Monday, September 25, 2017

TPSC YAASWA KUFANYA TAFITI ZA KUSAIDIA JAMII

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza katika mahafali ya 27 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika mkoani Singida mwishoni mwa wiki
Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wakiwa katika mahafali ya 27 ya Chuo hicho hivi karibuni mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema( wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wa pili kushoto ni Mkuu wa chuo hicho na Mtendaji Mkuu Dkt. Henry Mambo. 
Na  mwandishi Wetu, Singida
Serikali imekitaka Chuo Cha Utumishi wa Umma Tanzani (TPSC) kufanya tafiti, kutoa mafunzo na kutoa ushauri unaolenga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kwa sasa ikiwamo umasikini.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mahafali ya 27 ya TPSC kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) Angellah Kairuki, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi alisema kuwa  mafunzo yanayotolewa na chuo hicho pia yalenge katika kukabiliana na Rushwa, mmomonyoko wa maadili na kufanya kazi kwa mazoea katika sekta ya umma.

“Ni matumaini yangu kuwa aina ya mafunzo na shauri za kitaalam zinazotolewa na zinazoendelea kutolewa na chuo hiki zitakwenda sambamba na maboresho katika sekta ya umma na pia kuwawezesha watumishi wa serikali na na wale watakaoingia serikalini siku za usoni kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea hapa nchini na Duniani kote,” alisema.

Alisema kuwa katika kuelekea Tanzania ya Viwanda serikali inasisitiza mafunzo na tafiti zinazofanywa na chuo hicho kujikita katika kuandaa watu mahiri , wenye weledi na ujuzi utakaotumika kuisaidia kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda na hivyo kutimiza ndoto za Rais Dkt.John Pombe Magufuli za kujenga Tanzania ya Viwanda.

Alisema kuwa   serikali inaunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na taaisi hiyo zenye lengo la kuboresha huduma mbalimbali zitolewazo na chuo baadhi ya maboresho hayo yakiwa ni kuanzishwa ka kozi za shahada katika fani za Uhazili na Menejimenti ya Kumbukumbu,Ukamilishaji wa mchakato wa ujenzi wa jengo la Maktaba katika Tawi la Tabora sanjari uandaaji wa mpango wa ujenzi (Master Plan) Tawi la Singida.

Awali katika Mahafali hayo Mtendaji Mkuu wa TPSC Dkt.Henry Mambo alisema kuwa  wahitimu 6332 walihitimu mkatika mahafali hayo wakitoka katika matawi sita ya chuo hicho yaliyoko katika mikoa ya Singida, Dar es Salaam, Mtwara, Tanga,Mbeya na Tabora.

Dkt. Mambo alizitaja aina za vyeti na idadi ya wahitimu kwenye mabano kuwa ni Astashahada ya Awali (2,368),Astashahada (1,781) na Stashahada (2183).
Alisema katika kuelekea Uchumi wa kati, ifikapo mwaka 2025 chuo kimeendela kuboresha huduma zake mbalimbali ikiwamo usimikazi wa utoaji elimu bora yenye viwango  vya kukidhi hali ya soko la ajira na kiushindani.
“Pia tunaendeleza watumishi wetu ili wafikie viwango vinavyohitajika,” alisema.
Mkuu huyo wa Chuo alisema kuwa TPSC imeendelea kufanya vizuri katika eneo la tafiti na machapisho na shauri za kitaalam ili kubaini changamoto zilizopo katika utumishi wa umma na kutoa majawabu ya changamoto hizo kupitia tafiti.

No comments: