Friday, September 22, 2017

Tamasha la Utamaduni Tukuyu Ni Chachu ya Kukuza Na Kuendeleza Utamaduni Nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa mashuka ya Kimasai) akiongea na washiriki wa tamasha la Ngoma za jadi linaloratibiwa na Taasisi ya Tulia Trust leo wilayani Tukuyu mkoani Mbeya. Wa kwanza kushoto ni Mwasisi wa taasisi hiyo ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makala akifungua tamasha la ngoma za jadi leo wilayani Tukuyu mkoani humo ambapo amesisitiza Watanzania kukuza na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania hatua inayoongeza fursa ya ajira kwa vijana mkoani humo.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akipokea zawadi ya CD kutoka kwa Mchungaji Damian Matipa wa Kanisa la Uponyaji Mbeya Mjini yenye nyimbo za kumpongeza Naibu Spika kwa kazi anazofanya.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel mara baada ya kuwasili Tukuyu mkoani Mbeya.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akiteta jambo na Mkuu wa Majeshi Mtaafu Jenerali Davis Mwamunyange wakati wa tamasha la Ngoma za jadi linaloratibiwa na Taasisi ya Tulia Trust leo wilayani Tukuyu mkoani Mbeya.
Ngoma ya Bugobo gobo kutoka Bujara mkoani Mwanza
Baadhi ya viongozi wakiwa wamebeba moja ya vifaa Bugoyangi (nyoka) vinavyotumiwa na kikundi cha kucheza ngoma cha Bujora mkoani Mwanza.
Picha na Eleuteri Mangi, WHUSM, Tukuyu, Mbeya


Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Tukuyu Mbeya


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Watanzania kuenzi na kuimarisha utamaduni wao ili kuepukana na chamgamoto ya utamaduni kutoka nchi za magharibi unaoletwa ukuaji wa sayansi na teknolojia.


Prof. Elisante ametoa kauli hiyo leo Tukuyu wakati wa ufunguzi wa tamasha la Ngoma za jadi linaloratibiwa na Taasisi ya Tulia Trust inayoongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson inayojishughulisha na masuala ya kukuza na kuendeleza utamaduni nchini.


Prof. Elisante amewahakikishia vijana kuwa kuwekeza mahali salama, hivyo waendelee kukuza sanaa yao iweze kujijengea jina na kutambulika ndani na nje ya nchi.


“Vijana muendelee kuthamini utamaduni wetu, tusiposimamia, kuwekeza na kuthamini utamaduni wetu, utamaduni wan chi za magharibi utawachukua vijana wetu na kuacha tunu yetu ya asili tangu enzi za babu zetu” alisema Prof. Elisante


Prof. Elisante amewahakikishia waandaaji wa tamasha hilo kuwa Serikali ipo sambamba nao na kuwataka wapanue wigo wa tamasha hilo ili liweze kuwa na matawi na kuwafikia watu wengi zaidi nchi nzima.


Akifungua tamasha hilo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makala amesema limekuwa kichocheo cha kukuza na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania hatua inayoongeza fursa ya ajira kwa vijana mkoani Mbeya. 


“Utamaduni ukitumika vizuri una fursa nyingi kwa vijana katika maeneo mbalimbali ikiwemo tasnia ya sanaa ambayo itawasaidi kujipatia ajira hatua inayowasaidia kuinua kipato chao na uchumi wa taifa” alisema Mkuu huyo wa mkoa.


Kwa upande wake Mwasisi wa Taasisi ya Tulia Trust ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa tamasha hilo linafanyika kwa mara ya pili ambapo mwaka huu limakuwa na wigo mpana kwa kushirikisha vikundi vya ngoma kutoka maeneo mbalimbali nchini.


Kuhusu manufaa ya tamasha hilo, Dkt. Tulia amesema kuwa mwaka jana taasisi hiyo ilipeleka vijana 20 kupata mafunzo ya kitaalamu kwenye fani ya sanaa na utamaduni katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) na mwaka huu wanatarajia kupeleka vijana 27 ili waweze kupata ujuzi utakaowasaidia kufanya shughuli zao kwa tija.


Tamasha hilo linahusisha mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Lindi, Katavi, Dodoma, Kagera, Tanga, Mtwara, Kigoma na wenyeji mkoa wa Mbeya.

No comments: