Washiriki wakiwa katika mafunzo hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, Bw. Hiiti Sillo akitoa maelezo ya utangulizi kwa washiriki.
Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto , Dkt. Ulisubisya Mpoki akisisitiza jambo katika hotuba yake ya ufunguzi.
Picha ya pamoja baina ya Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto , Dkt. Ulisubisya Mpoki (wa tatu kushoto, msitari wa mbele), akiwa na waratibu, na washiriki wa mafunzo ya kutathimini kwa ulinganifu ufanisi na usalama wa dawa katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Sekeretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wameshiriki katika uratibu wa mafunzo hayo na kutoa misaada ya hali na mali.
Serikali imesisitiza umuhimu wa mafunzo zaidi kwa wataalamu wa ukaguzi na udhibiti ili kuhakikisha dawa zinazoingizwa na kutengenezwa nchini zina ubora kwa kuzingatia viwango na vigezo vilivyowekwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Ulisubisya Mpoki amesema kuwa moja ya changamoto kubwa zinazozikabili nchi nyingi barani Afrika katika kuwapatia wananchi wake huduma bora za afya ni ukosefu wa wataalamu wa kutosha wa ukaguzi wa dawa hivyo mafunzo ya wataalamu hao hayana budi kupewa kipaumbele.
“Tanzania tunaagiza asilimia themanini ya mahitaji yetu ya dawa na kutengeneza kiasi kilichobaki hivyo suala la weledi katika ukaguzi na udhibiti wa dawa ni jambo linalopaswa kupewa umuhimu mkubwa” Dk. Mpoki alisema.
Katibu Mkuu huyo amesema hayo leo wakati akifungua rasmi mafunzo ya siku tisa ya ulinganishaji wa viwango vya dawa kwa wakaguzi na wataalamu wa udhibiti wa dawa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika kituo Mahsusi cha Kanda cha Ukaguzi na Udhibiti wa Dawa kwa Afrika Mashariki kilichopo Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi ya Afya, Muhimbili.
Kwa hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia kwa makini mafunzo hayo kwa kuwa yatawaongezea uwezo wa kuhakikisha dawa zinazotumiwa wananchi wa nchi zao ni zenye ubora na salama.
“Tumieni fursa ya mafunzo haya kuhakikisha mnapata ujuzi wa kutosha utakaowawezesha kufanya maamuzi sahihi katika kuamua ubora wa dawa katika nchi zenu” Dk. Mpoki alisisitiza.
Aliongeza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu ya kukabiliana na changamoto hiyo na kueleza utayari na dhamira ya Serikali ya kuendelea kukiunga mkono kituo hicho ili kiweze kutimiza majukumu yake.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo amesema lengo la kituo hicho ni kufundisha wataalamu wengi zaidi kutosheleza mahitaji ya nchi wanachama ili kuhakikisha kazi ya ukaguzi na udhibiti wa ubora wa dawa unaimarika katika nchi hizo.
Alifafanua kuwa katika Programu ya Ulinganishi wa Dawa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, TFDA ndio taasisi kiongozi wa kuratibu na kusajili dawa.Aliongeza kuwa uamuzi wa TFDA kupewa dhamana hiyo unatolaka na uwezo wa kitaalamu na miundombinu iliyopo nchini katika kutekeleza jukumu hilo.
Mkurugenzi Mkuu huyo alibainisha kuwa kituo hicho ambacho kilianzsihwa mwaka 2014 na kuanza shughuli zake mwaka 2015 na kinaendeshwa kwa pamoja kati Jumuiya ya Afrika Mashariki, TFDA na Shule ya Phamasi ya Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili.
No comments:
Post a Comment