Thursday, September 21, 2017

TBS yawataka wadau wa Umeme kutumia vifaa vyenye viwango stahili

WADAU katika sekta ujenzi nchini wametakiwa kutumia bidhaa zenye viwango na ubora unaostahili ili kulinda ukuaji wa sekta hiyo na kuleta matokea chanya kwa ustawi na maendelea ya taifa na watu wake.

Akizungumza kwenye semina iliyowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wahandisi, makandarasi, wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa nyaya za umeme jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bi. Edna Ndumbaro alisema bidhaa zinazotumika kwenye masuala ya umeme zinahitaji kuwa na viwango na ubora unaostahili.

“Badiliko la rangi mpya za nyaya za umeme (New Colour Codes) limewaleta wadau hawa muhimu kujadiliana kwa pamoja na kuazimia kwa pamoja namna bora ya utekelezaji wake,” Bi. Ndumbaro alisema. Alisema rangi mpya ya nyaya ya umeme ilishaazimiwa kama kiwango cha lazima kufuatwa tangu mwaka 2016 na hivyo ni vyema kwa wadau na wataalamu wakazingatia kuwa viwango ni jambo muhimu sana likapewa kipaumbele zaidi.

“Sisi kama TBS tutaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa viwango na ubora kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ikiwemo tovuti ya shirika,” Bi. Ndumbaro alisema na kuongeza kuwa washiriki wa semina hiyo watakuwa walimu wazuri.

Awali, Afisa Viwango wa TBS, Bw. Henry Massawe katika Mada yake aliyoiwasilisha katika semina hiyo, alisema rangi mpya za nyaya za umeme zitasaidia kuzuia uwezekano wa kuyumbisha bei za nyaya ya umeme. Bw. Massawe ambaye aliwasilisha mada kuhusu mahitaji ya utambuzi wa viwango na rangi za nyaya za Umeme alisema ni vizuri wadau wakatambua kuwa Viwango vifuatwe kabla ya matumizi.

“Viwango vikifuatwa na kuzingatiwa katika matumizi ya vifaa ya nyaya za umeme vitapunguza kama siyo kuondoa kabisa madhara ya vifaa umeme vinavyoingizwa kutoka nje,” Bw. Massawe alisisitiza.

Kwa upande wake, Mshiriki kutoka Kampuni ya NAMIS Corporate Limited, Bwana Bright Naimani alisema badiliko la Rangi mpya za nyaya za umeme ni muhimu katika kulinda ubora na kiwango kwani wadau walipata fursa ya kujifunza na kujadiliana masuala mbalimbali ya viwango.

Semina hiyo ambayo iliandaliwa na TBS kwa lengo la kuhamasisha na kuwajengea uwezo wadau mbalimbali umuhimu wa matumizi ya rangi mpya za nyaya za umeme.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bi. Edna Ndumbaro akisisitiza jambo kwenye Semina ya wadau kwenye semina iliyowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wahandisi, makandarasi, wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa nyaya za umeme jijini Dar es Salaam jana kuhusu matumizi ya Rangi mpya za nyaya za umeme.
Afisa Viwango wa Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw. Henry Massawe akiwasilisha mad kwenye Semina ya wadau kwenye semina iliyowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wahandisi, makandarasi, wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa nyaya za umeme jijini Dar es Salaam jana kuhusu matumizi ya Rangi mpya za nyaya za umeme.

Baadhi ya washiriki wa semina ya wadau kwenye semina iliyowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wahandisi, makandarasi, wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa nyaya za umeme jijini Dar es Salaam jana kuhusu matumizi ya Rangi mpya za nyaya za umeme semina hiyo imeandaliwa na Shirika Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

No comments: