Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
inaungana na wadau wote duniani katika kuadhimisha siku ya wazee duniani. Wakati
dunia inaadhimisha siku hii, Tume inatoa wito kwa jamii ya Watanzania kuondoa
vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi ya wazee ili kuhakikisha kuwa wanaishi
katika kutekeleza kauli mbiu ya taifa inayosema “Kuelekea uchumi wa viwanda:
Tuthamini mchango, uzoefu na ushiriki wa wazee kwa maendeleo ya taifa.”
Uzee na kuzeeka havikwepeki; hivyo ustaarabu wa jamii au
nchi yoyote duniani si wingi wa raslimali na mazingira mazuri bali katika
uwekaji wa mifumo madhubuti ya kulinda na kutetea haki za makundi maalum
yanayohitaji ulinzi wa jamii husika. Kwa kulitambua hilo Desemba 14, 1990,
Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Azimio lake Na. 45/106 ulipitisha
tarehe 01 Oktoba, ya kila mwaka kuwa siku ya wazee Duniani. Vipaumbele katika Azimio
hilo ni pamoja na suala la uhuru wa wazee, wazee kushiriki na kushirikishwa
katika shughuli za maendeleo, kutunzwa na kuheshimiwa.
Hivyo siku hii ya tarehe 01 Oktoba, dunia inawapa nafasi
wazee kukutana pamoja na kubadilishana mawazo juu ya nini cha kufanya kuhusiana
na mustakabali wa haki zao kwa ujumla, katika kuleta maendeleo ya Taifa
tunapoelekea Tanzania ya viwanda.
Katika kutambua, kulinda kukuza na kutetea haki za wazee
serikali imeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, yaani “The African Charter on Human and People’
Rights (ACHPR)” pamoja na Itifaki ya kusimamia haki za wazee ’’Protocol to the African Charter on Human
and People’ Rights on the Rights of elder persons in Africa”. Kadhalika kuna Mkataba wa Kimataifa wa Haki
za Kiraia na Kisiasa, yaani The International Convenant on Civil and
Political Rights (ICCPR), na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi,
Kijamii na Kiutamaduni, yaani The International
Convenant on Economic, Social and Cultural Rights (ICESCR).
Kitaifa, kuna Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake ibara ya 12 (2) na ibara ya 14 ambazo zimeeleza
juu ya wazee kupewa heshima na kupata hifadhi kutoka kwa jamii wanamoishi.
Aidha, kuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
ambayo ni Idara huru ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 129 (1)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na Sheria Na. 7 ya Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya mwaka 2001 ambayo ni kitovu cha kulinda,
kutetea na kukuza haki za binadamu nchini.
Takwimu za wazee kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002,
Tanzania ilikuwa na wazee 1,952,041 (sawa na wanaume 940,229 na wanawake
1,011,812) na katika sensa ya mwaka 2012 idadi ya wazee iliongezeka hadi
kufikia 2,507,568 (wanaume 1,200,210 na wanawake 1,307,358) sawa na 5.6% ya
wananchi wote. Hivyo, kwa kadiri idadi ya wazee inavyoongezeka ndivyo
changamoto zinazowakabili zinavyoongezeka. Hivyo jitihada mahsusi lazima
zifanyike kukabiliana nazo.
Tume kama taasisi ya kitaifa yenye
jukumu la kulinda, kukuza na kutetea haki za binadamu imefanya jitihada
mbalimbali kuhakikisha kuwa wazee wanapata haki zao. Jitihada hizo ni pamoja
na:
i)
Kushughulikia malalamiko yanayohusu uvunjifu
wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa wastaafu hasa
katika suala linalohusu mapunjo na wastaafu kutolipwa stahiki zao kwa wakati.
ii)
Tume imekuwa ikitoa elimu ya haki za binadamu
ikiwemo haki za wazee kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwemo taasisi za
serikali, asasi za kiraia na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na umma kwa
ujumla.
iii)
Tume imeshiriki kikamilifu katika mchakato wa
kutunga sheria ya wazee kwa kutoa maoni yanayohakikisha kuwa haki za wazee
zinalindwa na kuhifadhiwa. Pia inashiriki katika mchakato wa mpango wa pensheni
jamii.
iv)
Tume imetoa matamko mbalimbali kulaani mauaji
ya wananchi wakiwemo wazee yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Tume inapongeza sana jitihada zinazochukuliwa na Serikali
ya awamu ya tano katika kushughulikia masuala ya wazee. Jitihada hizo ni pamoja
na:
i)
Kuimarisha Wizara inayoshughulikia masuala ya
wazee kwa kutaja neno “wazee” katika jina la Wizara.
ii)
Kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza bajeti
ya Afya inayoiwezesha Serikali kununua dawa na vifaa tiba kwa wakati.
iii)
Kuweka madirisha ya wazee katika hospitali na
vituo vya afya.
iv)
Kuanzisha mchakato wa mfuko wa Afya ya jamii.
v)
Kuanzisha mchakato wa malipo ya pensheni kwa
wazee wote.
vi)
Kuanzisha mchakato wa kupambana na mauaji ya
wazee.
vii)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
imeanzisha mpango wa malipo ya pensheni jamii kwa wazee wenye umri wa miaka 70+.
viii)
SMZ pia imo katika mchakato wa kutoa
vitambulisho maalum kwa wazee vitakavyowawezesha kupata huduma mbalimbali.
ix)
SMZ imeimarisha huduma za wazee kwa kuanzisha
idara ya wazee.
Pamoja na jitihada ambazo zimefanywa na Serikali, Tume,
Asasi za Kiraia, Mikataba, Maazimio na Itifaki za kikanda na kimataifa, bado
wazee wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kimsingi huvunja haki.
Changamoto hizo ni pamoja na:
i)
Ukosefu wa Sheria maalum inayoweka ulinzi na
kuzitambua haki za wazee.
ii)
Wazee walio wengi kutofaidika na mafao
mbalimbali ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (Pensheni jamii) licha ya kwamba
maendeleo yaliyofikiwa na nchi hii ni matokeo ya mchango wa wazee kwa kazi zao
walizofanya.
iii)
Umaskini wa kipato miongoni mwa wazee.
iv)
Usalama mdogo kwa wazee kutokana na ukatili
na manyanyaso wanayofanyiwa, hususani vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake,
walemavu na mauaji ya wazee kutokana na imani potofu. Kwa mfano, takwimu za
Wizara ya Mambo ya Ndani (2016) zinaonyesha kuwa wazee wameendelea kuuawa
katika sehemu mbalimbali nchini. Kwa mfano, mwaka 2014 waliuawa wazee 557, mwaka 2015 wazee 190 na katika kipindi cha
mwezi Januari hadi Oktoba 2016 wazee 119
waliuawa. Mikoa inayoongoza kwa mauaji ya wazee kwa kipindi cha Julai 2015 hadi
Machi 2016 ni: Tabora (49), Shinyanga (17), Mbeya (15), Geita (11), Rukwa (9),
Njombe (9) na Simiyu (7).
Kutokana na changamoto hizo, na ili kuhakikisha kuwa haki
za wazee zinalindwa, zinadumishwa, zinakuzwa na kuendelezwa, Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora inatoa mapendekezo yafuatayo kwa Serikali, wadau na
jamii kwa ujumla:
i)
Elimu ya haki za binadamu na misingi ya
utawala bora itolewe kwa wananchi wote. Hii itasaidia katika kujenga jamii
inayoheshimu haki za binadamu nchini.
ii)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikamilishe kutunga Sheria ya Wazee ili kurahisisha utekelezaji wa Sera ya Wazee
ya mwaka 2003.
iii)
Serikali iendelee kuboresha huduma za afya na
zitolewe bure kwa wazee wote, ikiwa ni pamoja na kukamilisha mpango wa afya ya
jamii.
iv)
Serikali ikamilishe mpango wa malipo ya
pensheni jamii (Social Pension) kwa wazee wote.
v)
Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama
ihakikishe panakuwepo ulinzi madhubuti kwa wazee ikiwa ni pamoja na kuwakamata
wahusika wa mauaji ya wazee na kuwafikisha katika vyombo vya dola kwa wakati na
jamii ijitokeze kutoa ushahidi.
vi)
Kamati za ulinzi za Kata na Vijiji ziimarishwe
ili kulinda maisha ya wazee.
vii)
Kupitia mkakati wa kunusuru kaya maskini
unaosimamiwa na TASAF, kipaumbele kitolewe kwa wazee kote nchini.
viii)
Mabaraza ya wazee yaanzishwe na kuimarishwa
ili kutoa nafasi ya ushirikishwaji wa wazee katika maendeleo ya nchi.
Mwisho, Tume inatoa rai kwa Serikali na wananchi wote kwa
ujumla kulinda na kutetea haki za wazee. Aidha, tuthamini mchango, uzoefu na
ushiriki wa wazee kwa maendeleo ya taifa.
“Uzee
na kuzeeka havikwepeki”
Imetolewa
na:
Iddi Ramadhani Mapuri
Makamu Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Oktoba 1, 2017
No comments:
Post a Comment