Greyson Mwase na Asteria Muhozya.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ameeleza vipaumbele vyake katika Wizara kuwa ni pamoja na udhibiti wa utoroshaji wa madini nchini, maslahi kwa wafanyakazi huku akiwataka watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.
Kairuki ameyasema hayo mapema leo tarehe 10 Oktoba, 2017 jijini Dar es Salaam alipozungumza na watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake, waliopo Dar es Salaam na Makao Makuu ya Wizara Dodoma. Lengo La kikao hicho lilikuwa ni kufahamiana na kupanga mikakati ya kushirikiana ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi wa nchi.
Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI) pamoja na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini na Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (TEITI).
Amesema kuwa Sekta ya Madini inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwataka wataalam wa madini kubuni mbinu za ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye uchimbaji madini.
Katika hatua nyingine aliwataka wataalam hao kubuni mikakati ya kuzuia utoroshaji wa madini nchini ili nchi ipate mapato stahiki.Amewataka watumishi kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na kuwa wabunifu ili sekta hiyo iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewakumbusha watumishi kuzingatia Dira na Dhima ya Wizara ikiwemo kufanya kazi kwa tija ili hatimaye sekta ya madini iweze kuchangia katika uchumi wa nchi kwa kuwa mchango wa sekta husika bado ni kidogo.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) akitoa maelekezo kwa watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake (hawapo pichani) Kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Kaimu Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (kushoto mbele) pamoja na watendaji wengine wa Wizara wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki. (hayupo pichani).
Sehemu ya watendaji wa Wizara ya Madini wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akifafanua jambo katika kikao hicho. Kushoto ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kulia mbele) akieleza majukumu ya Wizara ya Madini kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hawapo pichani)
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Madini, Makao Makuu Dodoma wakifuatilia maelekezo kutoka kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) kwa njia ya video conference.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo(kulia) wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (hayupo pichani)
No comments:
Post a Comment