkopo ambao unatarajiwa kupatikana ifikapo Novemba, 2018 na tumekubaliana mradi huu uweze kutekelezwa haraka iwezekanavyo” Alifafanua zaidi Dkt. Mpango

Alisema kuwa mradi mwingine utaotekelezwa na Benki hiyo ni mradi mkubwa wa kupeleka na kusambaza umeme kwenye miji mikuu yote hapa nchini unaogharimu Dola milioni 274, unaotarajiwa kukamilika ifikapo Julai, 2019 ili miji hiyo iweze kuchochea uwekezaji wa viwanda kwakuwa na nishati imara na ya bei nafuu.

Dkt. Mpango aliisifu Benki hiyo kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania na kwamba uhusiano huo utaendelea kuimarishwa kwa faida ya pande hizo mbili.

No comments: